Rushwa bungeni ni zaidi ya uhaini


Kondo Tutindaga's picture

Na Kondo Tutindaga - Imechapwa 06 June 2012

Printer-friendly version
Uchambuzi
Mbunge wa Bahi (CCM) Omary Badwell

TAARIFA za Bunge au wabunge kujihusisha na vitendo vya rushwa ni za hatari sana. Kwanza, hata kuzusha tu kuwa wabunge wanapokea rushwa ni hatari isiyovumilika kwa sababu watu wengi wamezoea kuona wabunge wanahonga si kuhongwa.

Kwa hali hiyo, taarifa kuwa Mbunge wa Jimbo la Bahi (CCM) Omary Badwell yuko mikononi mwa TAKUKURU kwa kukutwa akipokea rushwa, zinakatisha tamaa.

Kama angekamatwa kama wengine walivyowahi kukamatwa akitoa rushwa kwa wapiga kura, tungejaribu kuelewa kuwa ni kiwewe cha uchaguzi hata kama haikubaliki.

Lakini, kwa habari zilizopo, Mheshimiwa huyo alikamatwa hotelini, Dar es Salaam, akipokea rushwa ya Sh. 1 milioni kutoka kwa afisa wa serikali.

Sitaki kubuni ni kwa nini Afisa atoe rushwa kwa mbunge, lakini kwa kuwa Mheshimiwa Mbunge ni mjumbe wa kamati inayojadili mahesabu ya Halmashauri, ni wazi rushwa hii ina kazi ya kumfumba macho asione anachotakiwa kuona katika mahesabu hayo.

Sitaki kuingia undani wa suala hili kwa sasa, niishie kusema, tumepitwa na mangapi ya namna hii katika shughuli ya kamati zetu za bunge? Tujadili kidogo.

Kama neno “uhaini” maana yake ni kuangusha serikali, basi kitendo cha mbunge kupokea rushwa ni zaidi ya uhaini. Hii ni kwa sababu, mbunge anayechaguliwa na wananchi anapopokea rushwa ili asifanye kazi yake kwa niaba ya wananchi, haiangushi serikali kama taasisi, bali anawaangusha wananchi.

Wananchi hawa ndio wanaoiunda serikali na kwa hiyo wananchi wako juu ya serikali. Kama kuiangusha serikali iliyo ndogo kwa wananchi kunaitwa uhaini, basi kuwaangusha wananchi walio juu ya serikali, kunahitaji msamiati mwingine ambao kwa sasa hatuna.

Kwamba, wananchi wanamwamini mtu mmoja aende bungeni kuiwajibisha serikali, serikali hiyo inaamua kumhonga na kumpa upofu ili asione, na yeye kwa shibe na upofu wa rushwa hiyo, anakaa kimya maslahi ya wananchi yaangamie. Huu hauwezi kuitwa uhaini.

Juzi juzi tulikuwa na uchaguzi wa wabunge wa Afrika Mashariki katika bunge letu. Tulisikia na kushuhudia viroja vya wabunge kuhongana. Kwamba, wabunge wetu siyo kwamba wanahonga na kuhongwa na wananchi wa kawaida, bali hata wao kwa wao wanahongana ili kugawana madaraka ya kututawala!

Nikiwa Dodoma wakati huo, niliongea na wakubwa wetu wa ofisi za juu zaidi. Maskini! Wote walikuwa wanalalamika na kuomboleza bila kujua wafanyeje. Mkuu wa dola aliishia kusema hatuna la kufanya kwa sababu wote wametoa ila wamezidiana viwango.

Kwa hiyo, Bwana mkubwa na wenzake wanajua na kukubali kuwa wawakilishi wetu tuliowatuma katika bunge la Afrika Mashariki ni watoa rushwa watupu. Kama walikuwa hawajui, sasa nawaambia wazi kuwa, wakuu wa dola yetu wanawaona ni watosa rushwa wakubwa.

Bila rushwa wasingeweza kushinda. Katika dola makini, ingetosha kufuta uchaguzi ule na kuitisha uchaguzi upya kwa misingi mipya. Ingerejesha heshima kidogo katika taifa letu. Lakini wapi? Nani hakuingia kwa rushwa katika nafasi aliyo nayo ndani ya chama chetu na serikali yetu? Kigugumizi cha kushughulikia rushwa kinatoka wapi kama si katika hatia ya kuwa hata wakubwa waliingia kwa rushwa?

Hali hii ya kwamba “wote wameoza” ndiyo itakayomuokoa mbunge wa Bahi, Mheshimiwa Omary Badwell. Hapo alipo, mahabusu au huru, anajutia jambo moja tu: kwamba hakuwa mwangalifu na matokeo yake akakamatwa. Wabunge wenzake watamiminika mahakamani kumpa dhamana na kumpa pole.

Itakuwa ni pole ya kumwona ana bahati mbaya ndiyo maana amekamatwa. Wengine watamchangia fedha ili aweke mwanasheria mzuri. Wote hawa watakuwa hawaumizwi na kitendo chake cha kupokea rushwa, bali kitendo cha TAKUKURU kumkamata.

Hilo ndilo bunge letu. Hatutasikia hoja binafsi bungeni ya kuipongeza TAKUKURU kwa kazi hiyo na wala hatutasikia mwongozo kwa spika kutaka ufafanuzi wa bunge kudhalilishwa na Badwell. 

 La ajabu tunaweza kupata mwongozo wa spika kutaka ufafanuzi wa kwa nini TAKUKURU imeingilia shughuli na uhuru wa bunge kwa kumkamata mbunge akiwa katika shughuli za bunge.

Kwamba, shilingi milioni moja zilikuwa za vocha za kupigia simu lakini mtoaji alimgeuzia kibao Mheshimiwa na kuzibadilisha ziwe za TAKUKURU kwa sababu ya visa binafsi!

Nisemayo hapo juu si mageni. Tuko wapi na sakata la Wikiliki juu ya matamshi ya Edward Hosea, mkurugenzi wa TAKUKURU mbele ya ofisa wa ubalozi wa Marekani, kwamba  taasisi hiyo inakwamishwa na wakubwa katika shughuli zake.

Kwamba hata yeye alikuwa anaona usalama wake uko hatarini kwa kushikilia msimamo wa kuwakamata vigogo! Kwa nini hata pale TAKUKURU ilipojaribu kukamata wanaoitwa vigogo, walikuwa ni wale ambao hawako madarani tena?

Kumbe si rahisi kumkamata mtoaji na mpokeaji wa rushwa ambaye bado yuko madarakani? Hii vita ya rushwa inaangalia uso wa watu.

Hivi sasa makamanda wa TAKUKURU wote wilayani na mikoani ni wajumbe wa kamati za ulinzi na usalama na kwa hiyo wanawajibika kwa wakuu wa wilaya na mikoa. Hii ni sawa na kusema kuwa wakuu wetu wa wilaya na mikoa hawawezi kutoa wala kupokea rushwa na wakifanya hivyo hawawezi kukamatwa?

Kwa hiyo tutaachaje kuamini kuwa hivi sasa inaandaliwa hati ya kuachiwa huru kwa Mbunge Badwell kwa kuwa kuendelea kumshikilia ni kuliaibisha bunge na serikali?

Liko wapi sakata la David Jairo? Jairo alituhumiwa kuidhinisha fedha kwa ajili ya “kuwahonga” wabunge wapitishe bajeti ya wizara ya nishati na madini mwaka jana. Baada ya mshike mshike kati ya bunge na serikali, hatimaye Jairo alisimamishwa kazi na kuchunguzwa.

Ripoti yake ilisomwa bungeni na kumkuta ana hatia. Ikafuata danadana kati ya serikali na bunge ambayo mpaka ninapoandika makala hii, hata spika mwenyewe hajui afanye nini nayo.

Hapa tunazungumzia suala la wabunge kuhongwa hata kama fedha yenyewe ilibatizwa jina la posho, uwezeshwaji, au hata “miwani ya kusoma” bajeti ya wizara ya nishati. Kimsingi, kumtia hatiani Jairo ni kuwatia hatiani wabunge wote wakiongozwa na Waziri Mkuu na Spika maana umma uliona sahihi za waheshimiwa hawa katika orodha ya waliopokea fedha hizo. Mpaka hapa nani anabisha kuwa bunge alihongi wala halihongwi?

Nimekuwa ninapokea taarifa mbalimbali kuhusu tabia ya kamati za bunge kuwa wajumbe wake na wenyeviti wao, ama wanadai rushwa au wanawajengea watendaji wa serikali na mashirika mazingira ya kuwapa rushwa. Nimesikia kuwa kamati inaongoza kwa tabia hii, ni hii anamotoka Mheshimiwa mbunge wa Bahi Omary Badwell.

Kwamba, mawakala wanatangulia katika Halmashauri husika kuwaandaa wakurugenzi na kuwafundisha namna ya kumwingia Mwenyekiti wa Kamati. Na kwamba kiasi cha mwenyekiti wa Kamati kinajulikana, hakina ubishi.

Na kwamba, kiasi hicho hakiwekwi benki bali hutangulizwa hotelini. Na kwamba, akiishawekwa sawa Mwenyekiti, ni juu ya wajumbe wa kamati kujijua watakavypata cha kwao na atakayechelewa mawindoni, basi mguu wake utakatwa. Yawezekana, Mheshimiwa Badwell alichelewa, akakamatwa na hiyo haina maana kuwa alikuwa peke yake.

Watoa habari wanadai, ukarimu wa halmashauri husika kwa kamati unaamuliwa na muda unaotumika katika kujadili halmashauri hiyo. Kama hutaki halmashauri yako ijadiliwe sana, toa nyingi. Ukiwa na mkono wa bikira, utachambuliwa kama karanga. Tungekuwa na mwadilifu mmoja aliyebaki bungeni na serikalini, kwa ushahidi huu wa Badwell, ilitosha kubatilisha ripoti zote za kamati.

tutikondo@yahoo.com
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: