Rostam ndiye Dowans


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 12 January 2011

Printer-friendly version
Rostam  Aziz

MJUMBE wa Kamati Kuu (CC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na mbunge wa Igunga, Rostam Aziz ni moja ya nguzo kuu ndani ya kampuni ya kufua umeme ya Dowans, imefahamika.

Kwa maana hiyo, Rostam atakuwa mmoja wa watakaofaidika na mabilioni ya shilingi pale serikali itakapokubali kulipa Dowans Sh. 94 bilioni kwa kile kinachoitwa fidia za kuvunja mkataba.

Taarifa zilizopo zinaonyesha kuwa, hata kabla ya Dowans Holdings SA (Costa Rica) kuwepo – kwani usajili wake una utata mkubwa – tayari Rostam alikuwa “amepewa” nguvu ya kisheria (Powers of Attorney) ya kusimamia shughuli za kampuni hiyo.

Nyaraka za Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICC), zinaonyesha kuwa Rostam alipewa mamlaka hiyo 28 Novemba 2005.

Bali kampuni ya Dowans Holdings SA (Costa Rica) inadaiwa kusajiliwa Februari 2007, miaka miwili baada ya Rostam kupewa mamlaka ya kisheria ya kuiwakilisha.

Haikufahamika Rostam alikuwaje na mamlaka hiyo kabla kampuni haijaundwa; na bado uundaji na usajili wake haujathibitika kuwa halali.

Ofisi ya msajili wa makampuni nchini Costa Rica, alimwandikia Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Tanzania, 3 Agosti 2008 akieleza kuwa Dowans Holdings SA haimo kwenye orodha ya makampuni ya nchi hiyo. Barua hiyo ilisainiwa na Marianela Jimenez.

Aidha, taarifa zinasema wakati Rostam anakabidhiwa nguvu hiyo ya kisheria, mkataba kati ya Shirika la umeme la Taifa (TANESCO) na kampuni ya kufua umeme ya Richmond Development Company (LLC), ulikuwa haujasainiwa.

Mkataba kati ya TANESCO na Richmond ulisainiwa 23 Juni 2006, mwaka mmoja kabla tarehe inayodaiwa Dowans ilisajiliwa na karibu miaka miwili kabla Richmond “kubadilishana” mkataba na Dowans.

Kuibuka kwa taarifa hizi kumekuja wiki moja baada ya gazeti hili kuripoti kuwa Dowans tayari wamewasilisha Hazina, ankara ya madai yake ikitaka serikali kuilipa kinyume cha taratibu.

Tarehe 17 Februari 2008, Rostam alikana kumiliki aina yeyote ya hisa kwenye makampuni matatu – Dowans Tanzania Limited, Dowans Holding SA na Richmond. Alikana pia kufahamu wamiliki wa makampuni hayo.

Bali kutajwa kwake katika shauri hilo kuwa ndiye msimamizi wa Dowans Holdings SA (Costa Rica), kunaweza kuchukuliwa kuwa, ama amekuwa akificha ukweli au akisema uwongo kuhusiana na suala hilo.

Rostam ndiye amekuwa akitajwa pia katika ukwapuaji wa zaidi ya Sh. 40 bilioni kutoka Benki Kuu ya Taifa (BoT) kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) kupitia kampuni ya Kagoda Agriculture Limited. Mara zote amekana.

Kwa mujibu wa nyaraka za ICC, Mwenyekiti wa mahakama hiyo, Gerald Aksen na wasuluhishi wenzake wawili, Jonathan Parker na Swithin Munyantwali, walijiridhisha na kiapo kilichompa Rostam mamlaka ya kusimamia maslahi ya Dowans.

Katika hukumu yake, ICC inasema TANESCO inaamini kuwa Dowans Holdings SA (Costa Rica), ni “taasisi ya, au inasimamiwa na, au ni kitu kinachomhusu Rostam Aziz, mwanasiasa wa Tanzania.”

Kwenye ukurasa wa 121 wa hukumu hiyo, ICC inasema jitihada za TANESCO kupinga uhalali wa Dowans kulipwa mabilioni hayo ya shilingi, zilikosa nguvu kwa kuwa shirika hilo halikukataa kusaini mkataba na Dowans hata hata pale lilipotambua utata wa Richmond.

Wakati hayo yakiibuka, taarifa zinasema Richmond, ambayo haikuwa halali kisheria, haikuwa na uwezo kifedha wala kitaaluma, inasubiri Dowans walipwe ili nayo “ichukue chake.”

Kuna taarifa kuwa wanaoitwa wawakilishi wa Richmond, wanadai kuwa walizalisha umeme wa megawati 20 kabla hawajafungishwa virago.

Wachunguzi wa mambo wanasema kile ambacho Richmond wanasubiri, ni hichohicho ambacho wanasubiri wote waliosaidia kuipa kampuni hiyo mkataba kwa upendeleo.

Taarifa zinasema wawakilishi wa “Richmond hewa” wanataka kuiomba mahakama kuzuia malipo kwa Dowans hadi hapo mahakama itakapolipatia ufumbuzi shauri lao.

Alhamisi iliyopita, Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja alitaja, mbele ya waandishi wa habari, wakurugenzi wa Dowans, huku akishindwa kueleza lolote kuhusu uhusiano wa Rostam na Dowans.

Kushindwa kwa Ngeleja kumtaja Rostam kunatokana na madai kuwa kabla ya kuwa mbunge na waziri, Ngeleja alikuwa mtumishi wa kampuni ya Vodacom ambako Rostam alikuwa mmoja wa wakurugenzi.

Katika hali inayothibitisha umiliki wa kampuni hiyo kugubikwa na utata, Ngeleja alitaja kampuni ya Portek International ya Indonesia kuwa ni miongoni mwa wana hisa ndani ya Dowans Holdings SA (Costa Rica). Alisema inamiliki asilimia 39 ya hisa za kampuni hiyo.

Lakini MwanaHALISI limegundua kampuni ya Portek International haina uhusiano na Dowans Holdings SA.

Bali Portek International iliyotajwa na Ngeleja, ni moja ya makampuni tanzu ya Portek Systems and Instruments ya Singapore chini ya shirika lake la Portek Engineering Holdings Pte, inayomiliki asilimia mia moja ya hisa za Portek International.

Hadi mwaka 2008 kampuni hiyo ya Indonesia haikuwa na hisa yoyote katika Dowans Holdings SA wala haikuonesha kuwa wanaitambua kwa namna yoyote ile.

Portek International ni kampuni inayohusiana na huduma za bandari sehemu mbalimbali duniani. Kwa mujibu wa tovuti yake ya  http://www.portek.com.

Shughuli nyingine zinazofanywa na Portek International iliyoanzishwa mwaka 1988, ni pamoja na kuboresha vifaa na mashine zinazotumika bandarini, kubeba makontena, kukodisha vifaa hivyo kwa makampuni mengine duniani, kuuza vipuri vya mashine na kutoa ushauri wa kitaalam katika kuendesha huduma za bandari.

Kwa muda wa miaka yote hii mitano tangu sakata la Dowans lianze, kampuni ya Portek haijawahi kutajwa au yenyewe kuitaja Dowans Tanzania Limited au Dowans Holdings SA kuwa ni miongoni mwa makampuni yake tanzu.

Zaidi ya yote, katika ripoti za kila mwaka kuanzia 2006, kampuni hiyo haijaonyesha mahali popote kumiliki kampuni ya Dowans Tanzania Limited.

Taarifa zinasema kama kweli Dowans Tanzania Limited, ingekuwa inamilikiwa na kampuni hiyo, basi ni lazima wangeitaja, hasa kutokana na kubanwa na sheria za uuzaji hisa katika soko la hisa la New York, nchini Marekani.

Katika soko la hisa la New York, kampuni ya Portek International inatumia alama ya PORT:SI.

Kutokuonekana kwa kampuni ya Dowans kuwa sehemu ya orodha ya makampuni ya Portek International, kunaacha maswali mengi kwa kauli ya waziri Ngeleja aliyeitaja.

Hata hivyo, imefahamika kuwa kamapuni ya Portek International ina uhusiano wa kibiashara na kampuni ya TICTS ambayo mmoja wa wakurugenzi wake ni Nazir Karamagi.

Kampuni hiyo ndiyo iliyoingiza nchini winchi zinazotumiwa na TICTS ambayo imeingia mkataba wa miaka 25 na serikali wa kupakua na kupakia mizigo katika bandari ya Dar es Salaam.

Taarifa zilizopatikana wakati tunakwenda mtamboni na ambazo hazijathibitishwa, zinasema serikali ya Tanzania iliwahi kutuma ujumbe Costa Rica na Indonesia kutafuta ukweli juu ya Dowans, lakini haikuambulia chochote.

Wasemaji wa wizara ya Fedha, Sheria na Nishati hawakuweza kupatikana kusemea hilo.

0
Your rating: None Average: 3 (2 votes)
Soma zaidi kuhusu: