Safari za Kikwete zakausha hazina


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 12 May 2010

Printer-friendly version
Rais Jakaya Kikwete

SAFARI za Rais Jakaya Kikwete nje ya nchi, tangu alipoingia madarakani, zimeligharimu taifa mabilioni ya shilingi, MwanaHALISI limebaini.

Uchunguzi umeonyesha kuwa katika kipindi cha miaka minne tangu awe rais, Kikwete amekaa nje ya nchi kwa takribani siku 120, sawa na miezi minne.

Hadi mwishoni mwa mwaka jana, kiasi cha Sh. 2.4 bilioni zilikuwa zimetumika kwa ajili ya posho na gharama za malazi kwa rais na ujumbe wake nchi za nje.

Mara nyingi, ujumbe wa rais huhusisha mkewe, walinzi, waziri kutoka wizara inayohusika na safari, waziri wa mambo ya nje, pamoja na wasaidizi binafsi wa rais na wale wa mke wake.

Kwa mujibu wa uzoefu wa safari, ujumbe wa rais anaposafiri nje ya nchi huwa na kati ya wajumbe 15 na 22.

Kwa viwango vya serikali, watu wanaosafiri kwenye msafara wa rais hulipwa kiasi cha kati ya dola 350 na 500 (Sh. 600,000 kwa siku).

Hata hivyo, MwanaHALISI limeambiwa kuwa rais hutakiwa kulala katika hoteli yenye hadhi ya aina yake – ambayo gharama yake huwa kati ya dola 800 na 1,200.

Kwa kuimarisha ulinzi na kukabiliana na upweke, hoteli anakolala rais hulaza pia walau watu wanne, gazeti limeelezwa.

Hawa wanaweza kuwa walinzi wa rais, daktari na wasaidizi wake wa karibu ambao anaweza kuwahitaji wakati wowote.

Kwa hiyo, kwa msafara wa watu 20 ambayo ni idadi ya kawaida kwa msafara wa rais, hasa anapokwenda nje ya nchi, wastani wa matumizi  kwa siku inaweza kufikia kiasi cha dola 15,000 (Sh. milioni 20).

Kwa safari kama ya Mei 12 hadi Mei 26 mwaka 2006, wakati Rais Kikwete alipokuwa nje ya nchi kwa karibu wiki mbili, kiasi cha Sh. 273 milioni  kilitumika kwa ajili ya safari hiyo pekee.

Katika safari yake hiyo, Rais Kikwete alitembelea Uganda, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Ufaransa na Marekani.

Katika mahojiano mbalimbali ambayo MwanaHALISI limefanya na wafanyakazi wa ikulu pamoja na wizara ya mambo ya nje, gazeti limeambiwa kwamba kiasi hicho (Sh milioni 273) “si kikubwa sana” kwa viwango vya  matumizi wakati wa ziara za wakubwa nje ya nchi.

Kwa safari hiyo pekee, Kikwete alitumia fedha nyingi kuliko kiasi cha fedha kilichotengwa kwa ajili ya safari zake zote za nje ya nchi kwa mwaka huu wa fedha (2009/2010).

Kwa mujibu wa bajeti ya mwaka huu, rais ametengewa Sh. 115 milioni kwa safari za nje; takwimu ambazo zimeleta utata ikilinganishwa na matumizi kwa safari za ughaibuni.

Kwa mfano, bajeti ya safari za nje, kwa mujibu wa bajeti ya 2009/2010, imekuwa ndogo kiasi kwamba kwa uzoefu, fedha zote zinaweza kutumika kwa safari moja tu.

Aidha, bajeti ya ikulu ya safari za ndani ya nchi nayo imeongezeka kutoka Sh. 608,419,000 kwa bajeti ya mwaka 2008/2009 hadi Sh. 723,360,000 kwa mwaka 2009/2010, ikiwa ni ongezeko la Sh. milioni 114.9.

Kwa takwimu hizi, matumizi ya safari za ndani za ikulu (rais) yanaonekana kuwa makubwa kuliko yale ya nje, jambo ambalo wazoefu wa safari za ikulu wameeleza kuwa siyo sahihi.

Miongoni mwa mambo ambayo Rais Kikwete amekuwa akilalamikiwa na wanasiasa, wanaharakati na wananchi kwa jumla, ni wingi wa safari zake za nje ambazo zinaelezwa kuwa zinachota fedha nyingi kwa manufaa haba.

Rais alifanya safari nyingi mwaka 2006 hadi kulalamikiwa na wananchi. Miongoni mwa safari za mwaka huo pekee ni kama ifuatavyo:

 • Tarehe 19-25 Januari alikuwa Khartoum, Sudan kuhudhuria mkutano wa nchi za Afrika (AU)
 • 23 Machi  alifanya ziara ya siku moja ya kiserikali kujitambulisha Kigali, Rwanda.
 • Tarehe 22 Machi rais alikwenda Kampala, Uganda kwa ziara ya siku moja ya kujitambulisha
 • 24 Machi alikwenda Nairobi, Kenya
 • 19-20 Aprili alikuwa Lesotho na Swaziland.
 • Tarehe 21-22 Aprili rais alikuwa ziarani Maputo, Msumbiji;
 • 28 Aprili alikuwa Harare na Bulawayo, nchini Zimbabwe
 • 6 Aprili alikuwa Gaborone, Botswana.
 • Rais alikuwa ziarani Namibia 10-12 Aprili;
 • Tarehe 7-9 Mei alikuwa Pretoria, Afrika Kusini.
 • Tarehe 12 Mei rais alianza ziara ya wiki mbili katika nchi za Uganda (13 Mei), Arabuni (15 Mei), Ufaransa (16-19 Mei) na Marekani (21-26 Mei).
 • Tarehe 31 Mei hadi 3 Juni rais alihudhuria Jukwaa la Kiuchumi la Dunia mjini Cape Town, Afrika Kusini
 • Tarehe 4 Julai alihudhuria mkutano wa AU, Banjul nchini Gambia.
 • Julai 10-12 rais alikuwa Cape Town, Afrika Kusini kuhudhuria mkutano wa viongozi wa serikali ulioandaliwa na kampuni ya Microsoft ya Marekani
 • 20 Julai alihudhuria mkutano wa Leon Sullivan, Abuja nchini Nigeria.
 • Rais alikuwa Berlin 21 na 22 Julai kwa ajili ya kuchunguza afya yake;
 • Alihudhuria mkutano wa SADC, Maseru nchini Lesotho kati ya 19 na 20 Agosti
 • Tarehe 21-22 mwezi huo alikuwa ziarani Angola.
 • Rais Jakaya Kikwete alikuwa Cuba tarehe 12 Septemba kwa maandalizi ya kikao cha Nchi zisizofungamana na upande wowote (NAM);
 • 15 Septemba alikwenda Madrid, Hispania kwenye Uwanja wa Mpira wa uwanja wa Santiago Bernabeau unaotumiwa na klabu mashuhuri ya Real Madrid.
 • Septemba 15 hadi18, rais alikuwa Havana, Cuba kwa mkutano wa NAM
 • Kati ya 19 na 25 Septemba, rais alikuwa kwenye mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, New York.

MwanaHALISI lina taarifa kuwa tayari matumizi ya serikali kwa jumla mwaka huu wa fedha yamezidi kiwango kilichoombwa wakati wa kikao cha Bunge la bajeti mwaka jana.

Enzi za utawala wa Rais Benjamin Mkapa, kuna wakati ilidaiwa kwamba Waziri Mkuu, Frederick Sumaye, alitumia kiasi cha Sh. 500 milioni kwa safari moja tu nchini Marekani.

Pia mwaka 1990, msafara wa Tanzania ulioongozwa na Rais Ali Hassan Mwinyi kwenye mkutano wa Dunia wa Mazingira uliofanyika Rio de Janeiro nchini Brazil, ulinusurika kuzuiwa kuondoka baada ya kumaliza fedha zote zilizotolewa.

Miongoni mwa maofisa wa ngazi za juu wa wizara ya mambo ya nje waliozungumza na gazeti hili wiki iliyopita, wakati wa safari yoyote ya rais nje ya nchi, sharti msafara uwe na angalau dola 50,000 hadi 100,000 (kati ya Sh. 70 na 140 milioni).

“Unajua haya mambo wakati mwingine yanategemea na kiongozi wa nchi uliye naye. Kama unasafiri na Nyerere siyo sawa na kama unasafiri na Mobutu. Kama kiongozi ni mfujaji mtatumia fedha nyingi na kama kiongozi si mfujaji basi mtatumia fedha kidogo.

“Cha msingi ni kwa mkuu wa msafara kutoa taarifa serikalini kuhusu matumizi. Si kwamba kama utapewa dola 50,000 basi ni lazima uzitumie zote hadi ziishe. Lakini kama kiongozi anajua kutumia, hela zitaisha tu. Si mradi zitolewe maelezo tu,” alisema.

Uchunguzi umebaini kuwa tangu awe rais, Kikwete ameonekana kupendelea sana kwenda nchini Marekani na Uingereza.

Hadi mwanzoni mwa mwaka huu, Kikwete ametembelea Marekani mara nane na Uingereza zaidi ya mara nne; mara nyingine akipitia tu kutoka katika nchi nyingine.

Tathmini ya MwanaHALISI imeonyesha kwamba kwa wastani, ziara za Kikwete katika nchi za Afrika huchukua wastani wa siku mbili wakati Ulaya huchukua wastani wa siku tatu hadi nne.

Pia, Kikwete alifanya safari nyingi zaidi ughaibuni mwaka 2006 kwa lengo la kujitambulisha kwa nchi mbalimbali na mwaka 2008 alipokuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU).

MwanaHALISI limefanikiwa kukusanya orodha ya safari zote ambazo Kikwete amefanya tangu alipoingia madarakani hadi mwanzoni mwa mwaka huu.

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: