Sakata la Posho mbili: Hakuna atakayepona


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 04 November 2009

Printer-friendly version
Wapo waliochota hadi pensheni mbili kwa mkupuo
Ni Kigoda, Ngwilizi, Mapuri na Mbatia
Mbunge wa Handeni, Dk.  Abdallah Kigoda

SAKATA la posho mbili kwa wabunge linatishia kumlipua hata Rais Jakaya Kikwete na viongozi kadhaa ndani ya Chama Cha Mapinduzi na serikali.

Iwapo hilo litatokea, juhudi za Katiku Mkuu Ikulu, Philemon Luhanjo za kukaba koo wabunge kuwa wanakula posho mara mbili, zitakuwa zimemwingiza bosi wake katika tuhuma nzito.

Taarifa ambazo zimefikia MwanaHALISI zinasema hoja ya sasa siyo tena watunga sheria kulipwa posho wakati tayari wamelipwa na Bunge, bali kuna waliolipwa pensheni mara mbili.

“Hilo la posho ni ‘chamtoto,’ kuna waliokula pensheni mara mbili katika chama na serikali na bado wako madarakani na hawaguswi,” kimeeleza chanzo cha habari hizi.

Luhanjo anadaiwa kuandika waraka kwa taasisi za umma, ikiwa ni pamoja na halmshauri za miji na wilaya, akielekeza kuwa wajumbe wa kamati za bunge wanaotembelea ofisi hizo wasilipwe posho “kwa kuwa tayari wamekwishalipwa na bunge.”

Hatua ya Luhanjo ndiyo imevaliwa njuga na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Edward Hoseah ya kutaka kuwahoji wabunge juu ya kupewa malipo ugenini wakati wakiwa wamelipwa na bunge.

“Hili la posho likiachwa liendelee kwa njia ya sasa inayoonekana kama kukomoana, basi litaingizwa la pensheni na matumizi mengine ya fedha za umma. Ikifikia hatua hiyo, hakuna atakayepona,” kimeeleza chanzo cha habari.

Gazeti hili limepata orodha ndefu ya viongozi ambao wamekula pensheni mara mbili – ndani ya chama na serikali lakini shutuma zimekuwa zikielekezwa kwa wabunge pindi wanapokwenda kukagua ofisi za umma.

Aidha, kwa wiki mbili sasa kumekuwa na mvumo wa taarifa kwamba hata viongozi wakuu hubeba fedha kila waendapo safari; bali wakifika waendako hukirimiwa kila kitu na wao kubaki na fedha zao bila hata kufikiria kuzirejesha serikalini.

Ni katika mazingira haya anatajwa Rais Kikwete kuwa yeye na msafara wake hubeba posho zao kila wanapokwenda safari, lakini kuna sehemu nyingi ambako hukirimiwa na wao wasitumie hata senti.

“Ndiyo. Katika hali hii, hata kama ni msafara wa rais, wahusika ambao walikirimiwa wanastahili kurejesha fedha walizopewa kwa kuwa hazikutumika,” anaeleza mmoja wa wabunge wa CCM.

Anatoa mfano wa ziara kama ile ya rais ya kwenda nchini Libya yapata miezi miwili iliyopita.

Anasema kama kwa mfano ujumbe huo ulipewa Sh. 300 milioni na huko kiongozi wa Libya Muammar Ghadaffi akawakirimu katika kila kitu, basi wahusika walipaswa kurejesha mamilioni hayo “kabla hayajazoea mifuko yao.”

Ni kawaida kwa rais kwenda safari na msafara wa watu wengi – ndani na nje ya nchi. Lakini inadaiwa kuwa, hata ndani ya nchi, wengi kama siyo wote, hukuta wanagharamiwa kila kitu na hivyo kurejea na fedha zote walizopewa bila kutumika.

Mbunge mmoja ambaye hakutaka kutajwa jina gazetini ameliambia gazeti hili, “Je, hawa Hoseah anawajua? Yeye kavalia njuga wabunge kwa kuwa walitaka awajibishwe. Nani atawajibisha waliomo katika msafara wa rais?”

Imeelezwa pia kuwa gharama hizo za malipo hufanywa pia kwa misafara wa Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), mawaziri wa Muungano, mawaziri wa SMZ, naibu mawaziri, makatibu wa CCM wa mikoa na wilaya na hata kwa wenyeviti wa CCM wa mikoa.

Taarifa zinasema hata rais wa Zanzibar au Waziri Kiongozi anapokuja Tanzania Bara kuhudhuria vikao vya CCM au serikali, hulipwa na SMZ na hutumia ndege za serikali; wakati chama hulipa posho wajumbe wa vikao.

“Ukimtaka rais wa Zanzibar kuja kukufungulia mkutano wako au semina, lazima ulipe kwa serikali ya Zanzibar Sh. 10 milioni zikiwa gharama za kumleta.

“Shilingi 7 milioni ni kwa ajili ya kukodi ndege na Sh. Sh. 3 milioni ni posho kwa ajili ya msafara wake. Lakini tunajua kwamba kule Zanzibar, serikali inagharamia baadhi ya safari zao, ndiyo maana wakati mwingine fedha za kukodi ndege zinalipwa lakini wao wanatumia ndege ya serikali,” anaeleza mtoa taarifa.

“Hata wanapokuja Dodoma au Dar es Salaam kuhudhuria mikutano ya chama, wanalipwa posho na serikali na chama kinawalipa,” anasema kiongozi mmoja wa CCM, kuthibitisha kile kinachoweza kuitwa, “hakuna atakayeokoka.”

Lakini taarifa za uhakika zinataja orodha ndefu ya viongozi wa CCM ambao tayari wamepokea pensheni katika chama na wanasubiri, au tayari waliishachukua pensheni serikalini.

MwanaHALISI imefanikiwa kupata nyaraka kadhaa zinazoonyesha na kuthibitisha kuwa wanasiasa hao na wengine, wamelipwa fedha zinazotajwa kama pensheni na chama chao, wakati huohuo wakiwa wamelipwa pensheni na Bunge.

Kwa mujibu wa taarifa, mbunge wa Mlalo Hassani Ngwilizi tayari amelipwa pensheni kwa “kukitumikia chama” chake katika kipindi hichohicho ambamo alilipwa pensheni ya bunge. Ngwilizi alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM.

Wengine waliolipwa na CCM na huku wakilipwa pensheni na Bunge, ni mbunge wa Handeni mkoani Tanga, Dk. Abdallah Kigoda. Hivi sasa wanasubiri kuchukua pensheni nyingine kutoka bungeni. 

Mbali na pensheni Dk. Kigoda na Ngwilizi walikuwa wakilipwa na CCM posho ya Sh. 40,000 kila siku ambazo walikuwa Dar es Salaam. Malipo hayo yalifanywa kwa hoja kwamba kituo cha kazi cha Ngwilizi na Dk. Kigoda kilikuwa Dodoma, kwa mujibu wa kanuni za utumishi wa CCM.

Kigoda alikuwa waziri wa nchi katika Ofisi ya Rais, Uchumi na Mipango na Ngwilizi alikuwa Waziri wa nchi ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).

Mbali na posho Kigoda na Ngwilizi walikuwa wanatumia gari la CCM na walikuwa wanalipwa madereva wao posho na chama.

Balozi wa Tanzania nchini Urusi, Jaka Mwambi amelipwa Sh. 16,320,000 zikiwa pensheni kwa kutumikia CCM.

Kwa mujibu wa nyaraka zilizopo, Mwambi aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Tanzania Bara alilipwa pensheni yake 28 Novemba 2007 kupitia hundi Namb. 062332 ya Benki ya CRDB.

Mwingine aliyelipwa pensheni na CCM na wakati huohuo akachukua pensheni bungeni, ni Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Aggrey Mwanri ambaye amelipwa Sh. 3.7 milioni. Malipo hayo yamefanyika kupitia hundi Na. 062333 katika Benki ya CRDB.

Katika orodha hiyo, yumo pia mfanyabiashara na mbunge wa Igunga, Rostam Aziz. Rostam “amelipwa” kiasi cha Sh. 3,520,000. Malipo ya Rostam yalifanyika  tarehe 10 Desemba 2007 kupitia hundi Namb. 062331 ya Benki ya CRDB.

Malipo kwa Rostam yalikuwa ni pensheni ya utumishi wa kazi ya Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Fedha na Uchumi.

Uchunguzi wa gazeti hili umeonyesha kuwa wengine waliolipwa pensheni na CCM ni aliyekuwa Katibu wa NEC, Fedha na Uchumi, Salome Mbatia na Balozi wa Tanzania nchini China, Omari Ramadhani Mapuri. Mapuri na Mbatia wote walilipwa pensheni na Bunge.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: