Sakata la Dowans: Waziri Ngeleja siyo mkweli


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 18 March 2009

Printer-friendly version

SAKATA la ununuzi wa mitambo ya kufua umeme kutoka kampuni ya Dowans Holding (Tanzania) Limited, halijapatiwa ufumbuzi.

Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja amenukuliwa Ijumaa iliyopita katika mkutano wake na waandishi wa habari akisema, “Serikali imefunga mjadala wa Dowans kwa sababu Tanesco imesema hainunui tena mitambo hiyo.”

Kauli ya Ngeleja imekuja wiki moja baada ya Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Dk. Idris Rashid kutangaza kujitoa kwa shirika hilo  katika mpango wa kununua mitambo ya Dowans.

Dk. Rashid anasema shirika lake limeamua kuchukua hatua hiyo kwa kile alichodai, “Masuala ya msingi ya taaluma ya ufundi kumezwa na wanasiasa.”

Hata hivyo, ukichunguza kwa makini kauli za Ngeleja na Dk. Rashid, utabaini mara moja kwamba bado serikali inatamani kununua mitambo ya Dowans.

Hii ni kutokana na kauli ya Ngeleja kwamba, “Hakuna sheria yoyote ya manunuzi ya umma inayozuia ununuzi wa mitambo iliyotumika.” Anasema jambo hilo liko kwenye kanuni za Bunge tu.

Anasema waziri wa nishati na madini anaweza kuruhusu kununua mitambo chakavu, kulingana na mazingira.

Hakuishia hapo. Alifikia hata hatua ya kupotosha ukweli kwamba Bunge limeruhusu serikali kununua mitambo iliyotumika kutoka kampuni ya Independent Power Company (IPTL), lakini wakati huohuo linapinga ununuzi wa mitambo ya Dowans.

Kwanza, waziri amedanganya kwa kusema kwamba hakuna sheria yoyote inayozuia ununuzi wa mitambo iliyochoka. Sheria ya Manunuzi ya Umma (PPA) ya mwaka 2004 katika kifungu cha 58 (3) inakataza kabisa ununuzi wa mitambo chakavu.

Bali, kuna kanuni inayokubali ununuzi wa mitambo chakavu. Na hiyo si sheria, ni kanuni. Ngeleja anashindwa kutofautisha kati ya kanuni na sheria.

Kanuni ikigongana na sheria, sheria ndiyo inachukuliwa kuwa sahihi kwa kuzingatia mantiki na mtima wa sheria kama ilivyonuiwa na watunga sheria wenyewe (wabunge).

Pili, mkataba kati ya IPTL na serikali una uhai wa takriban miaka 20. Ulisainiwa mwaka 1995 katika kipindi kile ambacho taifa lilitumbikia katika tatizo kubwa la uhaba wa umeme kwa mara ya kwanza.

Tangu wakati huo hadi sasa, Tanesco haijaweka msingi imara wa kupambana na tatizo la uhaba wa umeme. Wala serikali haijajenga vyanzo vya uhakika vya upatikanaji umeme.

Inadaiwa kwamba vyanzo karibu vyote vya kuzalisha umeme vilivyopo sasa, vilijengwa au kuanzishwa wakati wa utawala wa awamu ya kwanza chini ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Mabwawa ya Mtera, Kihansi, Kidatu na Nyumba ya Mungu yalijengwa wakati wa Mwalimu.

Katika kipindi chote cha uhai wa mkataba, Tanesco wanalazimika kulipa kampuni ya IPTL Sh. 3.5 bilioni kila mwezi zikiwa gharama za kuweka tu mtambo – uwe unazalisha au hauzalishi.

Bunge lilipendekeza kwa serikali, ama kununua mitambo ya IPTL, au kuibadilisha ili iweze kutumia gesi asilia badala ya dizeli kama ilivyo sasa.

Bunge liliamini kwamba kwa kuibadilisha mitambo hiyo kutoka matumizi ya dizeli hadi gesi, Tanesco ingeweza kupunguza bei ya umeme unaozalishwa na IPTL.

Hata hivyo, mpaka sasa mapendekezo ya Bunge hayatekelezwa na wizara ya Ngeleja, ingawa tayari Tanesco imependekeza kwa serikali kufanya hivyo haraka. Hata Rais Jakaya Kikwete ametoa wito kwa Ngeleja kununua mitambo ya IPTL.

Akizindua mitambo ya Tanesco ya megawati 102.4 iliyopo Ubungo, tarehe 5 Novemba 2008, Rais Jakaya Kikwete alimtaka Ngeleja ahakikishe mitambo ya IPTL inageuzwa kutoka matumizi ya mafuta kwenda gesi asilia ili kupunguza gharama.

Kikwete alisema anataka kesho na kesho kutwa kusiwepo visingizio vya kukosekana kwa umeme kutokana na mitambo ya IPTL.

Lakini ambacho Ngeleja hajakisema, au hakijui, ni kwamba Bunge linataka serikali inunue kampuni ya IPTL, si mitambo peke yake. Kampuni na mitambo ni vitu viwili tofauti.

Kwa kununua kampuni, serikali haitalipa tena Sh. 3.5 bilioni kwa mwezi au Sh. 42 bilioni kwa kila mwaka zinazolipwa kwa kampuni hiyo kama malipo ya kuweka mitambo kwa muda wote wa uhai wa mkataba.

Hicho ndiyo chanzo cha serikali kutoa ruzuku kwa Tanesco ili iweze kujiendesha. Hapo ndipo Bunge lilipotaka serikali kununua kampuni ya IPTL.

Hali hiyo ni tofauti kwa upande wa Dowans. Katika Dowans, serikali inataka kununua mitambo, hainunui kampuni.

Kutokana na hali hiyo, haijafahamika mwanasheria aliyebobea kama Ngeleja anashindwa vipi kujua tofauti ya kununua kampuni na mitambo?

Badala yake, anadanganya kwa kusema, “Hata Hansard za Bunge (kumbukumbu za Bunge)” zinaruhusu serikali kununua mitambo ya IPTL. Hili si la kweli hata kidogo.

Kibaya zaidi, Dowans hawana mkataba na serikali. Kampuni hiyo imerithi kinyemela mkataba huo kutoka kampuni ya Richmond ambayo tayari imethibitishwa kuwa ilikuwa kampuni ya kitapeli, isiyokuwa na hadhi wala uwezo wa kufanya kazi iliyoomba.

Katika IPTL, wananchi wanajua nani anayejadiliana na serikali. Nani anayelipwa na nani aliyefunga mkataba. Lakini kwa Dowans hakuna kinachojulikana. Ni kiza kitupu.

Kwa hiyo siyo sahihi kulinganisha Dowans na IPTL. Kujaribu kufanya hivyo ni kutaka kuwatupia madongo usoni wananchi wengi ambao huenda hawajui vema makampuni haya.

Aidha, kufanya hivyo, ni kujenga pazia mbele ya umma na kutaka kufanya mambo gizani au kwa ulaghai wa makusudi.

Wananchi wenye uzalendo wangependa kusikia na kuona, kwa uthibitisho, mitambo ya Dowans ikitaifishwa na serikali kutokana, kama ilivyoelezwa hapo juu, na mitambo hiyo kuwa sehemu ya mkataba ulioghubikwa na ulaghai. Je, serikali inangoja nini?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: