Sababu 51 za Rais Kikwete kutogombea


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 10 February 2010

Printer-friendly version
Ametanguliza maslahi ya marafiki kuliko ya taifa
Rais Jakaya Kikwete

07: KATIKA miaka minne ya utawala wake, tayari Rais Jakaya Kikwete ameonyesha mfano mbaya katika kusimamia wasaidizi wake. Mara kadhaa watu wamekuwa wakituhumu wasaidizi wa Kikwete, kwamba ndiyo chanzo cha serikali kuboronga.

Lakini muda si mrefu wapiga debe wake watahubiri, “Kikwete anayo nia bali anaangushwa na watendaji wake.” Watasema ana dhamira njema lakini mafisadi ndio wanamuangusha.

Kwamba akiruhusiwa kugombea tena na tukampa nafasi, nia yake hiyo itakuwa vitendo. Hata hivyo, sote tunajua kuwa ng’ombe hanenepei mnanadani.

Kwa miaka minne Kikwete ameshindwa kufukuza au kuwajibisha hata msaidizi wake mmoja kwa uzembe. Ni makosa kufikiri kuwa akichaguliwa kwa mara ya pili atafunguka.

06: Rais Kikwete si kiongozi mwenye maono. Tanzania inahitaji kiongozi mwenye maono makubwa na ambaye yuko tayari kutushawishi kama taifa tukubali maono hayo ambayo yatatupeleka mbele. Kikwete si wa viwango hivyo.

Ameahidi kujenga barabara za juu kwenye jiji la Dar es Salaam, treni ziendazo kasi huku taifa likiwa linakabiliwa na tatizo sugu la umeme ambao unahitajika kusukuma treni hizo.

Bado kuna kipindupindu Dar, bado kuna tatizo la maji, bado kuna matatizo ya shule, mashimo ya takataka, usafi na barabara za kawaida zikiwa zimesheni mashimo hadi kuweza kupandwa miti! Yaani katika mambo yale ya msingi ambayo tunahita kufanya hatutaki kufanya na badala yake tunataka mabarabara yanayokwenda juu kwa juu.

Kama haya ni mambo mazuri kwanini wasiamue kuchimba handaki ya treni zinazokwenda chini kwa chini ili kuondoa msongamano? Kwanini wasiamue kupiga barabara zote lami zikiwamo zile za mitaa na kuweka barabara za kuongozea magari karibu kila kona?

Msongomano wa magari Dar es Salaam hautokani hasa na wingi wa magari kama wengi wanavyotaka tuamini, bali unatokana na mipango mibovu ya ujenzi wa nyumba na barabara, usimamizi mbaya wa sheria za barabarani, na zaidi ya yote ufinyu na uchache wa barabara za kawaida.

Kama mnafikiri barabara za juu kwa juu zitatua matatizo ya msongamano subirini; kama hatujajikuta mnasongamana juu kwa juu na kulazimika kutafuta barabara za chini kwa nini!

Unapokuwa na kiongozi anayefikiria kujenga barabara za juu kwa juu, meli na mitumbwi iendayo kasi – vitu ambavyo anavishangaa anapotembelea nchi zilizoendelea - huku umeme ukiwa haujafakia hata robo ya watu wetu, maji safi bado ni tatizo, ujue hapo kuna tatizo.

Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alisema, “kabla ya wachache wetu hawajaishi katika anasa, wengi wetu ni lazima kwanza wapate mahitaji yao muhimu.”

Hii ina maana ya kwamba badala ya Nyerere kufikiria wachache serikalini kupata televisheni, aliona muhimu kwa wengi kupata redio. Kabla ya wachache kuanza kuendesha magari ya kifahari ya serikali, aliona ni bora kwanza kuwa na mabasi ya Kamata, UDA na reli ya Tazara.

Lakini sasa ni kinyume chake. Chini ya utawala wa Kikwete, serikali inataka kuwahakikishia watu wachache maisha ya anasa kama yale ya New York na Tokyo wakati mamilioni ya wananchi bado wanaishi kwa mlo mmoja kwa siku au wengine wanalala na njaa.

Ndiyo maana serikali imetenga Sh. 7 bilioni kwa ajili ya kombe la dunia, halafu wanaomba Sh. 10 bilioni kujenga miundo mbinu katika wilaya ya Kilosa ambayo imeharibiwa na mafuriko! Huu si uongozi; ni kuburuzana.

05: Hana uwezo wa kuchochea mwamko wa kitaifa. Naomba nikiri kwamba miongoni mwa watu ambao awali waliamini kuwa Rais Kikwete angechochea mwamko mpya wa ujenzi wa taifa nami nimo. Niliamini mvuto aliokuwa nao kabla ya uchaguzi wa mwaka 2005 na mwitikio wa wananchi waliomchagua ungemfanya aamue kutumia mtaji huo wa kisiasa kuchochea mwamko mpya kwa wananchi. Nilikosea!

Miaka mitano imepita kwa aibu. Ameshindwa kuchochea taifa katika ujenzi wa taifa la kisasa. Ameshindwa hata kuchochea viongozi wenzake kuamsha mwamko mpya wa taifa na sasa kila mmoja anajiendea kivyake.

Kuna watu wanafikiria kuwa Kikwete ambaye ameshindwa hata kusimama kupaka rangi shule, akipewa miaka mingine mitano ndiyo ataanzisha mwamko mpya wa taifa.

Inavyoonekana tukimrudisha tena, atakuwa bilionea wa kutupwa kama Benjamin Mkapa; huku akijikabidhi yeye na wanawe urithi wa taifa.

04: Ameweka mbele maslahi ya marafiki zake kuliko taifa. Ameonyesha kuwa yeye ni kiongozi dhaifu zaidi kwa kuogopa kuudhi rafiki na baadhi ya watu wake wa karibu. Hata tukimpa miaka mingine mitano haitakuwa tofauti.

03: Si kiongozi wa matokeo bali wa mchakato. Mojawapo ya udhaifu mkubwa wa Rais Kikwete kama kiongozi ni kuwa anapenda au anaamini sana katika mchakato kuliko matokeo.

Kiongozi ambaye tunamhitaji si yule anayetuambia na kusimamia michakato, bali ni yule anayeweza kuonyesha matokeo ambayo yanaendana na uwekezaji wa nguvu kazi katika elimu na raslimali zetu.

Tanzania tunazo raslimali za kutosha, kinachotakiwa ni ubunifu na kuamua kwa dhati kukitekeleza kile tunachotaka. Tunaweza kuziondoa familia 2.5 milioni katika lindi la umaskini.”

02: Anaongoza pasipo mwelekeo. Hivi kuna mtu yeyote anaweza kusema kwa uhakika kuwa miaka hii minne iliyopita Kikwete amekuwa akiliongoza taifa kuelekea wapi?

Ukiangalia sana taifa ambalo Kikwete analifikiria ni taifa ambalo linategemea wafadhili, taifa ambalo raslimali zake zinachukuliwa na wageni, na ambalo wananchi wake wanaendelea kuwa tegemezi.

Ni kutokana na ukweli huu si yeye wala wasaidizi wake wanaoimba tena kauli mbiu ya “Maisha bora kwa kila Mtanzania yanawezekana.” Ninaposema hawana mwelekeo ni zaidi ya kukosa maono tu ni kwamba sera wanazozitekeleza hazielekezi kwenye maono waliyonayo.

01: Hana uwezo wa kuongoza kufikia suluhisho la matatizo ya taifa letu, na uongozi ni uwezo, wala si umri au elimu, au jina ama uzuri wa sura.

Yeye ana uwezo wa kutawala, ana uwezo wa kufurahisha, ana uwezo wa kuvutia watu na mashabiki, ana uwezo wa kuzungumza maneno matamu na ahadi za pepo, lakini linapokuja kwenye kuongoza, nasikitika sana kusema kuwa hana uwezo wa kuongoza.

Sasa hili si tusi au kejeli au dharau bali ni kukiri kitu kilicho dhahiri. Uwezo huu hauji kwa kupigiwa saluti au kupigiwa mizinga; uwezo huu hauji kwa kushangiliwa na kuimbiwa nyimbo; uwezo huu hauji kwa sababu Yusuph Makamba anasema “Kikwete ni mtaji wa ushindi.”

Mwenyezi Mungu katupa uwezo wa kuona, kufikiri, kuamua na kutenda. Tumeona miaka minne iliyopita; tumeweza kuchangamsha fikra mpya katika jamii, sasa historia inatuita tuamue. Na uamuzi huo unapaswa kuoneshwa katika vitendo.

Binafsi namshukuru rais Kikwete kwa kujaribu kuongoza; namshukuru kwa nafasi zote ambazo amatumia kwa kadiri ya uwezo wake wote kuonesha kuwa yuko makini na anauwezo.

Lakini nasema miaka mitano inatosha. Tanzania haistahili miaka mingine ya uongozi ule ule wenye fikra zile zile na wenye ahadi zile zile, maana tutapata matokeo yale yale. Tunataka matokeo tofauti na ili tuyapate ni lazima tuwe na uongozi tofauti.

Asante rais Kikwete kwa kulitumikia taifa kwa kadiri ya uwezo wako wote. Kwaheri Kikwete.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: