Rostam Aziz balaa


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 26 May 2009

Printer-friendly version
Anamiliki makampuni kama uyoga
Lakini jina lake halionekani popote
ROSTAM Aziz,  mbunge wa Igunga

ROSTAM Aziz, mbunge wa Igunga, anamiliki makampuni mengi ambamo jina lake halionekani, MwanaHALISI limegundua.

Hata pale anapokiri hadharani kuwa anamiliki kampuni fulani, bado kampuni hiyo haina jina lake kamili la Rostam Abdulrasul Aziz kama linavyofahamika katika kumbukumbu za bunge.

Rostam anatajwa kumiliki makampuni 10 yaliyoanzishwa jijini Dar es Salaam kwa nyakati tofauti, lakini jina lake linaonekana katika kampuni moja tu, kwa mujibu wa fomu za Wakala wa Usajili wa makampuni na Leseni za Biashara (BRELA).

Kampuni ambako jina lake linatajwa ni African Trade Development (T) Limited (ATDL) ambako pia limeongezewa jina jingine “Sakarri” kwenye safu ya majina ya ukoo, ambalo hata hivyo halifahamiki kwa wengi.

Katika ATDL, orodha ya waanzilishi wenye hisa inaonyesha kuna Rostam watano (5) huku jina “Rostam” likiwa ama limekosewa au limebadilishwa herufi kadhaa au wahusika wakiwa na ubini tofauti.

Hata katika ununuzi wa magazeti ya Rai, Mtanzania, The African, Dimba, Bingwa na “chuo” cha uandishi wa habari – MAMET, kutoka kampuni ya Habari Corporation Limited (HCL), hakuna jina lake.

MwanaHALISI linaweza kuripoti kuwa magazeti hayo yaliuzwa kwa kampuni inayoitwa Isenegeja Limited ya Dar es Salaam ambako jina la Rostam halionekani.

Aidha, ni Rostam Aziz aliyekiri mbele ya waandishi wa habari, 3 Mei mwaka huu katika hoteli ya Kilimanjaro Kempinski, kuwa anamiliki magazeti hayo kupitia kampuni ya New Habari Limited ambayo pia bado ni kitendawili.

Siku tatu kabla ya kauli yake kwamba anamiliki kampuni hiyo, gazeti lake la Rai liliripoti kuwa “inasadikika kwamba Rai linamilikiwa na Rostam.”

Kwa mujibu wa barua ya Katibu wa Bodi ya Wakurugenzi ya HCL, Shaaban Kanuwa ya 30 Aprili mwaka huu, bado wamiliki wa sasa wa magazeti hayo hawajayalipia.

Barua hiyo inayoandikwa kwa Isenegeja Company Limited, kupitia New Habari (2006) Limited (NHL), ambayo Rostam Aziz anadai kumiliki, inasema MAMET na magazeti ya Dimba na Bingwa, bado hayajalipiwa.

Kanuwa anasema katika barua hiyo, kwamba wakurugenzi wa HCL wanapendekeza zilipwe mara moja Sh. 100 milioni ambazo walikubaliana wakati wa ununuzi wa kampuni hiyo.

Wakati huohuo, Kanuwa anaelekeza kuwa iwapo Isenegeja haijawa tayari au imeshindwa kulipia magazeti mawili ya Dimba na Bingwa na MAMET, basi iache  kuvitumia, kwa maana ya kuyachapisha na kuendesha chuo.

Habari Corporation iliuzwa miaka mitatu iliyopita. Haijafahamika magazeti ya Rai, Mtanzania na The African yaliuzwa kwa kiasi gani.

Lakini barua ya bodi ya HCL inasema gharama ya magazeti ambayo hayajalipiwa ilikuwa kama ifuatavyo: Dimba Sh.40 milioni, Bingwa Sh. 30 milioni na chuo Sh. 10 milioni na ilitaka kiasi hicho kilipwe ifikapo 29 Mei mwaka huu.

MwanaHALISI haikuweza kufahamu  majengo ya HCL yaliuzwa kwa kiasi gani. Kanuwa alipoulizwa iwapo Isenegeja wamekwishawalipa, alisema swali hilo aulizwe mwenyekiti wa bodi, Jenerali Ulimwengu ambaye imefahamika yuko nje ya nchi na hakuweza kufikiwa.

Uchunguzi wa gazeti hili haukuweza kubaini faili la NHL ambako ulitegemea kukuta jina la Rostam Aziz aliyesema anamiliki kampuni hiyo na magazeti yake.

Lakini miezi miwili iliyopita, kulikuwa na andishi kwenye mtandao wa jamiiforum.com lililokuwa linaenda kwa Rostam Aziz kumtahadharisha kuwa alikuwa anaendesha kampuni ya NHL bila kusajiliwa na bila mwelekeo wowote.

Andishi lililosainiwa kwa jina moja la Salva, halikujulikana iwapo lilikuwa linatoka kwa  mmoja wa wakurugenzi wa HCL na ambaye hivi sasa ni mkurugenzi wa mawasiliano ikulu, Salva Rweyemamu.

Mwandishi alikuwa anaonya juu ya kutozingatia sheria za nchi, kushindwa kuendesha kampuni kwa misingi bora ya menejimenti ambako kulikuwa kunaelekea “kuua kampuni.”

Haijafahamika pia uhusiano wa NHL na Isenegeja, na uhusiano wa Rostam na makampuni yote mawili – NHL na Isenegeja. Waanzilishi na wamiliki wa Isenegeja ni Hassani Haidari na Gulam Abdulrasul wote wa anwani za Dar es Salaam.

Katika umiliki wa kampuni ya African Trade Development (T) Limited (ATDL) ndiko kuna vimbwanga vya majina yanayohusiana na Rostam.

Majina yaliyotumika kusajili kampuni hiyo ni Rostom A. Sakarri, Rostam Sakarri, Rustom Aziz Sakarri, Rustam Sakarri na Rustam Sakaari.

Wanahisa wengine wa kampuni hii waliojiandikisha BRELA, ni Gulam Abdulrasul Chakaar, Bahram Abdulrasul Chakaar na Abdulkadir Mehrab.

Rostam hakupatikana kuthibitisha iwapo Rustam, Rustom, Rostom na Rostam Sakarri yalikuwa majina yake, kulikuwa na jina lake au yalikuwa ya ndugu zake wa karibu. Simu yake ilijibu wakati wote kuwa haipatikani.

Kwenye muhutasari wa kikao cha kampuni ya ATDL cha 17 Machi 1993, kuna saini mbili za Rustam Chakaari (mkurugenzi) na Bahram A Chakaar (mwenyekiti).

Kubadilikabadilika kwa tahajia (spelling) za jina Rostam na mwingiliano wa majina ya ukoo, ni mambo yanayoacha kitendawili kigumu kutegua.

Kwa mfano, siyo rahisi kujua iwapo majina haya yameparanganyishwa kwa makusudi: Rustam Sakarri na Rustam Sakaari.

Mwanasheria aliyezungumza na MwanaHALISI kuhusu utata huu, amesema ni vigumu kumhusisha Rostam na majina hayo matano iwapo kunazuka matatizo ya kisheria kwenye kampuni hizo.

Amesema akihusishwa ataweza “kuruka kihunzi” na kudai hahusiki kwa kuwa nchi nzima, na labda vyeti vyake, kama anavyo, vinaonyesha anafahamika kwa jina la Rostam Abdulrasul Aziz.

Mwanasheria huyo alisema labda mtu wa aina hiyo anaweza kunaswa kwa kutumia ushahidi wa mazingira.

Makampuni ambayo yanatajwa kumilikiwa na Rostam, lakini jina lake halionekani BRELA, ni pamoja na Africa Tanneries Limited, Tanzania Leather Industries Limited na Wembere Hunting Safaris Limited.

Mengine ambako jina lake halionekani ni Tanzania Packages Manufacturers Limited na Caspian Construction Limited ambayo anwani zake zilikuwa zinatumiwa na kampuni tata ya kufua umeme ya Dowans.

Gazeti hili lina orodha ya makampuni ambayo yanadaiwa kuwa ya Rostam, wale wote waliotajwa kuwa waanzilishi na baadhi ya ofisi za makampuni haya ambako inadaiwa alikuwa anakwenda binafsi kuhimiza utendaji au kufuatilia malipo.

Madai ya Rostam kumiliki kampuni zisizo na majina yake yalianza kujitokeza lilipozuka sakata la yeye kuhusishwa na kampuni kadhaa zenye kashfa, zikiwamo Dowans na Kagoda.

Rostam mweyewe alikiri kuwa na uhusiano na Dowans, lakini akadai hamiliki kampuni hiyo isipokuwa anuani na barua pepe za kampuni yake ya Caspian Construction zilikuwa zinatumiwa na kampuni hiyo ya Dowans.

Jina la Rostam linatajwa katika umiliki wa kampuni tata ya Kagoda. Wakili wa Mahakama Kuu, Byidinka Michael Sanze amenukuliwa katika hati yake ya kiapo,  akisema kwamba Rostam ndiye aliyemtaka kushuhudia hati za mikataba ya Kagoda.

Kampuni ya Kagoda ilichota zaidi ya Sh. 40 bilioni katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: