Rostam kinara wa Dowans


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 11 March 2009

Printer-friendly version
Anajuana na Dowans, Kagoda
Serikali yamwangalia tu
Rostam Aziz

MWANASIASA na mfanyabiashara Rostam Aziz ana siri kubwa kuhusu makampuni ya Dowans na Kagoda Agriculture Limited yanayotuhumiwa kwa kuhujumu uchumi.

Dowans ambao imekuwa vigumu kujua makazi ya ofisi zao na maofisa wake wanaowasiliana na serikali, imekuwa kampuni kivuli kama ilivyo Kagoda.

Lakini Rostam Aziz alinukuliwa na vyombo vya habari wiki iliyopita akikiri kuwafahamu wamiliki wa kampuni ya Dowans iliyorithi mkataba wa kufua umeme wa Richmond.

Wakati Rostam anakiri kufahamu wamiliki wa Dowans, kwa madai kwamba aliwahi kuwaomba kazi, taarifa zilizopo zinamtaja mfanyabiashara huyo kuwa na mkono katika mkakati wa kukwapua zaidi ya Sh. 40 bilioni kutoka Benki Kuu (BoT) kwa jina la Kagoda.

Kwa mujibu wa taarifa za Wakala wa Usajili wa Makapuni nchini (BRELA), wenye hisa wote wa Dowans wana anwani za nje ya nchi za Costa Rica na Singapore.

Wenye hisa katika kampuni hiyo ni Dowans Holdings SA ya Avenida de la Rosas 3J; CALLE BLANCOS, 1150 ya San Jose, Costa Rica wenye hisa 81.

Wengine ni Portek Systems wenye hisa 19 na Equipment PTE Ltd., wenye hisa 35 na ambao wanatumia anwani moja ya 20 Harbour Drive, #02 01 PSA VISTA ya Singapore.

Hata hivyo ni Dowans Holdings SA ya Costa Rica ambayo hadi sasa imefahamika kutokuwa na ofisi nchini humo; kutokuwa na gari, simu wala sanduku la barua.

Kukiri kwa Rostam kufahamu wamiliki wa Dowans kunamfanya awe mtu muhimu nchini katika kuchunguza tuhuma zinazokabili kampuni hiyo.

Aidha, mmoja wa wafanyakazi katika kampuni ya Rostam Aziz ya Caspian, anadaiwa kuwa mmoja wa watia saini kwenye hundi za malipo yaliyofanywa kwa kampuni ya Zakhem Contractors Limited ya Mbagala, Dar es Salaam iliyojenga msingi wa kuweka mashine za Richmond/Dowans.

Gazeti hili liliwahi kuchapisha kivuli cha moja ya hundi mbili zilizolipwa kwa Zakhem kupitia EuroAfrica Bank (sasa BOA Bank) ambako, hata hivyo, zilirejeshwa bila kulipwa kwa maelezo kuwa akaunti haikuwa na fedha.

Ni Rostam huyohuyo ambaye imethibitika kuwa mmoja wa wafanyakazi wake, John Kyomuhendo, alikuwa mmoja wa waanzilishi wa kampuni ya Kagoda ambayo ilichota mabilioni ya shilingi kutoka BoT.

Namba ya kiwanja na kitalu, Na 87 katika eneo la viwanda Kipawa (Industrial Area) zilizotajwa kuwa makazi ya Kagoda, hazipo kwenye ramani ya jiji.

Wiki mbili zilizopita, wakili Bhyidinka Michael Sanze alinukuliwa na gazeti hili, katika andishi maalum kwa Kamati ya Rais kuhusu wizi kwenye akaunti ya madeni ya nje (EPA), akimtaja Rostam kuwa mtu muhimu katika ukwapuaji wa mabilioni benki.

Sanze alieleza kwa maandishi kuwa aliitwa na Rostam katika ofisi yake iliyoko Mirambo 50 jijini Dar es Salaam, ambako aliambiwa na wakili wake kiongozi, Bered Malegesi kusaini mkataba wa Kagoda wa kuchota mabilioni ya shilingi kutoka BoT.

Kwa mujibu wa Sanze, katika ofisi ya Rostam alikuwemo pia Peter Noni ambaye hivi sasa ni Mkurugenzi wa Mipango Kimkakati wa BoT na shahidi wa serikali katika kesi za ufisadi.

Alisema Rostam alimweleza kuwa ni rais mstaafu Benjamin Mkapa aliyeagiza fedha hizo zichotwe na kukabidhiwa kwake (Rostam) kwa ajili ya kusaidia CCM katika uchaguzi mkuu wa 2005.

Tangu kutangazwa kwa taarifa hizo, si Rostam wala yeyote aliyetajwa katika andishi la Sanze amejitokeza kukana.

Kwa ushahidi uliopo, na kwa kuzingatia kukiri kwake, Rostam ana uhusiano wa karibu na Dowans, Richmond na Kagoda, makampuni ambayo wananchi wanalia nayo kuhusu ufukarishaji wa nchi.

Vilevile Rostam anatajwa kuwa mfuatiliaji mkuu wa malipo ya Richmond/Dowans kutoka Hazina na BoT kila alipoona malipo yanacheleweshwa.

Bali hakuna ushahidi wowote kuhusu juhudi za serikali kutumia mtu huyu, mwenye ukaribu na makampuni haya ya kifisadi, kuchunguza na hata kurejesha asilimia ndogo tu ya fedha zilizoibwa.

Kwa wiki nzima, gazeti limekuwa likimtafuta Rostam kupata kauli yake, lakini simu yake ya mkononi, Na. 0754 555555 imekuwa ikijibu kuwa hapatikani. Hata ujumbe wa maandishi uliopelekwa kwake haukujibiwa ingawa ulionyesha kuwa ulipokelewa.

“Huo ndio umaarufu wa Rostam; biashara zake zenyewe hazionekani lakini yuko kila mahali penye shina la fedha,” ameeleza mmoja wa wafanyabiashara wakubwa jijini Dar es Salaam.

Kutoonekana kwa Rostam katika maandishi kuhusu umiliki wa makampuni ya Kagoda, Richmond na Dowans, kumeelezwa kuwa siyo jambo la bahati mbaya kwake.

Rostam Aziz haonekani hata katika New Habari Group iliyonunua kampuni ya Habari Corporation, wachapishaji wa magazeti ya Rai, Dimba, Mtanzania, Bingwa na The African.

Lakini ni Rostam anayetajwa na kufahamika kuwa mmiliki wa kampuni hiyo; mwenye mamlaka ya kuteua na kuajiri menejimenti; kuajiri na kulipa wafanyakazi.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: