SAKATA LA MWAKYEMBE: Iwe kweli au uwongo, yote ni mabaya


Kondo Tutindaga's picture

Na Kondo Tutindaga - Imechapwa 22 February 2012

Printer-friendly version

SAKATA la naibu waziri wa ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe kupewa sumu limezidi kuchukua sura mpya kila uchao. Safari hii, kila mmoja anamkimbia mwenzake – serikali na Mwakyembe.

Jeshi la polisi limeshikwa kigugumizi. Pale inapoamua kusema haimalizi ilichokusudia, jambo ambalo linasababisha maswali mengi zaidi.

Naye Dk. Mwakyembe mwenyewe amekuwa ama kimya au akisema bila kutamka wazi wazi ni nini kimemsibu. Mtindo huu wa Dk. Mwakyembe, haumsaidii yeye, haulisaidii taifa wala mtu yeyote isipokuwa kuwasaidia hao anaodhani walimpa sumu.

Anayenufaika na kigugumizi cha jeshi la polisi ni hao wanaodhaniwa walimpa sumu Dk. Mwakyembe.

Wizara ya Afya nayo imekuwa na mbweteko wa ajabu katika suala hili. Tuhuma za kiongozi wa serikali kupewa sumu zinapogeuzwa kuwa ni ugonjwa na kwa hiyo kuifanya wizara kushikilia msimamo wa kutunza siri za mgonjwa, wizara ndiyo inayogeuka kuwa mgonjwa.

Tuhuma za kupewa sumu kwa kiongozi wa serikali si suala la ugonjwa bali ni jinai, tena yenye harufu ya uhaini. Maana tunaweza kushtuka sumu hiyo kama ipo imeingia katika mwili wa “serikali” yenyewe na kuiangusha.

Msimamo wa wizara kujifanya wanalinda siri za “mgonjwa bandia” aitwaye Dk. Harrison Mwakyembe ni uzembe usiovumilika. Matokeo ya uzembe huu sasa yanasabisha serikali yenyewe kwa yenyewe inarushiana tuhuma kana kwamba sumu hiyo walipeana ndani ya baraza la mawaziri.

Kwangu mimi, iwe ni kweli Dk. Mwakyembe alilishwa sumu au hakushikishwa sumu, ni suala baya na la hatari. Iwe ni uwongo na uzushi kama jeshi la polisi linavyoeleza, nalo ni baya na chafu sana. Kwa hiyo, iwe kweli au uwongo, tuna dude mikononi mwetu linaloweza kutusumbua sana kama taifa.

Kama ni kweli kuwa Dk. Mwakyembe alilishwa au alishikishwa sumu ni jambo baya na la hatari. Sitaki kuhoji sumu hiyo iliingiaje nchini kwa sababu naelewa mwanya tuliouweka sisi wenyewe wa kuwaweka viongozi wetu juu ya sheria za nchi, unaweza kutumika kutorosha chochote kutoka nchini mwetu au kuingiza chochote nchini mwetu pasipo shaka yoyote.

Inapofika hata nyumba ndogo za wakubwa zinapewa hadhi za kibalozi na kupitia VIP katika viwanja vya ndege, ni wazi sumu ya hatari yaweza kuingizwa nchini pasipo shaka yoyote.

Inapofikia mitandao ya kusaka madaraka inajipenyeza hata katika hospitali zetu, hakuna shaka kuwa sumu za hatari zinaweza kutengezwa ndani ya maabara zetu na hatimaye kupenyezwa katika miili ya watu hasa mahasimu wa wasaka madaraka.

Inapofikia madaktari wanamwambia waziri mkuu Mizengo Pinda wamechoka kupokea amri kutoka kwa watawala zinazowataka kuandaa rufaa za kupeleka watu India kwa matibabu yanayoweza kupatikana nchini, ujue inawezekana pia watawala hao hao wakaamrisha ripoti wanazotaka ziandikwe kuhusu ugonjwa wa watu hao.

Ikiwa tumeruhusu mianya inayowafanya wana usalama wetu waonekane na kufanya kazi zao kana kwamba wameajiriwa na viongozi wa chama tawala, hatuna njia tena ya kukubali wala kukanusha ukweli wa madai ya Dk. Mwakyembe kulishwa sumu au kushikishwa sumu.

Mianya hiyo imeruhusu chokochoko na hisia mbaya kuwa makarani wahutasi, madereva, walinzi, wapenzi rasmi na wasio rasmi, wapishi na wasaidizi wa karibu wa viongozi wetu wanatumiwa na genge la mafisadi kuhujumu uhai wa watawala wetu na familia zao.

Hili tumelilea wenyewe; litatumaliza muda si mrefu. Lakini heri litumalize sisi mapema, kabla halijaangamiza taifa letu lisilo na hatia.

Ikiwa sumu ya hatari ya namna hiyo kama inavyosemwa katika mitandao ya kijamii imeingizwa nchini, taifa zima haliko salama. Hao wanaotuhumiwa kuingiza sumu hiyo nchini, watashindwaje kupenyeza sumu hiyo katika miundo mbinu ya maji, viyoyozi vya maofisini, mahospitalini, makanisani katika sakramenti za komunio, na hata katika viwanda vya vinywaji ili kuangamiza watu wengi zaidi?

Serikali inapokaa kimya bila kushughulikia suala la hatari namna hii, ni sawa na kusema kuwa sumu hiyo ya hatari tayari imeanza kufanya kazi katika mwili wake.

Kama si kweli kuwa Dk. Mwakyembe alilishwa au kushikishwa sumu, hili nalo ni baya na chafu sawa tu na kama angelishwa au kushikishwa.

Kwa kiongozi wa serikali ngazi ya waziri, pamoja na marafiki zake wa kisiasa, kutunga, kuzusha na kueneza jambo la hatari namna hiyo, haiwezi kusameheka. Kuzusha kupewa sumu si mchezo wa kitoto au kichekesho cha vunja mbavu.

Ni jambo la hatari linaloweza kuviweka vyombo vya usalama katika hali ya hatari huku raslimali tusizokuwa nazo zikitumika ili kulinda usalama wa vongozi wetu dhidi ya tishio lisilokuwapo. Uzushi wa namna hii unaweza kutumiwa na maadui wa ndani na nje kutimiza malengo yao mabaya kwa sababu tu, wamepata mwanya kupitia uzushi wa watu wachache wanaokaa na kujiundia maadui wasiokuwapo.

Nimesoma katika tamko la Dk. Mwakyembe alilolitoa kujibu taarifa ya jeshi la polisi na kuona kana kwamba anawatuhumu mafisadi wa Richmond, EPA na wale wa kashfa ya Rada.

Kwangu mimi, wahusika wa kashfa hizo ni maadui wa taifa zima na si maadui wa Dk. Mwakyembe peke yake.

Ni hatari kwa Dk. Mwakyembe kujifanya yeye ni taifa hata achukiwe na mafisadi wanaohujumu taifa lakini pia ni kosa la kufikiri kwa mafisadi hao kumfanya Dk. Mwakyembe kuwa ni mtu muhimu mno ambaye kama akifa, hujuma zao na matunda haramu waliyochuma yatakuwa salama.

Kinachoonekana wazi hapa ni kuwa taifa limeuziwa kesi ya ugomvi binafsi kati ya wanaoitwa mafisadi na Dk. Mwakyembe na kundi lake, na sasa serikali nzima imepooza isijue la kufanya.

Mchezo wa kuchelewa kuchukua hatua katika masuala nyeti na magumu unaigharimu serikali hii na muda si mrefu taifa litalipa gharama kubwa zaidi.

Tumefikaje hapa? Historia ni ndefu mno. Watanzania hatutunzi kumbukumbu na vyombo vyetu vya habari havitusaidii kutunza kumbukumbu hizo. Tumekuwa watu wa kubabaishwa na jambo moja na kabla hatujajipanga kulitolea ufumbuzi, linazushwa jingine haraka ili kutondoa katika lile la kwanza. Mafisadi na serikali legevu ni wajanja wa kutumia mtindo huu ili kuwafanya watanzania wasiungane kutafuta suluhu ya matatizo yao.

Kinachofurahisha mpaka hapa ni ukweli kuwa mchezo huu sasa unawarudi waliouasisi. Mafisadi waliopoamua kuhujumu na kuharibu ushahidi walidhani yamekwisha. Dk. Mwakyembe alipoongoza Kamati Teule ya Bunge kuandaa ripoti ya nusu-ukweli alidhani anaisadia serikali, lakini sasa imemgeuka.

Aliyekuwa Spika wa Bunge, Samwel Sitta alipozima mjadala wa Richmond kwa rungu lake kuu alidhani anaisaidia serikali. Kumbe sivyo. Leo inamwona mwongo na mzushi.

Rais Jakaya Kikwete alipomtumia Dk. Mwakyembe kummaliza Edward Lowassa alidhani amemaliza kazi, lakini sasa si Dk. Mwakyembe wala Lowassa anayemwamini Kikwete.

Hata pale Kikwete alipomdanganya Lowassa akajiuzuru na kwa ahadi atamlinda na kumsafisha tayari kuwa rais wa awamu ya tano, alidhani uwongo huo ni chanjo, lakini yanayotokea sasa hata Kikwete anajuta kumdanganya swahiba wake huyo wa zamani.

Naye Lowassa alipokubali kujiuzuru ili kulinda Kikwete kwa imani ya kusafishwa baadaye alidhani anasaidia chama chake na serikali, lakini sasa ameona alivyogeuka kuwa adui wa kila mtu na asiyeweza kuaminiwa na yeyote. Je, tunajifunza nini?

Kwa uchungu, tukubali taifa liwe la kwanza na mengine yafuate baadaye. Bila kukubali ukweli huu, sumu tutakula sana, suluhu haitapatikana. Ni heri kujitenga na mtandao na serikali ya namna hiyo. Atakayefanya hilo, atasema na kusikilizwa hata kama hatapata madaraka.

Vinginevyo, tutazusha sana kupewa sumu, lakini hakuna suluhu itakayopatikana.  

tutikondo@yahoo.com
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: