Sababu 51 za Rais Kikwete kutogombea


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 03 February 2010

Printer-friendly version
Kisima cha Mjadala
Anatoa taarifa zisizo sahihi
Rais Jakaya Kikwete

Mtindo wa uongozi wa Rais Jakaya Kikwete hautufai. Na Rais Kikwete hawezi kubadilika, maana hii ndiyo hulka yake, na ndiyo maana naendelea kusisitiza kuwa hastahili kugombea tena mwaka huu, kwa sababu zifuatazo:

15: Rais Kikwete si mwepesi wa kuchukua hatua. Kuna mambo mengine yanapotokea nchini hayahitaji kupigiwa kura, kufanya mijadala ya usiku kucha au kutafuta mtu wa kupiga ramli ya kisiasa. Unahitajika uamuzi wa haraka na wa maramoja.

Ipo mifano mingi katika miaka hii minne iliyopita inayoonyesha udhaifu huu wa kiuongozi. Mara baada ya kashfa za Benki Kuu ya Taifa (BoT) kuanza kufumuka, uamuzi wa haraka wa kurudisha imani kwa taasisi hiyo ulitakiwa ufanyike.

Lakini ilichukua karibu miaka miwili kwa Rais Kikwete kuamua kuunda tume kufuatilia suala hilo na miezi mingine mingi ya uchunguzi huo na hatimaye kuanza kazi. Leo hii miaka minne baadaye, hakuna kesi hata moja iliyofikia hatua ya kwanza ya maamuzi.

Matokeo yake tukijumlisha siku ambazo baadhi ya kesi zitafikia tamati na tukija kuweka muda wa rufaa (ambao kwa hakika utakuwepo) kesi hizi zitachukua miaka kama 10. Haya ni matokeo ya rais kushindwa kuchukua hatua haraka.

14: Rais Kikwete ameshindwa kusimama matumizi ya fedha za umma kama alivyokuwa ameahidi. Mtangulizi wake, Rais Mstaafu Benjamin Mkapa aliongoza serikali iliyoongeza mapato ya serikali mara tano sambamba na kuweka mfumo mpya na wa kisasa wa kudhibiti matumizi. Aliongeza pia uwazi katika bajeti ya serikali.

Tunapoangalia matumizi ya serikali kwenye ujenzi wa paradiso ya gavana na manaibu wake tunaweza kusema kwa kipimo chochote kuwa rais ameshindwa kusimamia vema mapato ya fedha za umma. Kikwete yuko tayari kutumia bilioni saba kwenye “kombe la dunia,” lakini hayuko tayari kuwekeza katika maeneo muhimu kama vile Shirika la Ndege la Taifa (ATC), Reli na kwingineko.

13: Wakati baadhi ya matukio yanahitaji uamuzi na hatua za jumla, thabiti na zisizo na kukopesha, Rais Kikwete amekuwa akiyakabili matukio hayo kwa uamuzi wa vipande vipande.

Mifano michache ni wizi katika Akaunti ya wa EPA ambapo ni sehemu kidogo tu ya ufisadi ndani ya BoT. Suala hilo lilimegwa megwa kiasi kwamba haki yenyewe si tu haionekani kutendeka bali kimsingi haiwezi kutendeka.

Inawezekana vipi kwenye suala moja wapo watu wanafikishwa mahakamani na wengine hawafikishwi mahakamani? Inakuwaje kwenye suala hilo hilo moja kuna watu wanakamatika na wengine “hawakamatiki,” au wakikakamatwa “taifa litalipuka?”

12: Anaacha wasaidizi wake kubeba lawama, yeye ananawa mikono. Kiongozi ni lazima awe tayari kubeba lawama za makosa ya wasaidizi wake. Mojawapo ya mambo ambayo hadi leo hii ninaamini yalifanyika kwa haki kabisa ni kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa na mawaziri wengine kutokana na kashfa ya Richmond.

Karibu wote hawakukubali kuwa wamekosea na hakuna hata mmojawapo aliyekubali makosa yake. Badala yake wanatoa sababu za kipuuzi – kuwajibika kisiasa. Katika yote yaliyotokea hadi leo hii Rais Kikwete hajakubali au kubeba lawama hata moja na kusema kuwa yeye amekosea.

Nitawapa kielelezo. Baada ya jaribio la kulipua ndege pale Detroit wiki chache zilizopita vyombo mbalimbali vya usalama vya Kimarekani vilitupiwa lawama nyingi. Kuanzia FBI, CIA, NSA, TSA, na vinginevyo, vyote vilitupiwa tuhuma na shutuma, na lawama hizo zilielekezwa moja kwa moja Ikulu. Wapo hata waliotaka baadhi ya watendaji wakuu wa taasisi hizo wawajibishwe.

Rais Barack Obama alipoona joto linazidi jikoni akaamua yeye mwenye kuzungumzia suala hilo na moja kwa moja akakubali kuwa lawama zote atupiwe yeye kwani wasaidizi wake wote wanafanya kazi kwa ridhaa yake. Na kutokana na hilo ni yeye mwenyewe aliyeamua kutengeneza pale alipoharibu. Huo ndio uongozi.

Pamoja na yote yaliyotokea hadi hivi sasa nchini mwetu wanasiasa wetu hasa ndani ya chama tawala Rais Kikwete hajawa tayari kusema kuwa (kwa kiasi fulani) anahusika na kilichotendeka. Hatuwezi na hatupaswi kuwa na kiongozi ambaye hajui na kukubali upungufu wake.

11: Ameendela kuacha Idara ya Usalama wa Taifa izorote. Hapa sizungumzii ofisa mmoja mmoja wa idara hiyo, bali sheria, mfumo, muundo na utendaji wake.

Mambo mengi ambayo tunayaona yametoka nchini ndani ya miaka minne ni ishara ya kubomonyoka kwa mihimili ya idara hii. Idara yetu haiwezi kuokolewa kwa kuziba matundu au kwa kuweka plasta.

Bila kuamua kuijenga upya, kuiwezesha upya na kuiimarisha kama kinga yetu ya kwanza dhidi ya wale wanaotaka kutishia uhuru wetu na haki yetu kuwepo kama taifa, tutaendelea kulipa gharama ya ufisadi na makuwadi wa ufisadi. Rais Kikwete amepewa nafasi kubwa katika historia ya kuunda idara hii upya. Matokeo yake tunaona mapendekezo ya mabadiliko ambayo yataendeleza mambo yaleyale!

Angalau safari hii wabunge wameamua kupinga mswada uliotarajiwa kurekebisha sheria mbalimbali na kuunda Baraza la Usalama wa Taifa. Japo kwa kiasi fulani sikubaliani na hoja zilizotolewa na Dk. Willibrod Slaa na Hassani Ngwilizi, naona mantiki ya kukataa kwao.

Haitoshi kwa wabunge wetu kukataa mswada wa Sofia Simba bila ya wao wenyewe kutoa mapendekezo ya mabadiliko wanayoyataka kwenye idara hiyo. Kama wanaona kuwa mswada huu si mzuri na kuwa unampunguzia rais madaraka, je wanaridhika na hali na mfumo wa usalama wa taifa ulivyo sasa?

Kama ni ndiyo, basi waseme hivyo. Kama  hapana walete mapendekezo ya kuboresha idara hii.  Lakini rais yuko wapi katika hili? Ameona upungufu wa idara hii katika utendaji wake wa kazi?

Je, tuna uhakika kuwa mapendekezo anayotaka kuleta hayatakuwa sawa na yale yaliyofanywa na Rais Mkapa na kutupa sheria ya sasa ya usalama wa taifa, ambayo imefungulia uwezekano wa uporaji wa mali na urithi wa taifa? Tutajuaje kuwa mabadiliko wanayoyapendekeza hayatafungulia mlango wa uporaji mwingine wa dakika za mwisho kama ule uliofanywa na Rais Mkapa katika ngwe yake ya pili? Au hata haki ya kuhoji tena hatuna?

10: Ana tatizo la kutoa taarifa sahihi kwa wananchi. Kuanzia suala la mapanki na masuala mengine yaliyofuata,  mara kadhaa sasa Rais Kikwete akipewa nafasi ya kutoa taarifa za vitu rasmi amekuwa na taarifa zisizo sahihi au zilizotiwa nyongeza.

Mfano wa hivi karibuni unahusu gharama ya ujenzi wa miundo mbinu iliyoharibiwa na mafuriko. Alipozungumza na mabalozi katika sherehe ya mwaka mpya, Rais Kikwete alisema gharama ya kujenga miundombinu iliyoharibiwa na mafuriko ingekuwa ni Sh. 6.7, na kuwa serikali itatenga fedha hizo kutoka kwenye bajeti ijayo - na hivyo kukata matumizi kwenye baadhi ya Wizara.

Cha kushangaza ni kuwa alipokuwa njiani kwenda Uswisi wiki iliyopita, alimuambia Rais wa Libya, Kanali Muamar Ghadafi, kuwa Tanzania inahitaji dola milioni 15 kuweza kurejesha miundombinu hiyo iliyoharibiwa kwa mafuriko. Dola hizo ni karibu na Shilingi 19bilioni  za Kitanzania!

Kama hiyo haitoshi Katibu Mkuu wa Wizara ya Miundo, Omar Chambo,  siku chache tu kabla ya hapo alisema kuwa wizara yake  imekadiria gharama ya kujenga upya miundombinu hiyo kuwa Shilingi 10 bilioni  na hizo ndizo walizoomba, na Ikulu wanajua. Huo ni mfano mmoja tu. Kuna mingi mingine.

Tutamalizia sehemu ya mwisho wiki ijayo.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: