Rostam umelisikia hili?


Said Shango's picture

Na Said Shango - Imechapwa 28 April 2009

Printer-friendly version

NOVEMBA mwaka jana Rais Jakaya Kikwete alifanya ziara ya kikazi wilayani Igunga, mkoani Tabora. Katika ziara hiyo, Kikwete alielezwa “kero za wananchi.” Naye akaeleza mengi yanayo husu taifa.

Miongoni mwa kero hizo ni tatizo sugu la daraja la Mto Mbutu. Mwenyekiti wa Kijiji cha Igunga, Komba Kasoma, alilieleza hili japo si kwa upana uliohitajika.

Kwa bahati mbaya siku hiyo alipoulizwa Ofisa wa Wakala wa Barabara (TANROAD) mkoa wa Tabora alishindwa kueleza hili.

Rais akaahidi wananchi wa Igunga, kwamba tumuachie atahakikisha tatizo la daraja na barabara ya Igunga linatatuliwa. Hakuna kilichofanywa.

Tangu mwaka 2006 daraja lilizolewa na maji na kuleta usumbufu mkubwa. Watu wanaotaka kuvuka hulazimika kutoa hadi Sh. 3,000 ili kuvushwa na vijana waogeleaji. Kwa yule anayevushwa akiwa na baiskeli yake, anatozwa hadi Sh. 2,000 zaidi.

Ukosefu wa daraja umechochea mfumko mkubwa wa bei za bidhaa kutokana na hatua ya wafanyabiashara hulazimika kutoa fedha nyingi kulipa wapiga mbizi wanaovusha bidhaa kutokea Igunga mjini kwenda ng’ambo ya pili ya Mbutu.

Mwanamke mmoja aliyekuwa akivuka daraja hili 22 Machi 2009, alianguka na kuvunja mkono.

Novemba mwaka 2007 kwenye kikao cha Kamati ya Maendeleo ya Kata Mbutu, Kaimu Mkurugenzi wa Wilaya, Dk. Tongola alisema tatizo hilo lilikuwa halijulikani mkoani wala ngazi ya taifa.

Kwa makisio yaliyofanywa, zilihitajika Sh. 607 milioni kutengeneza eneo la daraja lakini mapato ya Halmashauri nzima ya Wilaya kwa mwaka hayazidi Sh. 200 milioni.

Mkurugenzi akasema kata za Mbutu, Isakamaliwa, Kining’nila, Mwamashimba na Igurubi hazina uwezo wa kutengeneza daraja.

Mbunge wa Ingunga, Rostam Aziz tangu mwaka 1994 alipokuwa mbunge kwa mara ya kwanza wala hajulikani mahali anapoishi. Ni kawaida ya Rostam kuonekana wakati wa uchaguzi tu. Sitakuwa nadanganya nikisema hajasaidia.

Angekuwa ni mbunge anayefuatilia kero za wapiga kura wake, kwa kushirikiana na madiwani, angemaliza au angalau kupunguza shida hizi.

Maana mbali na kuwa mbunge, Rostam anatajwa kama mfanyabiashara na tajiri mkubwa nchini. Je, kama hayo ni ya kweli, anashindwaje kutumia uwezo wake wa mali na kisiasa kubana viongozi wa serikali wakatengeneza daraja la Mto Mbutu?

Wakati wa uchaguzi, tuliambiwa tumchague Rostam maana ni tajiri. Kwake Sh. 1 bilioni ni kitu kidogo sana. Mpaka sasa bado tunajiuliza alitaka nini kutoa pesa nyingi kwa ajili ya Kanisa mjini Dar es Salaam wakati wapiga kura wake Igunga wana matatizo mengi?

Rais, waziri mkuu aliyefukuzwa, Edward Lowassa aliliona tatizo la daraja hili na kuahidi litajengwa. Alitoa Sh. 60 milioni za utengenezaji wa barabara lilipo daraja. Lakini hatujui pesa zimetumikaje. Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Celina Kombani, aliahidi pia kupatia ufumbuzi, lakini hakuna kilichofanyika.

Hatukusikia daraja hili kuingizwa katika mpango wa bajeti ya Wizara ya Miundombinu mwaka 2008/09. Inawezekana kabisa kwamba ilitokana na madiwani na mbunge wa Igunga kutoguswa na tatizo ikawa sababu.

Mwaka 2006, serikali ilitoa Sh. 10 bilioni kwa ajili ya kutengeneza maeneo ya barabara yaliyoharibika. Tunasikia mkoa wa Tabora ulipata mgao wa Sh. 478 milioni na maelekezo ni kwamba fedha hizo zitumike kwenye sehemu zilizoharibika.

Uko wapi mgao wa Igunga? Yuko wapi Rostam Aziz ambaye amejigamba kwamba ana uwezo wa kuleta maendeleo na kutetea wananchi? Yuko wapi huyo aliyejifanya swahiba wa Rais Jakaya Kikwete ambapo alisema akiguna tu, serikali inatetemeka? Vinginevyo, wana-Igunga “wasije kulaumiwa mwaka 2010.”

Makala imeandikwa na Said John Shango, msomaji wa MwanaHALISI anayeishi Bukama, Kata ya Mbutu, wilayani Igunga. Anapatikana kwa simu namba 0757 007237
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: