Sakata la RICHMOND: Serikali kukwaa kisiki


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 29 September 2009

Printer-friendly version
Waziri Mkuu, Mizengo  Pinda

MVUTANO wa aina yake unatarajiwa kuibuka wiki ijayo kati ya bunge na serikali juu ya kampuni ya kufua umeme ya Richmond, imefahamika.

Baadhi ya wabunge wamejiapiza kwamba hawatakubali "maneno matupu." Mbunge wa Chama Cha Mapinduzi ambaye alikuwa hajawahi kusikika sana katika hoja hii, amesema:

"Anayefukuzwa kazi afukuzwe. Anayekimbia kabla ya kufukuzwa, kama alivyofanya Edward Lowassa, afanye hivyo mapema. Kwa hili, wala hatudanganyiki."

Wabunge wengi walioongea na gazeti hili juu ya Richmond, walisema wanatarajia serikali kuwa jasiri na kumaliza mvutano huu.

Tayari wabunge wamewasili Dar es Salaam kwa vikao vya kamati za bunge na mmoja baada ya mwingine, wanasema sharti Richmond ifikie tamati.

"Sasa ni kusuka au kunyoa, lakini sharti suala la kashfa ya Richmond limalizike," ameeleza mbunge huyo.

Kwa mujibu wa ratiba ya mikutano ya kamati za bunge, suala la utekelezaji wa maazimio 23 ya bunge juu ya Richmond, ni miongoni mwa ajenda zitakazofikishwa mbele ya kamati.

Kamati zinapitia masuala muhimu ambayo yatajadiliwa katika mkutano wa 17 wa Bunge la Jamhuri utakaofanyika baadaye mwezi huu.

"Hatutarajii serikali kuondoka tena kwa aibu mbele ya bunge. Tunataka maamuzi na ni vyema Rais Jakaya Kikwete ameahidi tayari kuleta ripoti inayokidhi matarajio ya bunge," ameeleza mbunge kutoka kanda ya Ziwa Viktoria.

Mkutano wa 16 wa bunge uliisha Agosti kukiwa na mvutano mkubwa kati yake na serikali kufuatia bunge kukataa taarifa ya utekelezaji maazimio yake iliyowasilishwa na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Adam Malima.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini, William Shelukindo aliliambia MwanaHALISI juzi, Jumatatu kuwa Kamati yake inasubiri suala la Richmond kwa shauku kubwa.

"Tunataka kumaliza suala hili. Tunataka Richmond ifike mwisho. Kuna watu wamehusika, hivyo tunataka kuona wakichukuliwa hatua zinazostahili," alisema.

Katika taarifa iliyowasilishwa na Malima, serikali ilisema ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Edward Hoseah ambaye alipewa onyo kwa "kutokuwa makini katika utoaji taarifa."

Serikali haikusema lolote juu ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika; bali ilitoa onyo kwa Katibu Mkuu wa Nishati na Madini, Arthur Mwakapungu.

Kilichoshangaza wabunge wengi na wananchi, ni kauli ya serikali kwamba imefanya uchunguzi.

Wabunge walishangaa kauli hiyo kwani miongoni mwa watuhumiwa ambao serikali inadai kuchunguza, hakuna aliyekuwa amesimamishwa kazi, kuhamishwa au kunyang'anywa madaraka wakati wa "uchunguzi."

"Utafanyaje uchunguzi juu ya mtu ambaye ni lazima umwombe faili lake ili upate taarifa. Huu sasa ni mzaha," ameeleza mmoja wa wabunge wa vyama vya upinzani.

Shelukindo amesema serikali itakuwa imefanya makosa makubwa iwapo itaendelea kulinda wale alioita, "Wahusika wakuu katika mkataba," na kwamba Bunge haliwezi kukubali kuona jambo hilo linafumbiwa macho.

"Tumeshasema mapema kwamba wapo watu wamehusika katika kufikia mkataba wa Richmond. Hawa wanajulikana na makosa yao yako wazi. Hivyo ni jukumu la serikali kuchukua hatua dhidi ya wale wanaotajwa," alisisitiza.

Alipoulizwa juu ya kauli ya Rais Kikwete kuwa Richmond imemshinda na kwamba anatafuta wapelelezi wa kimataifa ili kuja kuichunguza, Shelukindo alisema hatarajii "yanayotakiwa na Bunge kupatiwa ufumbuzi na wataalamu wa nje."

"Rais amesema, ‘serikali itakuja na taarifa nzuri. Hivyo basi, hatutarajii tena hilo lisifanyike.' "

Bunge lilirudisha serikalini kilichoitwa taarifa ya utekelezaji wa maazimio ya bunge, likitaka mamlaka ya juu ichukue hatua za kuwawajibisha maafisa waandamizi wa serikali waliohusika.

Kampuni ya Umeme, TANESCO kwa niaba ya serikali, iliingia mkataba wa kuzalisha umeme wa dharura na kampuni ya Richmond Development Company (LLC) ya Marekani hapo 23 Juni 2006.

Haikuchukua muda, iligundulika kuwa kampuni hiyo haikuwa na fedha, utaalam wala hadhi ya kuendesha mradi mkubwa wa aina hiyo na kwamba maofisa wa serikali walikuwa wameikingia kifua tu.

Ni Ripoti ya Uchunguzi ya kamati teule ya Bunge, chini ya Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe, iliyoibua uozo katika mkataba na hata kusababisha kujiuzulu kwa aliyekuwa waziri mkuu, Edward Lowassa, Februari mwaka jana.

Kufuatia taarifa ya Kamati, bunge lilitoa maazimio 23 na kuitaka serikali iyatekeleze. Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, aliahidi kuwa serikali ingeyatekeleza yote kikamilifu.

Miongoni mwa maazimio ya bunge ni kuona mamlaka inawajibisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Edward Hoseah, Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini na Kamishna wa Nishati wa wizara hiyo, Bashir Mrindoko.

Wengine ambao bunge lilitaka wawajibishwe ni wajumbe wa Timu ya Mazungumzo ya Mikataba Serikalini (GNT).

Kwa mujibu wa ratiba ya vikao vya kamati, taarifa ya utekelezaji wa maazimio ya Richmond itajadiliwa Oktoba 6 na 7 mwaka huu.

Wajumbe wa kamati ya nishati watakuwa katika mnyukano na serikali itakayokuwa inawakilishwa na Wizara ya Nishati na Madini na Ofisi ya Waziri Mkuu.

Hata hivyo, Rais Kikwete alisema mapema mwezi huu, wakati wa kujibu maswali ya papo kwa papo ya wananchi, kuwa bado kuna hatua zaidi zinazopaswa kuchukuliwa kwa maafisa wa serikali waliohusika katika mkataba wa Richmond.

Rais alisema serikali itatoa taarifa nzuri juu ya suala la Richmond katika mkutano ujao wa bunge baadaye mwaka huu.

Kauli ya rais inaonekana kulenga kukidhi matakwa ya bunge ya kutaka kuona serikali inamaliza suala la Richmond katika mkutano huo.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: