Sakata la Mkapa: Vyombo vya habari vimetimiza wajibu wake


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 30 June 2009

Printer-friendly version

HATIMAYE kazi ya vyombo vya habari imeonekana. Kumbe king’ang’anizi kina manufaa yake na hasa ndilo jukumu la uandishi wa habari.

Kwa miaka miwili sasa, vyombo vya habari vimeshika bango. Vinadai kuna tuhuma nyingi zinazomwandama rais mstaafu Benjamin Mkapa na kwamba hakuna sababu ya kuzifumbia macho.

Wiki iliyopita, serikali kupitia Waziri Mkuu Mizengo Pinda, iliamua kujitwisha mzigo wa kumtetea Benjamin Mkapa.

Hatua ya waziri mkuu inavunja kimya cha muda mrefu cha serikali. Lakini wakati serikali imekaa kimya, vyombo vya habari vimekataa kukaa kimya.

Kila baada ya siku, wiki na hata mwezi, vyombo vya habari vimekuwa vikikumbusha na kuuliza, “kulikoni” kuhusu serikali kuchukua hatua.

Tuhuma zinazomkabili Mkapa zimekuwa nyingi. King’ang’anizi nacho kimekuwa kikubwa na cha mara kwa mara na kwa muda mrefu.

Sasa imefikia wakati serikali ikajua kuwa isiposema lolote juu ya tuhuma zinazomwandama Mkapa, basi vyombo vya habari vitaendelea kuandika, kukumbusha na kukumbusha.

Katika maisha ya kawaida, vyombo vya habarai vimekuwa mbu aliaye sikioni mwa anayetaka kusinzia. Husinzii kamwe. Utapiga huku na kule lakini huui mbu wala hupati usingizi.

Hatimaye utaamua kuamka na kumsaka mbu au itabidi uingie kwenye chandarua; upate usingizi lakini ukitoka humo utakuta mbu amekusubiri nje na kukupiga mshale wa sumu.

Hatua ya waziri mkuu, hata kama haina mantiki ya maana, inafuatia kazi nzuri ya vyombo vya habari kung’ang’ania jambo moja na kutaka kujua hatma yake.

Hata hapo hoja hii ilipofikia, bado hakuna sababu ya kunyamaza na bila shaka vyombo vya habari vitaendelea kudodosa na kukumbusha.

Wananchi wanataka kujua hatma ya tuhuma. Wanataka kujua iwapo ni kazi ya serikali “kununua tuhuma.” Wanataka kujua serikali italipwa na nani pale inapojitwisha mzigo wa watu wengine.

Mkapa anatuhumiwa kutenda kinyume na maadili ya urais wakati alipokuwa madarakani. Kwamba aliongoza kikao cha Baraza la Mawaziri kupitisha ubinafsishaji wa mgodi wa mkaa wa mawe wa Kiwira, mkoani Mbeya.

Kwamba baada ya uamuzi wa ubinafishaji wa Kiwira kupitishwa, Mkapa akamilikisha mgodi huo kwa kampuni yake na aliyekuwa waziri wake wa Nishati na Madini, Daniel Yona.

Akihitimisha mjadala wa hotuba ya bajeti ya ofisi yake bungeni, Ijumaa iliyopita, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alisema, “Mkapa ni mtu msafi, muadilifu na mcha Mungu.”

Alisema kama suala ni mgodi wa Kiwira, serikali iko tayari kuurudisha mgodi huo mikononi mwa wananchi.

Lakini kuna tuhuma nyingi zaidi. Tarehe 22 Februari 2007, akiwa mjini Burussels, Ubelgiji, Rais Jakaya Kikwete alitakiwa amtake Mkapa aseme lolote kuhusiana na ununuzi wa rada ya kijeshi.

Akiwa Sweden, Kikwete alimtetea tena Mkapa kwa kusema, “Mkapa asisakamwe.” Alikuwa akijibu hoja za Watanzania waishio Sweden ambao walikuwa wanataka kufahamu kilichotokea wakati wa zoezi la ubinafshaji wa mashirika ya umma na uuzaji wa nyumba za serikali.

Kwenye mkutano wake na waandishi wa habari, Ikulu, Dar es Salaam, miaka miwili iliyopita, alipoulizwa iwapo naye ataanzisha biashara akiwa ikulu na kama atachukua hatua dhidi ya Mkapa, Kikwete alisema, “Mwacheni Mzee Mkapa apumzuke.”

Mkapa, akiwa bado ikulu, alijiita mjasiliamali wakati wa kuanzisha kampuni binafsi.

Sasa hoja ya Pinda ni kwamba “Mkapa hajalimbikiza fedha katika mabenki ya nje.” Hii ni hoja ambayo hakika, haina mashiko na hakuna aliyemuuliza ameweka fedha nje au mchagoni.

Pili, kumiliki fedha katika mabenki, au kuweka mchagoni, si hoja. Hoja hapa ni kwamba Mkapa amekuwa akituhumiwa kutumia vibaya dhamana yake ya ukuu wa nchi na dola.

Mkapa amechanganya mamlaka hayo na ujasiriamali, kwa kuunda kampuni wakati akiwa madarakani. Ni kampuni hiyo inayodaiwa kutumika kumiliki Kiwira.

Wala hakuna ubishi kwamba hoja ya Mkapa kutumia vibaya madaraka ya urais, imepewa kipaumbele na vyombo vya habari hadi serikali kufikishwa hapa kwenye kona.

Katika taifa kama hili, ambalo watawala wanatenda kama vile kesho wanahama, ni muhimu kuwapo kwa vyombo huru vya habari ili kuweza kuibua na kufuchua tuhuma na shutuma dhidi ya wale waliokabidhiwa mamlaka.

Ni vyombo vya habari vilivyokuwa vya kwanza kufichua hatua ya Mkapa kuunda kampuni akiwa madarakani.

Ni vyombo hivyo hivyo, vilivyoanika hadharani jinsi Mkapa na mkewe walivyotumia kampuni hiyo kujimilikisha mgodi wa Kiwira wakishirikiana na kampuni nyingine nne, kujipatia hisa katika mgodi huo kwa kutumia kampuni mwavuli iitwayo TanPower Resources Limited.

Hadi sasa Pinda ana ukweli wote kuhusu tuhuma. Kile ambacho serikali imekuwa ikitakiwa kufanya ni kuchukua tuhuma hizo na kuzichunguza na kufikia mwisho wake.

Pinda aelewe kuwa vyombo vya habari havipati taarifa kutoka kwenye sayari nyingine, kama vile Mars au Jupiter. Afumbue macho kuwa wanahabari wanafanya kazi ndani ya jamii.

Wakati anaingia madarakani Mkapa alipachikwa jina la “Mr Clean” – mtu safi; na alitangaza hadharani mali zake. Lakini wakati wa kuondoka ameshindwa kufanya hivyo, na kamwe hana ubavu wa kufanya hivyo.

Ni vyombo vya habari vilivyobaini kuwa Mkapa alichafuka wakati akiwa Ikulu, baada ya kushika na kutumia madaraka na mamlaka yake vibaya.

Kama angekuwa anashauriwa vizuri, Pinda angeongoza harakati za serikali kumchunguza Mkapa, huku akitumia ushahidi unaowekwa hadharani katika vyombo vya habari kila uchao.

Pinda hajamaliza shutuma, tuhuma wala wasiwasi wa wananchi. Anachofanya ni kuzika hoja zikiwa hai. Tatizo ni kwamba hoja za aina hiyo huweza kumea na kuwa mimea

Hakuna ajuaye kuwa miaka hata 10 au 20 ijayo, hakuna atakayeyaibua yote yaliyozikwa. Vyombo vya habari vitaendelea kunukuu na kuwa shahidi.

Vyombo vya habari vingenyamazia tuhuma zinazoendelea dhidi ya Mkapa, serikali isingenyenyekea hata kuonekana kumwombea radhi rais mstaafu. Uhuru wa vyombo vya habari ni muhimu.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: