Sabuni ya Mbilinyi haimsafishi Mkapa


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 11 February 2009

Printer-friendly version
Mbilinyi atetea Mkapa, azamisha mkewe

WAZIRI wa Fedha wa zamani katika serikali ya Awamu ya Tatu, Profesa Simon Mbilinyi, amejitosa katika mjadala unaomhusisha rais mstaafu Benjamin Mkapa.

Katika mahojiano yake yaliochapishwa katika gazeti la RAI, Alhamisi iliyopita, Profesa Mbilinyi anasema anayestahili kuchunguzwa ni Anna Mkapa wala si mumewe, Benjamin Mkapa.

Anasema Anna Mkapa ndiye anayetakiwa aeleze jinsi alivyoendesha Mfuko wa Fursa Sawa kwa Wote (EOTF).

Profesa Mbilinyi, mchumi na mwanasiasa, alikuwa mbunge wa Peramiho, mkoani Ruvuma, kati ya mwaka 1995 na 2005.

Alijiuzulu wadhifa wake waziri wa fedha baada ya kukumbwa na kashifa ya kutoa misamaha ya kodi isivyo halali kwa wafanyabiashara ya minofu ya samaki katika Kanda ya Ziwa Viktoria.

Profesa Mbilinyi alisema Anna Mkapa ndiye anayestahili kuhojiwa kutokana na kujilimbikizia mali nyingi.

Alisema, “Huyu ndiye anayetakiwa kuhojiwa, tena kwa umakini. Anatakiwa kueleza hela za kuendesha mfuko ya EOTF zinatoka wapi, mafanikio yaliyofikiwa na hesabu za mfuko.” Mama Mkapa ndiye mwenyekiti wa taasisi hiyo.

“Mfuko wa Mama Mkapa,” ulianzishwa mara baaada ya Rais Mkapa kuingia madarakani, Novemba 1995. Kwa muda wote ambao Mkapa alikuwa ikulu, mfuko huu ulikuwa unaendeshea shughuli zake katika majengo ya Ikulu.

Taarifa zinasema, hata gharama za bili ya maji, umeme, simu na mishahara ya wafanyakazi vililipwa na serikali. Misaada na michango iliyotolewa na wafadhili, mingi ilitolewa kwa kuwa mwenyekiti wake ni mke wa rais; mfuko ulionekana kama vile ni wa umma.

Akiongea kama vile anataka kumuopoa Mkapa katika dhahama, Profesa Mbilinyi alisema, “Tumuache Mkapa apumzike. Tuangalie nyuma kafanya nini. Mkiangalia ya nyuma, basi mtakaa miaka 10 bila kufanya kitu. Hiyo ndiyo hofu yangu ya kumuondolea kinga Mkapa na kumshitaki.”

Lakini papohapo, Profesa amesema, “Anna Mkapa, amejilimbikizia mali nyingi zenye thamani kubwa; hivyo hoja ya kumchunguza inapata nguvu.”

Akionekana kutaka kumtokomeza Anna na kumuokoa Mkapa, Profesa Mbilinyi alisema, “Anna Mkapa ndiye anamiliki mali nyingi za thamani. Lakini hakuna haja ya kumvua kinga Mkapa kumshitaki kwa makosa anayotuhumiwa kufanya akiwa ikulu.”

Profesa Mbilinyi alikuwa waziri wa kwanza wa fedha katika serikali ya Benjamin Mkapa. Vilevile alikuwa waziri wa kwanza wa Mkapa kujiuzulu na kutoka katika serikali hiyo.

Ni Bunge la Muungano lililoshupalia Mbilinyi hadi kujiuzulu. Hata jitihada kubwa zilizofanywa na Mkapa kumuokoa waziri wake Mbilinyi hazikuweza kusaidia. Alilazimika kujiuzulu; tena shingo upande.

Hatua ya wabunge kushupalia Profesa Mbilinyi, haikumfurahisha Mkapa. Pamoja na mengine yaliyohusu waliochokonoa serikali yake, Mkapa alinukuliwa akiapiza kuchukua hatua kama kulipiza kisasi.

Kuna wakati alisema wabunge wasisahau kuwa atakuwa mwenyekiti wa kikao cha chama cha kupitisha majina ya wagombea katika uchaguzi mkuu uliokuwa unafuatia. Alifanikiwa kutimiza ahadi hiyo.

Bali kauli ya Profesa Mbilinyi imejikita katika maeneo mawili makuu. Kwanza, anamtetea Mkapa kwa kutumia vitisho dhidi ya wananchi. Anasema hatua ya kumpeleka Mkapa mahakamani inaweza kurudisha nyuma maendeleo ya taifa.

Pili, anamtetea Mkapa na kumtokomeza mkewe, Anna kwa madai kwamba “hakuna kosa lililofanywa na Mkapa. Anasema makosa yote yamefanywa na mkewe; huyu ndiye wa kulaumiwa.

Hakika Profesa Mbilinyi hawezi kumtetea Mkapa kwa kutaka kumtokomeza Mama Anna Mkapa. Benjamin Mkapa na mkewe, wote wanastahili kujibu tuhuma dhidi yao, kama zipo.

Kwa mfano, ni Anna na mumewe, waliootesha kampuni ya ANBEN Limited, wakiwa ikulu. Benjamin Mkapa na Anna Mkapa, wakiwa wakurugenzi na wamiliki.

Kampuni ya Mkapa na mkewe ilisajiliwa na kuanza biashara mwaka 1999, wakati huo Mkapa alikuwa rais na Anna alikuwa mke wa rais. Hapa huwezi kutenganisha Mkapa na Anna.

Anuani ambayo kampuni hii ilitumia, ilikuwa ileile iliyotumiwa na ikulu, na kwamba kampuni ya Mkapa na mkewe ilikuwa Mtaa wa Luthuli Na. 15, ambako taasisi ya EOTF iliweka makao yake. Hivi ni viwanja vya ikulu.

Je, hapa unaweza kumuweka Mkapa upandeni na kumshitaki Anna, au profesa anataka kutuambia kwamba kampuni hiyo haimhusu Mkapa?

Hata katika suala la utajiri wa Anna, Mkapa hawezi kujitenganisha nao. Kauli ya Mbilinyi inathibitisha hilo, kwamba mama Mkapa alitumia vibaya, ama fedha za mfuko au nafasi yake ya kuwa mke wa rais.

Kikubwa zaidi, mpaka sasa Mkapa mwenyewe hajasema kama mkewe alitumia vibaya madaraka yake.

Kuna haya madai ya Mkapa kuwa mmoja wa wamiliki wa mgodi wa mawe ya mkaa wa Kiwira mkoani Mbeya.

Katika sakata hilo, Mkapa haonekani. Wanaotajwa kuwa ni wakurugenzi ni mtoto wa kuzaa wa Benjamin Mkapa, Nick (Nicholas) Mkapa na mkewe Foster Mkapa, ambao wametajwa kuwa wamiliki wa kampuni ya Fosnik Enterprises, moja ya makampuni yanayomiliki mgodi huo.

Inawezekana aliyeshinikiza mchakato si Mkapa binafsi, bali ni mkewe Anna. Hata kama Mkapa ndiye aliyeshikiniza mchakato wa kukwapua mgodi wa Kiwira, bado Anna ana nafasi ndogo ya kufaulu kujinasua katika lawama.

Katika hili, mke ameshindwa kumshauri vema mumewe, Mkapa hadi mgodi umechukuliwa na watu walioko katika familia pana ya Baba na Mama B. Mkapa.

Kuhusu suala kwamba kumkamata Mkapa kutatia hofu watendaji wa serikali na hatimaye washindwe kutimiza majukumu yao, sina hakika iwapo profesa anaamini alichokisema.

Kutokana na hali hiyo, hoja ya Profesa Mbilinyi haina mashiko. Kwa bahati mbaya, hadi leo hii hakuna anayeweza kuamini kwamba Mkapa alitenda aliyotenda kwa nia njema.

Kitendo chake cha kuanzisha makampuni binafsi na kununua nyumba ya umma akiwa bado ikulu, vimewashinda hata watangulizi wake.

Utajiri wa Mkapa wakati anaondoka ikulu, ungelinganishwa na mali aliyoingia nayo wakati akiingia ikulu, bila shaka yangejengeka mashaka kuhusu kujitajirisha akiwa kwenye utawala.

Katika hili hakuna ubishi kwamba haihitajiki kuondoa kinga kwani kinga haihusiki na yaliyotendeka hayahusiani utendaji serikalini.

Inawezekana basi kujenga hoja kuwa Mkapa alitumia urais kurahisisha ufanikishaji biashara zake wakati akiwa ikulu. Hilo likithibitika, basi hakuna haja ya kinga, kwani kinga haihusiki katika mambo ambayo rais alitenda nje ya yale aliyopaswa kwa mujibu wa katiba.

Sabuni ya Profesa Mbilinyi inazidi kutonesha vidonda vya wananchi. Sasa wananchi wanafahamu kwamba “kumbe hakuwa Mkapa pekee yake, alikuwa pamoja na mkewe, Anna.”

Na kwa kuwa Profesa Mbilinyi alikuwa waziri wa fedha katika serikali ya Mkapa, basi anajua mengi. Tumsikilize zaidi.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: