Sakata la Richmond: Lowassa kikombe hakiepukiki


Edgar Lengai's picture

Na Edgar Lengai - Imechapwa 26 March 2008

Printer-friendly version
Edward Lowassa

NINAJADILI hapa baada ya kugundua jitihada zinazofanywa na baadhi ya vyombo vya habari kutaka kumsafisha aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, kuhusu uovu wa mkataba wa Richmond, baada ya mweyewe kushindwa kujitetea bungeni.

Lowassa anaijua nguvu ya vyombo vya habari ndiyo maana anavitumia baadhi yake ili kutimiza malengo yake.

Kwanza, kitendo cha kujizulu bila ya kutoa ufafanuzi kuhusu ushiriki wake katika kupewa kampuni ya Richmond kazi ya kuzalisha umeme wa dharura, kimeacha maswali mengi.

Tulitarajia alipopewa nafasi na Spika kusema, angalau angeeleza anachokijua. Hakusema, badala yake aliishia kulalamika, eti Kamati Teule ya Bunge haikumtendea haki kwa kutomhoji.

Kama msimamizi wa mchakato wa kupatikana kampuni ya kufua umeme wa dharura, angeeleza bayana kilichotokea kabla ya kutamka kujiuzulu.

Lowassa alikuwa na jukwaa zuri la kumsaidia si tu kujibu hoja za Kamati, bali pia kulieleza Bunge na wananchi kwanini hapaswi kuhusishwa na kashfa hii?

Ushiriki wake ulikuaje? Ni kweli hakuchukua rushwa? Au kwa nini alivunja maamuzi halali ya Baraza la Mawaziri? Kitu gani kilimsukuma avunje Sheria ya Manunuzi ya Umma?

Alitakiwa kusema si kutafuna maneno, kwanini aliruhusu kampuni hewa na isiyokuwa na uwezo kupewa zabuni kubwa na nyeti kama hiyo?

Katika yote haya, alikuwa anawasilisha ripoti yake kamilifu kwa bosi wake (Rais Jakaya Kikwete)? Kama ni hivyo, kwa nini alimdanganya rais hadi naye akaudanganya ulimwengu?

Mbona wakati haya yanafanyika, Lowassa na wenzake walinyamaza?

Katika mahojiano na Televisheni ya Taifa (TvT), anasema alitaka kuvunja mkataba mara mbili alipobaini Richmond ni kampuni ya kitapeli, lakini wataaalam walimkatalia.

Hili haliingii akilini hata kidogo. Hivi ni mtaalam gani wa sheria au hata mambo ya ugavi anayeweza kutetea kampuni ya kitapeli?

Au Lowassa anataka kusema hajui maana ya neno "tapeli?" Je, hajui utapeli ni kosa la jinai?

Kwanza serikali ndio ingekuwa ya kwanza kuishitaki Richmond kwa utapeli, kukaa kimya mpaka Bunge liunde Kamati Teule na ndipo hilo lijulikane, kunazidi kutuzuga.

Ripoti ya wataalam waliochunguza mikataba mingi ya kampuni za kuzalisha umeme na Shirika la Umeme nchini (TANESCO), inasema kwenye mkataba wa Tanesco na Richmond, kuna vipengele vinavyoipendelea Tanesco.

Kama ni hivyo, kwanini hakuruhusu Tanesco kujitoa katika mkataba huo baada ya Richmond kutoa taarifa za uongo kuhusu uhalali wake kisheria wakati wa kuingia mkataba na TANESCO?

Au Lowassa hajui kuwa kitendo hicho ni ukiukaji wa mkataba huo?

Kifungu 12.1(g) cha mkataba na Richmond kinasema, "Richmond itakuwa imekiuka mkataba ikitoa maelezo au taarifa zitakazothibitika ni za uongo wakati zilipotolewa na ambazo zinaathiri uwezo wa kampuni hiyo kutekeleza majukumu yake yaliyoainishwa na mkataba."

Na kwa mujibu wa masharti ya kifungu 12.3(c) cha mkataba, Tanesco ina haki ya kuuvunja kutokana na kitendo cha Richmond kuukiuka mapema.

Pia Tanesco ilikuwa na uhuru na haki ya kuvunja mkataba kutokana na kujaa kwa mabwawa yanayozalisha umeme kama inavyofafanuliwa na kifungu 12.4 cha mkataba.

"Hakuna madhara yoyote yangetokea kutokana na Tanesco kuvunja mkataba baada ya kuridhika na ongezeko la maji katika mabwawa yanayozalisha umeme."

Kifungu 4.4 cha mkataba kinatamka kuwa Richmond ilikuwa na wajibu wa kulipa fidia iwapo itashindwa kutimiza mkataba.

Lowassa atueleze hao wataalam anaodai walikuwa wakimshauri asivunje mkataba walitumia vigezo vipi?

Huyu ndiye Lowassa ambaye alipokuwa Waziri wa Maji na Maendeleo ya Mifugo aliitimua kampuni ya City Water ya Uingereza baada ya kuona ni wababaishaji, bila hata kusubiri maamuzi ya Baraza la Mawaziri? Wako wapi sasa wataalam waliomshauri?

Jambo nililogundua ni kuwa Lowassa anatafuta mtu wa kumfunga paka kengele.

Kitendo cha kuibebesha lawama Timu ya Makubaliano ya Serikali aliyoiteua mwenyewe ili kusimamia mchakato wa kupatikana mzabuni, pamoja na mawaziri wake ni kutaka kunawa mikono kama alivyofanya Pilato!

Lowassa anajikanganya kwa mambo mengi. Moja, kamati aliunda yeye na hivyo ilikuwa inawajibika kwake.

Alikuwa anapewa taarifa kila siku kuhusu mwenendo mzima wa mchakato wa zabuni ulivyokuwa unakwenda.

Pili, ni mwenyewe alisema hakuwa "mtu wa kukaa ofisini na kupokea taarifa, bali nafuatilia kwa ukaribu na kwa umakini taarifa za watendaji wangu."

Hii ina maana alikuwa anashiriki, au kujua kila hatua ya mchakato, badala ya kusuburi taarifa mezani.

Maneno 'kwa ukaribu na umakini' yanathibitisha dhahiri kuwa Lowassa alijua kila kitu na alishiriki kikamilifu mchakato wa kuipa Richmond mkataba.

Umakini na uhodari wake wa kuchapa kazi na hasa "staili" yake ya kufuatilia jambo kwa "umakini na kwa ukaribu sana," hatua kwa hatua kama anavyosema mwenyewe na Rais Jakaya Kikwete wakati anamteua, kunachochea wengi kuamini ilikuwa ni vigumu kwa mawaziri Dk. Ibrahim Msabaha na Nazir Karamagi, kufanya kazi kinyume na matakwa ya Lowassa.

Kwa msingi huo, Lowassa asingesubiri Kamati Teule iundwe ili umma ufahamu Richmond ilikuwa kampuni ya kitapeli wakati yeye alikuwa anajua siku nyingi.

Ni lazima kuna jambo alilotaka lifichwe.

Jambo jingine Lowassa na wapambe wake wanajitahidi kulijengea hoja, ni vile alivyojiuzulu.

Anasema, "?Mimi sikuwajibika kwa uzembe wangu, nimelazimika kuwajibika kwa uzembe wa wengine. Sikuwahi kuruhusu mambo yaende kienyeji. Sihusiki kabisa na suala hili kwani wapo wanaopaswa kubebeshwa mzigo huu (Msabaha, wajumbe wa GNT na watendaji wengine)."

Haishii hapo. Anasema kujizulu kwake kunafanana na kujiuzulu kwa akina Ali Hassan Mwinyi na Peter Kisumo.

Lowassa hapa anacheza karata za siasa. Anaficha ukweli. Tutofautishe kujizulu kwa mzee Mwinyi alipokuwa Waziri wa Mambo ya Ndani.

Huyu aliwajibika siyo kwa kuhusishwa na kuamuru (kushinikiza), au kusimamia, bali alijiuzulu kwa kuwa ndiye mwenye dhamana ya wizara hiyo.

Katika suala la Richmond, waliojiuzulu wametajwa kwa ushahidi wa moja kwa moja au wa mazingira.

Lowassa atajifananishaje na mzee Mwinyi wakati mazingira yao ya kujiuzulu ni tofauti kabisa?

Lakini lililo dhahiri ni kuwa Lowassa anajikanganya badala ya kujisafisha.

Mara aseme alikuwa anafuatilia kwa "ukaribu na umakini," mara hajawahi "kuruhusu mambo yaende kienyenji," mara "sihusiki kabisa na suala hili."

Kujikanganya huku, maana hawezi kusema hukuwa mtu wa kukaa tu ofisini na kusubiri taarifa ila alikuwa anafuatilia kwa ukaribu na kwa umakini, halafu hapohapo aseme hakuhusika na wala hakuruhusu mambo yaende kienyeji.

Ripoti ya PPRA na ya Dk. Mwakyembe zinasema wazi kulikuwepo ukiukwaji mkubwa na wa waziwazi wa Sheria ya Manunuzi ya Umma, na kwamba Richmond ilipata zabuni kwa mtindo wa "sandakalawe."

Leo tunaambiwa Lowassa na mkewe Regina walienda kuhiji Jerusalem kutokana na dhoruba hii.

Lakini maana ya kuhiji ni pamoja na kutubu dhambi zote na kwa vile kutubu huwa ni jambo la siri, tunaamini Lowassa atakuwa amemwambia Mungu ukweli wa dhambi zake zote (na Mungu anazijua).

Atakuwa ameahidi kutozirudia. Lakini ningefurahi aliporudi angechukua sehemu ya mali zake akawapa maskini kama watoto yatima kama alivyofanya Mfarisayo aliyemwendea Yesu na kumtaka afanye ili auone ufalme wa mbinguni!

Baada ya kueleza yote aliyofanya, Yesu akamwambia basi "kauze mali zako uwagawie maskini?."

Mwandishi wa makala haya amejitambulisha ni msomaji wa MwanaHASLII anayepatikana kwa imaili:e.lengai@hotmail.com
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: