Sababu 51 kwanini Kikwete asigombee tena


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 27 January 2010

Printer-friendly version
Kisima cha Mjadala
Rais Jakaya Kikwete

TUNAENDELEA na mjadala wetu wa sababu 51 za kumfanya Kikwete asigombee tena urais.

Nchi yetu inakabiliwa na mgogoro wa uongozi. Ili tupate viongozi wanaofaa, mgogoro huu ni wa lazima. Na mgogoro huu wa sasa unatulazimisha kufanya mabadiliko. Kama Chama Cha Mapinduzi (CCM) kingekuwa kinasoma alama za nyakati, kingetutangulia kabisa kumzuia Rais Kikwete kugombea, kwa sababu zile zile 30 tulizokwishakujadili, na nyingine 21 zinazofuata.

20: Kama tulivyoona huko nyuma majukumu makubwa mawili ya msingi ambayo yameanishwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM yameshindwa kutekelezeka. Rais Kikwete akielezea majukumu hayo alisema hivi katika hotuba yake ya kwanza Bungeni mwaka 2005:

“Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2005 imetamka bayana majukumu mawili ya msingi ya Serikali ya Awamu ya Nne:. Kwanza, kuitoa Tanzania kutoka kwenye dimbwi la uchumi ulio nyuma na tegemezi na kuiingiza katika mkondo wa uchumi wa kisasa wa taifa linalojitegemea. Pili, kuwashirikisha wananchi wote kwa njia ya uwezeshaji katika ujenzi wa uchumi na kuutokomeza umaskini.”

Tunaweza kuona kuwa misingi hiyo miwili imeshindwa kwa kiasi cha kutisha. Uchumi wa Tanzania ndani ya miaka minne iliyopita umekuwa tegemezi zaidi kuliko wakati wowote wa historia yetu.

Imefikia mahali yeye mwenyewe Rais Kikwete alitutangazia kuwa bila misaada ya wafadhili hatuwezi kuendelea! Hii ni kinyume kabisa cha dhamira ya Ilani ya Uchaguzi iliyomuingiza madarakani. Zaidi ya hayo, “wananchi wote” hawashirikishwi katika uchumi huu kama alivyoahidi.

19: Alitoa ahadi nyingine: “Serikali ya Awamu ya Nne itatimiza ipasavyo wajibu wake wa utawala na maendeleo, na itaendesha dola kwa misingi ya utawala bora na uwajibikaji; utawala wa sheria unaoheshimu na kulinda haki za binadamu; itaendeleza mapambano dhidi ya rushwa bila ya woga wala kuoneana muhali.”

Kwa baadhi ya mashabiki wake Rais Kikwete amekuwa akiheshimu mgawanyo wa madaraka na utawala wa sheria. Hata hivyo, ushahidi uliopo mbele yetu haukanishiki. Rais Kikwete amekuwa akiingilia michakato ya utafutaji na upatikanaji wa haki kiasi cha kutishia uhuru wa vyombo vingine vya serikali. Hapa yatosha kutoa mifano miwili mikubwa kati ya mingi iliyopo.

Baada ya matukio ya mauaji ya Wafanyabiashara kutoka Morogoro ambayo yalichangia hatimaye kufikishwa mahakamani kwa Kamanda Abdallah Zombe, Rais Kikwete hakuacha vyombo vya sheria kufanya kazi zake katika kushughulikia uhalifu.

Aliamua kuunda tume ambayo matokeo ya kazi yake yakatumika vile vile kuleta mashtaka dhidi ya Zombe na wenzake. Wengine tulipinga kwa Rais kuingiila masuala ya upatikanaji haki hata kama ni kwa nia njema.

Tuliona hatari ya Ikulu kuanza kuamua nani achunguzwe kwenye masuala ya kihalifu bila kufuata mkondo wa sheria. Matokeo yake tunayajua, kesi dhidi ya Zombe iliporomoka kirahisi kama ukingo wa biskuti uliomwagiwa maji. Kwa sababu ya Rais Kikwete, kesi ya zombe ilifunguliwa kisiasa, na matokeo yake tumeyaona.

Baada ya matukio ya ufisadi mkubwa kabisa kutoka na kuhusisha Benki Kuu katika bara la Afrika na yawezekana Rais Kikwete hakuacha vyombo vya dola vifanye kazi yake na mkondo wa sheria ufuate; akaamua kuunda chombo nje ya vile vya kisheria na kuwapa maagizo ya kufanya uchunguzi huku akiwa kama Jaji akihukumu matukio yake kuwa ni ya “kihalifu.”

Matokeo yake ni kuletwa kwa kesi dhaifu sana katika mahakama zetu huku matokeo ya kesi hizo yakitabirika kwa urahisi. Kwa maneno mengine inaonekana Rais Kikwete mwenyewe hana imani na uwezo wa vyombo vyetu vya sheria kufanya kazi zake bila kuingiliwa au kuagizwa na Ikulu.

Kama Mwanasheria Mkuu na Mwendesha Mashtaka Mkuu hawawezi kuanzisha uchunguzi wao wenyewe wa jambo linalohusu uhalifu hadi waitwe Ikulu na kupewa maelekezo, kimsingi tunakiri kuwa vyombo hivyo haviwezi kusimamia utawala wa sheria na matokeo yake ni kutekeleza maagizo ya Ikulu.

18: Rais Kikwete aliahidi: “Serikali ya Awamu ya Nne itaimarisha uwezo wake wa kulinda maisha na mali za raia wake. Tutapambana na uhalifu wa kila aina, na majambazi hayataachwa yatambe yatakavyo.”

Leo hii sijui kama tunaweza kuwaambia wananchi wa Ukerewe kuwa ahadi hii imetimizwa ipasavyo. Tumeshuhudia mauaji ya Albino, mauaji ya vikongwe (ambayo wengi hatuyasikii na ni wengi wameuawa kuliko maalbino) n.k

Matokeo yake utawala wake nusura uhalalishe “sheria mkononi” baada ya kuona unazidiwa nguvu. Na kama sisi wengine nao tungedandia ajenda yao ya “jino kwa jino,” taifa letu lingekuwa na utawala wa kufanyiziana.

17: Katika kushughulikia suala la Muungano na kuulinda Rais Kikwete aliahidi mambo manne yafuatayo:

“Tutakuwa makini na wepesi katika kushughulikia matatizo ya Muungano. Tutayazungumza kwa uwazi na kuchukua hatua muafaka kwa wakati muafaka; Pili, nitampunguzia Makamu wa Rais majukumu ya kuondoa umaskini ili apate muda wa kutosha wa kushughulikia masuala ya Muungano.

Tatu, nitaimarisha taratibu zilizoanzishwa na Serikali zilizopita za kujadili, kuainisha na kutatua matatizo ya Muungano; nk (na) Nne, nitaangalia upya mchango wa Serikali ya Muungano katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya Zanzibar, bila kuathiri haki na mamlaka kamili ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mambo ambayo si ya Muungano.”

Natamani ningeweza kuandika makala za kutosha juu ya hizi ahadi nne tu. Itoshe kusema kuwa serikali ya Rais Kikwete haijawa mwepesi wala makini katika kushughulikia matatizo ya muungano. wamekuwa goi goi sana.

Hadi sasa kuna hali tete visiwani Zanzibar baada ya Seif na Karume kuamua kumzunguka Rais Kikwete na kujiamulia mambo yao.

Makamu wa Rais hajatumia muda wake wa kutosha kushughulia matatizo ya Muungano kama ambavyo ingetarajiwa. Wakati bara inapopata matatizo ya umeme juhudi nzito zinafanywa kuhakikisha yanatatuliwa. Leo hii Visiwani Zanzibar wanapata adha ya umeme bila kujua Serikali ya Muungano inatoa msaada gani wa haraka wa kupunguza adha hiyo mara moja.

Tutawaachia wachambuzi wengine waangalia kwa kina mchango wa Serikali ya Muungano kwa ustawi wa watu wa Zanzibar.

16: Katika suala la Rushwa, Rais Kikwete aliahidi pepo! Sehemu mojawapo ya ahadi zake alisema hivi, “Katika harakati za kupambana na rushwa yapo mambo mawili mengine ambayo tutayaangalia kwa karibu. La kwanza ni mikataba. Tutaangalia upya taratibu za mikataba mbalimbali inayoingiwa na Serikali, mashirika ya umma na idara zinazojitegemea kwa nia ya kuongeza uwazi na uwajibikaji. Mikataba ni mwanya mkubwa wa rushwa hasa zile kubwa kubwa za wanaotafuta utajiri...Hatuna budi kuchukua hatua thabiti za kuzuia watumishi wa umma kutumia nafasi zao kujitajirisha na kujilimbikizia mali...”

Rais Kikwete anaweza kuonyesha kuwa yeye hajatumia nafasi yake ya miaka hii minne kujilimbikizia mali; je anaweza kuonyesha kwa mfano orodha ya mali zake (iliyo kwa jina lake, mke wake, watoto wake na ndugu zake wa karibu)?

Na kuelezea jinsi walivyozipata. Na akifanya hivyo yuko tayari kutaka Mawaziri wake wote kufanya hivyo hivyo? Japo Waziri Mkuu Mizengo Pinda ametuelezea “umaskini” alionao kwa hakika hakwenda mbali zaidi kwani hajafungua mlango wa utajiri wake wote kwa jina lake, mkewe, watoto na wale ambao kwa mujibu washeria maadili ya umma wanapaswa kutajwa?

Hivi tunaweza kusema kuwa viongozi wa awamu ya nne hawajajilimbikizia mali na kutumia nafasi zao kujinufaisha? Tumesahau jinsi gani maskini mmoja alivyokuzishwa kazi siku chache zilizopita kwa sababu ya kugongana maneneno na Waziri. Kisa, ATM?

Tutamalizia sababu za mwisho wiki ijayo.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: