Sababu tosha kutenganisha urais na uenyekiti wa chama


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 03 August 2011

Printer-friendly version
Tafakuri

“Kamati Kuu inasikitishwa na tatizo la umeme nchini kwani athari zake kwa uchumi wa taifa na mtu mmoja mmoja ni kubwa. Hivyo basi imeitaka serikali kutumia muda iliyopewa wa kurekebisha bajeti ya wizara ya nishati na madini kuja na mpango wa dharura wa kunusuru hali hii na kisha kulimaliza kabisa tatizo la umeme nchini.”

Nimeanza mjadala wangu kwa kunukuu moja ya maamuzi yaliyofikiwa na Kamati Kuu (CC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) iliyokaa mjini Dodoma 31 Julai  2011ili kuonyesha haja ya kufanyika kwa mageuzi makubwa ya kimuundo nchini.

Kamati Kuu iliyokuwa chini ya mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete, iliamua kuiagiza serikali kutafuta suluhu mgawo wa umeme.

Hapana shaka agizo la CC kwa upeo wangu ni utekelezaji wa wajibu wa chama tawala katika kuisimamia serikali yake; kwa hiyo inaingia akilini ukisema kwamba chama chenye serikali kinaisimamia kwa karibu katika kutatua kero na matatizo mbalimbali ya kitaifa, kikanda, mkoa, wilaya na hata ya mtu mmoja mmoja.

Hata hivyo, wakati huu ambao kuna tatizo kubwa la kimfumo juu ya uwezo wa chama tawala kuisimamia serikali yake unaochangiwa na mchanganyo wa kushindwa kujua ni lini chama kinasimama nje ya serikali na kinyume chake, inakuwa ni vigumu kujua kama kweli kimfumo chama kinaweza kusimamia serikali.

Mchanganyo wa kimfumo ninaozungumza hapa ni ule ninaoufananisha na mdudu anayeitwa paramecia ambaye ana sifa ya kipekee; kujigeuza umbo na kuwa aina tofauti kulingana na mazingira. Aghalabu sifa hii anayo pia kinyonga ambaye ingawa hajipadili umbo, lakini hujibadili rangi kulingana na mazingira aliyoko.

Unapokitazama chama tawala kama CCM unashindwa kujua ni lini chama kinasimama kama chama na ni lini hasa kinasimama kama chama dola kwa maana hiyo kushikanamana kama si kuwa ndani ya serikali moja kwa moja.

Rais wa Muungano ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM, hana uwezo wa kujitenga na serikali yake hata kwa chembe, ni rais na wakati huo huo ni mwenyekiti wa chama. Anasimamia  serikali na wakati huo huo ana maamuzi makubwa na yasiyohojiwa ndani ya chama, hata kama kikatiba mwenyekiti anaweza kuwajibishwa na mkutano mkuu wa chama.

Kimantiki hali hiyo haiwezekani kwa sababu vikao vyote vya maamuzi, kuanzia CC, Halmashauri Kuu ya taifa (NEC) hadi mkutano mkuu wa taifa yeye ndiye mwenyekiti. Haiingii akilini kusema kwamba anaweza kuhojiwa au kupingwa kwenye vikao hivyo.

Ni kwa mantiki hiyo nashindwa kujua Kamati Kuu inaigiza vipi serikali itatue tatizo la mgawo wa umeme wakati mwenye serikali ndiye mwenyekiti wa kamati kuu? Nani anamtuma nani? Je, ni kweli mwenyekiti halijui janga la umeme? Hajui jinsi linavyotafuna uchumi wa taifa hili?

Kila ninaposikia maamuzi kama haya ya  Kamati Kuu iliyochini ya Rais kuitaka serikali kutekeleza jambo fulani, napatwa na wakati mgumu kukataa hoja ya siku za hivi karibuni ya kutaka kutenganisha kofia ya urais na mwenyekiti wa chama tawala ili kuleta uwajibikaji wa kweli.

Ingawa hoja hii inabezwa na baadhi ya watu kwa maslahi yao kisiasa, hakika ni kitu kinachohitaji tafakari ya kina kwa sababu kama kweli tunataka kujenga uwajibikaji wa kweli, mfumo wa kinyonga na paramecia hautufai kitu katika zama za sasa.

Katika mfumo wa kisheria kama wa Tanzania ambao rais anamfuatia Mungu kwa mamlaka makubwa katika uhai na ustawi wa nchi, hakika chama chochote cha siasa chenye kutaka kuona serikali yake ikitekeleza majukumu yake ipasavyo, hakina budi kujaribu kutenganisha kofia hizi mbili.

Ni kweli kwamba mwaka 1985 Mwalimu Julius Nyerere mara baada ya kustaafu urais aliendelea kuwa mwenyekiti wa chama walau kwa miaka miwili kabla ya kuachia nafasi hiyo kwa Rais Ali Hassan Mwinyi; wakati huo ilionekana dhahiri kwamba chama kikitekeleza wajibu wake kama chama na serikali ikifanya kazi kama serikali.

Itakumbukwa kilichorejesha kofia hizo mbili kwa mtu mmoja ni hisia na hofu za kuepuka mgongano baina ya chama na serikali au kuwa wazi zaidi baina ya mwenyekiti wa chama na rais wa serikali; hakika zama za sasa ni muhimu zaidi kuwa na utenganisho wa kofia hizo mbili walau kwa sababu za kiuwajibikaji tu.

Katika mfumo wa sasa ambao serikali iliyoko madarakani inakabiliwa na changamoto kubwa na nzito, hasa kutokana na mfumo wa uwazi na demokrasia pana ya mfumo wa vyama vingi vya siasa, chama tawala ni lazima kiwe na ubavu wa kuikemea serikali yake na serikali iwe na hofu juu ya nguvu ya chama.

Ni kitu kisichowezekana kwa mfumo wa sasa ambao unaakisi zaidi utekelezaji wa mambo wa mfumo wa chama kimoja ambao mwenyekiti wa chama alionekana kama mtu mwenye miujiza, mwenye kujua kila kitu akiwa amesifiwa pande zote, akionekana kama mtu pekee mwenye fikra sahihi zinazostahili kuenziwa; wakati ushindani wa kisiasa unahitaji mfumo unaopokea changamoto na kuzifanyia kazi kwa kasi na tija inayohitajika.

Ukitazama kwa mapana yake sababu ya serikali nje na ndani ya Bunge kupwaya na kuyumba kwa maana ya kushindwa kutimiza wajibu wake, ni utamaduni wa kujigeuza umbo na rangi kwa viongozi wake. Hiwezekani rais ambaye pia ni mwenyekiti wa chama ajione kuwa na mzigo wa kiwajibu kwa chama wakati ni mtu huyu huyu. Mara nyingi kofia ya chama imetumika si kuifanya serikali iwajibike, ila ni njia ya kupitia kushika madaraka ya dola baada ya hapo chama kinabakia kuwa alama tu.

Ipo mifano ya kweli ambayo inaonyesha nguvu ya chama dhidi ya serikali pale inapoonekana kuwa serikali au Rais ameshindwa kutimiza wajibu wake sawa sawa. Mfano mmojawapo ni ule wa Afrika Kusini ambao Rais Thabo Mbeki aliondolewa madarakani na chama chake kwa sababu alionekana kuendesha mizengwe na hila dhidi ya Jacob Zuma.

Si lazima kufikia hali ya Afrika Kusini, lakini ni vema na haki kabisa huko tuendako kuanza kufikiria kama taifa nini faida na hasara za kuunganisha kofia mbili, yaani urais na uenyekiti wa chama tawala.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: