Sakata la Posho mbili: Tatizo sheria zisizo za haki


Bashiru Ally's picture

Na Bashiru Ally - Imechapwa 11 November 2009

Printer-friendly version
Spika wa Bunge Samwel Sitta

NAOMBA kupanua mjadala kuhusu wabunge na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) juu ya dhana nzima ya utawala wa sheria.

Lakini tatizo kubwa tulilonalo hivi sasa katika nchi yetu siyo tu ukosefu wa utawala wa sheria bali pia  ukosefu wa sheria za haki. Hili ni tatizo la kimfumo zaidi kuliko tabia za raia au utendaji wa taasisi za umma.

Hivi sasa tunalo tatizo kubwa la mgawanyo usio wa haki wa raslimali za nchi. Tatizo hili linajidhihirisha zaidi katika tofauti za kipato na pia kiwango cha umaskini miongoni mwa makundi mbalimbali. Swala la posho ni kiashiria cha tatizo la ugawaji usio wa haki wa raslimali za nchi.

Hivi karibuni Mzee Joseph Warioba alisema iwapo kima cha chini cha mshahara serikalini ni shilingi 100,000 na kima cha juu ni shilingi 5,000,000 basi upo uwezekano mkubwa wa kuzuka kwa tatizo la kimaadili na kushuka kwa tija katika utumishi wa umma.

Lakini tunaweza kuangalia maeneo mengi na kugundua kuwa mfumo wetu wa kugawa raslimali za umma siyo wa haki kiasi kwamba unafikia kiwango cha kutishia utengamano wa kisiasa wa nchi yetu.

Hali iko hivyo hata katika taasisi kama vile vyombo vya usalama, mahakama, bunge na vyuo vikuu vya umma. Tofauti kati ya mishahara, posho na marupurupu mengine baina ya watumishi wa vyeo vya chini na vyeo vya juu ni kubwa mno katika kila sekta ya umma.

Ingawa mishahara na marupurupu hayo vinalipwa kwa mujibu wa sheria, lakini sheria zinazohalalisha tofauti kubwa kiasi hicho siyo za haki. “Utawala wa sheria” wa aina hiyo ni utawala usio wa haki. Kwa hiyo tuna tatizo la kusimamia sheria ya posho na tatizo la sheria yenyewe ya posho ambayo inaruhusu mianya ya matumizi mabaya ya raslimali za umma.

Ni kweli sekta ya umma ndiyo imebeba jukumu kubwa la kutoa ajira na huduma za kijammii hapa nchini kuliko sekta yoyote. Hata hivyo hakuna mfumo wa haki wa kugawa na kusimamia raslimali za serikali.

Nafurahi kuwa tumeanza kuona ubaya wa viwango vikubwa vya posho na idadi kubwa ya vikao vya posho. Magari ya kifahari ya viongozi, safari za nje na ndani za viongozi, warsha na semina, samani katika ofisi za serikali na viongozi wa serikali, nyumba za viongozi wa serikali na takrima ni baadhi ya mijadala mikuu. 

Kwa ujumla raslimali nyingi zimeteketea serikalini kutokana na kutokuwepo mfumo bora na  wa haki wa kusimamia na kutumia raslimali za umma.

Kwa maoni yangu, tunapaswa kujadili kwa upana njia bora na ya haki ya kugawa na kusimamia raslimali za umma zilizopo. Hatuwezi tu kusisitiza utawala wa sheria ikiwa mfumo wa sheria tulionao sio wa haki.

Hili ni jukumu la bunge, kuhakikisha kuwa tunakuwa na mfumo wa sheria wa haki. Kama ambavyo wote tunataka kuwa na utawala wa sheria, tujaribu pia kurekebisha mifumo yetu ili iwe ya haki. Tukumbuke kuwa Watanzania wote tunastahili kunufaika na raslimali zetu.

Nasisitiza kuwa sio kila utawala wa sheria ni utawala wa haki.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: