Rostam Aziz anacheza kama Pele


Nyaronyo Kicheere's picture

Na Nyaronyo Kicheere - Imechapwa 19 October 2011

Printer-friendly version

ROSTAM Aziz, kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliyejiuzulu nyadhifa zake zote katika CCM kwa madai ya kuchoshwa na siasa uchwara, anajua kucheza kama Pele na kupanga mipango na mikakati kama Kanisa Katoliki.

Nimeanza na msemo huo hapo juu kwa kufahamu kwamba tangu dunia imeumbwa, hajatokea mchezaji wa mpira wa miguu aliyevuma zaidi na kufunga mabao mengi kama alivyokuwa Edson Arantes dos Nascimento “Pele”.

Nimeambiwa na wanazi wa mpira wa miguu au soka au kabumbu au gozi au futiboli kama wanavyoita wengi, kuwa Pele, mchezaji mweusi mzaliwa wa Brazil , alifunga zaidi ya mabao 1,500 na kuweka rekodi ambayo haijavunjwa.

Nimeambiwa pia kuwa Pele alicheza fainali za Kombe la Dunia mara tatu katika miaka ya sabini akiwa na magwiji wenzake wa kusakata gozi au kabumbu, kina Garincha.

Na mtu pekee ninayeweza kumlinganisha na Pele hapa nchini lakini yeye katika kutafuta ‘sabuni ya roho’ – kitu pesa; ni mbunge wa zamani wa Igunga, mweka hazina wa zamani CCM na mmiliki wa makampuni zaidi ya kumi nchini, Rostam Abdulrasul Aziz.

Rostam anapotafuta pesa, anapowekeza, anapofuatilia noti, hucheza kama Pele! Akikuacha bega tu, utakuta katengeneza milioni wakati wengine hata ndururu hamjapata. Huyo ndiye Rostam.

Lakini hayo ni tisa, 10 ni jinsi anavyojua kupanga na kupangua, akiweka mikakati ya kupata noti. Katika hili, taasisi pekee tunayoweza kumlinganisha nayo ni Kanisa Katoliki, lile Kanisa alilowahi kuliandikia Paulo Mtume wa Mungu, akiwahubiria Wagalatia, Wakorintho na Warumi.

Hapa sikaribishi ubishi. Angalia mambo yanavyoliendea vizuri Kanisa Katoliki hapa nchini. Na siku zote si kwa kupendelewa, la hasha, ni kutokana na Kanisa hilo kupanga mipango, mikakati na kutabiri mwenendo wa uchumi na utawala wa nchi utakavyokuwa.

Hakuna padiri wala mchungaji kihiyo. Bila digirii nenda kafuge nguruwe, hupati upadiri.

Wewe tazama mambo ya Kanisa Katoliki halafu uamue. Wakati wapagani wanatambika kwenye mapango na mapori ya Nyamongo, Namanyere, Nakapanya na Nyalikungu, Wakatoliki wanajenga makanisa mijini na kuruhusu wote waje kusali misa na rosari takatifu.

Wakati Waislamu wananunua maspika, maikrofoni na kukodi magari ya kubeba wahubiri kuwathibitishia waja wa Mwenyezi Mungu Subhana wa Taala kuwa Yesu yule Mnazareti siyo Mungu, Wakatoliki wao wanajenga Chuo Kikuu na kuruhusu wote waende kupata shahada na stashahada pale.

Wakati waungwana wanapiga kampeni nchi nzima wakitaka serikali iwaanzishie mahakama yao peke yao kwa ajili ya kuwatatulia migogoro ya mirathi, wakfu na mambo ya talaka, wao Wakatoliki wanajenga hospitali ya rufaa na kuruhusu yeyote atakaye aende kutibiwa pale.

Wakati wengine wanalalamikia serikali kwa kutowajengea barabara, wao Wakatoliki wanaomba na kupewa maeneo makubwa ya ardhi mbali na barabara huko maporini kwa ajili ya makanisa yao , shule zao za chekechea, msingi na sekondari; seminari zao na vyuo vyao. Narudia huko maporini!

Hebu jiulize kuna barabara kuu inapita Mbagala Spiritual Centre? Kuna barabara kuu inapita Kurasini Episcopal Centre? Jiulize tu kama kuna mgogoro wa eneo la kanisa barabara kuu za Kilwa, Nyerere, Morogoro, Bagamoyo au Kawawa, Mandela na Sam Nujoma jijini Dar es Salaam ? Nasema Kanisa Katoliki siyo vikanisa!

Hilo ndio Kanisa Katoliki. Kila mwaka wanakutana mara moja wale maaskofu wakubwa wa kanisa hilo na kupanga mipango, mikakati na kutoa maelekezo kwa mapadiri wao. Na mikutano yao hakuna waandishi wa habari na maazimio yao hayatangazwi.

Mtaona tu katika pori fulani wameomba eneo jirani na kijiji, mji au manispaa. Wakilipata eneo hilo wanaanza kujenga kanisa, inafuata zahanati, halafu shule ya watoto wadogo (chekechea), shule ya msingi na shule ya sekondari ambayo inafuatiwa na chuo cha ufundi.

Haujapita muda mnashangaa kijiji, mji au manispaa inakua kuelekea walipo Wakatoliki wale kwa sababu wamewekeza katika vitu vinavyotakiwa na jamii. Mnapozinduka kuwa Yesu awe Mungu au asiwe Mungu ni hoja inayowahusu wanaoamini hivyo, tayari Wakatoliki wamefikisha vyuo vikuu saba.

Mtakapogundua kwamba dini na maamrisho yake yapasa kutekelezwa na wale wanaoifuata dini hiyo na kwamba mahakama ya kidini yapasa kuanzishwa na wafuasi wa dini hiyo mtakuta tayari Wakatoliki wamejenga hospitali 20 au zaidi zinazotumiwa na serikali kama hospitali za wilaya. Ukiugua unataka utakwenda hutaki utapelekwa na nduguzo ukatibiwe huko.

Narudia, mtu pekee nchini anayeweza kucheza kama Pele na kupanga mipango ikapangika na mikakati ikatekelezeka kama Kanisa Katoliki ni mfanyabiashara maarufu Rostam Aziz. Mimi simsifii hivihivi tu. Hebu jaribu kufuatilia mafanikio yake.

Waziri wa sasa wa Nishati na Madini, Mheshimiwa sana , William Ngeleja aliwahi kuwa mwajiriwa wa Rostam. Hapo mwanzo, Ngeleja alikuwa Mkuu wa Kitengo cha Sheria katika kampuni ya Vodacom ambayo mmoja wa wamiliki wake ni Rostam. Upo?

Kabla ya Rostam kuanza kuwekeza kwenye nishati na madini, alimsaidia Ngeleja kugombea ubunge Jimbo la Sengerema na akashinda. Mimi nasema alishawishiwa kugombea na wale waliomhitaji na Ngeleja aliposhinda ubunge akapewa uwaziri wa Nishati na Madini.

Na sasa kampuni ya Richmond/Dowans imeshinda tuzo kwenye mahakama ya kimataifa na inatakiwa kulipwa fidia na Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO). Nasikia ni mabilioni ya shilingi. Lakini kabla pesa hizo hazijalipwa, mkuu wa kitengo cha sheria cha TANESCO aitwaye Subira Wandiba kaondolewa!

Hebu bashiri nani kaletwa kuchukua nafasi yake katika kitengo hicho wakati huu TANESCO ikitakiwa kumlipa mmiliki wa Richmond/Dowans ambaye mimi nimedokezwa na wanoko wa mjini kuwa ni Rostam Aziz?

Ndiyo umebashiri vizuri. Ni Godwin Ngwilini, mwanasheria mwingine kutoka Vodacom, ile kampuni ya Rostam Aziz! Kumbe atoke wapi? Kudadadeki, Mzaramo kalonga au kasema: kalaga baho na ubozi wako!

Ninachokiona hapa ni msomi mtaalamu wa sheria wa Rostam kapelekwa TANESCO ya serikali chini ya mwanasheria mwingine wa Rostam (Ngeleja) kusaidiana kuhakikisha sheria, kanuni na taratibu zinafuatwa kumlipa haraka iwezekanavyo mmiliki wa Richmond/Dowans ambaye ni Rostam.

Tena mengi hapa sikuyasema, nimeambiwa hata wanasheria walioendesha kesi ya Richmond/Dowans hapo zamani walikuwa wapangaji wa Rostam! Nyie mnaona watu wanashinda tu. Mmeula na chuya.

Ni mipango, mikakati na uwezo wa kuona mbali. Cheza kama Pele na panga mipango na mikakati kama Kanisa Katoliki. Usichezee shilingi chooni, usimrudishie mpira golikipa mbele ya adui. Wenye kujua wanachukua viwanja visivyo na migogoro mbali kabisa maporini, faida yake itakuja kujulikana miaka 20 baadaye.

0
Your rating: None Average: 4.5 (8 votes)
Soma zaidi kuhusu: