Rostam taabani


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 15 April 2008

Printer-friendly version
Rostam Aziz

MBUNGE wa Igunga (CCM), Rostam Aziz, ametishia kujiuzulu ubunge kutokana na hatua ya Kamati ya Uongozi ya Bunge kumzuia kuwasilisha hoja yake bungeni, MwanaHALISI limedokezwa.

Taarifa za uhakika kutoka ndani ya Kamati hiyo, zinasema Rostam alitoa tishio hilo mbele ya wajumbe wa Kamati ya Uongozi ambao ni pamoja na Spika wa Bunge, Samwel Sitta na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Inaelezwa kwamba baada ya Rostam kutoa kauli hiyo, Waziri Mkuu na Spika kwa pamoja walimtaka afanye hivyo haraka.

"Kabla Rostam hajamaliza kulalama, Spika hakumkawiza. Alisema, "Andika barua ya kujiuzulu sasa hivi. Hatuwezi kupeleka matusi haya ndani ya Bunge?," alinukuliwa na mjumbe mmoja wa Kamati.

Mjumbe huyo alisema kauli ya Rostam iliwaudhi wajumbe wa Kamati ya Uongozi kwani haraka Waziri Mkuu alitoa tamko la kuungana na Sitta kumtaka Rostam ajiuzulu ubunge.

Wiki iliyopita, Spika alimzuia Rostam kuwasilisha maelezo yake bungeni, baada ya kubaini kuwa aliyoyaeleza katika kile alichoita "hoja yake" hayakustahili kuwasilishwa bungeni.

Katika Mkutano wa Bunge uliopita (wa kumi), Bunge lilimtaka Rostam kuwasilisha maelezo yake katika mkutano unaoendelea sasa mjini Dodoma, baada ya kusikika akituhumu kwamba Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza mkataba wa Richmond, "iliendelea na kazi zake hata baada ya kuwasilisha ripoti yake kwa Spika."

Rostam, kwa mujibu wa taarifa, alitaka Spika, kwa kutumia hoja za Rostam, amwamuru Dk. Mwakyembe kumsafisha ndani ya Bunge.

Hata hivyo, shinikizo lake hilo lilikataliwa na Kamati ya Uongozi.

Taarifa za ndani ya Bunge, zinasema kukataliwa kwa maelezo binafsi ya Rostam kumetokana na kuonekana yamejaa tuhuma, shutuma na dharau kwa Bunge na Kamati Teule ya Mwakyembe.

Spika wa Bunge amekiri kupokea hoja binafsi ya Rostam, lakini alisema ameshindwa kuruhusu iwasilishwe bungeni kutokana na kwenda kinyume na Kanuni za Bunge.

Mjumbe mmoja wa Kamati ya Uongozi amemkariri Spika akisema Bunge halikujadili hoja ya Rostam, siyo kwa kumwogopa, kama baadhi ya magazeti yanavyotaka kuonyesha, bali kwa sababu hoja yenyewe inakiuka Kanuni za Bunge.

Alipopigiwa simu na gazeti hili kupata undani wa taarifa hiyo, Sitta alielekeza mwandishi awasiliane na Rostam mwenyewe ambaye, Spika alisema tayari amejulishwa uamuzi huo.

MwanaHALISI halikuweza kuwasiliana na Rostam kupata upande wake.

Katibu wa wabunge wa CCM, Ali Ameir Mohammed, alipoulizwa juu ya suala hilo alisema, "Sijui kilichojadiliwa. Sifahamu Kamati ya Uongozi ya Wabunge wamesema nini. Sikuwapo Dodoma, na wala sijakutana na mwenyekiti wangu (Waziri Mkuu) wala Rostam."

Hata hivyo, imefahamika kuwa wajumbe wa Kamati Teule, walikuwa wamejiandaa vilivyo kulithibitishia Taifa kuwa Rostam ndiye mwenye Richmond na Dowans.

Uchunguzi wa MwanaHALISI umeonyesha kuwa wajumbe walikuwa wamekamilisha kile kilichoitwa "misumari ya mwisho wa kumpigilia Rostam."

Wiki iliyopita Rostam alimweleza Spika wa Bunge, nia yake ya kutoa maelezo binafsi kuhusu madai ya Kamati Teule kuwa alihusika na njama za kifisadi za kuibeba Richmond.

Taarifa za Bunge zimesema hakukubaliwa kwa mujibu wa Kanuni za 53(8) na 54(4) za Kanuni za Kudumu za Bunge, toleo la 2007 zinazingatia kuwa "Mbunge yeyote hataruhusiwa kufufua jambo lolote ambalo Bunge lilikwisha kuliamua ama katika Mkutano huo au ule uliotangulia ...."

Imefahamika kuwa Rostam, katika hoja iliyokataliwa na Spika, aliwaita wabunge kuwa ni wasanii na wababaishaji kwa sababu tu walimshuku kwenye taarifa yao kuhusika na mkataba wa kifisadi wa Richmond/Dowans.

Uchunguzi wa gazeti hili umethibitisha kuwa Rostam aligawa fedha nyingi kwa baadhi ya wabunge, hasa wa Viti Maalum (majina tunayo), ili wampigie makofi ya nguvu wakati wa kuwasilisha maelezo yake.

Kuna madai pia kuwa "aligawa fedha nzuri" kwa baadhi ya waandishi wa habari (majina tunayo), ili kuipunguza makali Ripoti ya Kamati Teule.

Pamoja na jitihada hizo, bado zaidi ya asilimia 95 ya wabunge wanaiunga mkono Kamati Teule na wangetaka wahusika wote katika kashfa ya Richmond wachukuliwe hatua kali.

"Hawa watu hawajui kusoma mood ya wabunge. Wengi tuna hasira naye; tungemchanachana baada ya kuwasilisha utumbo wake. Sauti za Viti Maalum zingemezwa na sauti za wabunge wazalendo," amesema mbunge kijana na machachari.

Alipoulizwa Dk. Mwakyembe kama kweli Kamati yake ilikuwa na ushahidi wa ziada unaoonesha Rostam ndiye Richmond/Dowans, alisema kwa ufupi, "Tumwombee tu mwenzetu aruhusiwe kutoa dukuduku lake. Tutakayoyasema sisi yatajulikana palepale ulingoni."

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: