Sakata la Richmond: Sitta aachwe, abanwe Kikwete


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 17 March 2010

Printer-friendly version
Kisima cha Mjadala

KUNA viumbe viwili vya ajabu sana lakini kwa namna fulani vinafanana - kinyonga na kasuku. Kinyonga ameumbwa na uwezo wa kubadilika rangi kulingana na mazingira. Mbinu hii inamsadia katika kujihama dhidi ya aadui zake, hasa wanaomuwinda.

Kasuku ni miongoni mwa ndege wenye akili na wanaopendwa sana duniani. Kasuku aliyefundishwa vizuri aweza kurudia hata maneno elfu moja mbalimbali na kuna hadithi nyingi ya jinsi gani kasuku wamesababisha wezi wakamatwe au mtu kufumaniwa.

Kinyonga na kasuku wanafanana kwa uwezo wao wa kuigiza; kinyonga anaigiza rangi, kasuku anaigiza sauti.

Binadamu aliye kama kinyonga ni mtu asiye na masimamo. Kasuku ni mtu asiye na mawazo yake mwenyewe, bali huiga ya wengine.

Kwa mfano huu, napenda kujadili yaliyotokea bungeni siku chache zilizopita, ilipotolewa taarifa ya kufungwa kwa mjadala wa Richmond.

Swali: Je, ilikuwa sahihi kwa Bunge kuhamisha mjadala kutoka Bungeni (ambako umedumu kwa miaka kadhaa sasa) na kuupeleka Ikulu? Je, Ikulu watafanya wajibu wao ili hatimaye mjadala huu ufungwe rasmi?

Suala la Richmond lilitakiwa lishughulikiwe kwa maana ya kupokezana kwa kuachiana majukumu. Vyombo vya kuchunguza uhalifu vinafanya kazi, vyombo vya kuangalia sera na taratibu na mchakato wa kisiasa vinafanya majukumu yake, vyombo vya kuwajibishana navyo vinafanya kazi yake ili hadi mwishoni suala lingemalizika katika hali ya weledi uliotukuka na chembechembe za tuhuma za kisiasa zingekuwa na nafasi.

Kamati Teule ya Bunge ilifanya kazi yake kwa ukamilifu mkubwa na kutuletea ripoti nzuri kabisa ya kutosha. Baada ya ripoti ile kufanyiwa kazi na Bunge na Waziri Mkuu kujiuzulu pamoja na baraza la mawaziri, kilichotakiwa kufanyika ni kile kilichopendekezwa na Bunge.

Serikali ikakaidi waziwazi maagizo ya Bunge. Hii ni dharau kwa Bunge. Na wabunge wakawa waoga, bunge likageuzwa rasmi kuwa kijiwe cha wapiga soga; ukali mwingi, hawawezi kuisimamia serikali.

Sasa, mtu yeyote anayetaka matakwa ya Bunge yakamilike anatakiwa kutoa shinikizo kwa serikali, si kwa Bunge. Anatakiwa aandamane kumshinikiza Kikwete.

Hatuwezi kuwa na wakulima ambao wanataka kuangalia wengine wakilima huku wao wasubiri kupewa sifa wakati wa mavuno. Hadi sasa Rais Kikwete hajamuwajibisha yeyote kwa hiari yao kwenye suala la Richmond.

Kamati ya Shelukindo inasema hivi kuhusu malipo ya dola milioni 30,696,598 (karibu bilioni 40) kwa Dowans: “Benki Kuu ya Tanzania imerejea tena kufanya uchunguzi kuhusu suala hili.

Uchunguzi huo umeonyesha kuwa ni kweli kuwa kiasi cha US$ 4,865,000 kilicholipwa kwa Kampuni ya Dowans Holdings S.A tarehe 2 Februari 2007 kwa ajili ya usafirishaji wa mitambo ya kukodi ya umeme wa dharura kwa ndege ni zaidi ya kiasi cha US$ 30,696,598 cha gharama za awali (Mobilisation Cost) kilichoainishwa kwenye barua ya dhamana ya Benki (Letter of Credit) ya tarehe 25 Agosti 2006 na ile ya tarehe 28 Desemba 2007.”

“Kamati inampongeza Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa kuchunguza kwa umakini na kugundua kuwa malipo ya usafirishaji wa mitambo ulifanyika mara mbili, yaani kwa kutumia ndege na meli. Hivyo, Serikali iendelee kufuatilia suala hili ili fedha hizo zirejeshwe Serikalini.”

Serikali inatakiwa kurejesha fedha hizo zilizolipwa mara mbili na njia mojawapo ni kutaifisha mitambo ya Dowans! Kama ndugu yangu William Ngeleja ameweza kumtunishia msuli Zakaria Kakobe na nguzo za umeme, basi asimame ahesabiwe.

Anayetaka kuandamana aandamane mitambo ya Dowans itaifishwe. Haiwezekani tayari watu walipwe bilioni 40 kwa kusafirisha halafu watuuzie tena mitambo hiyo hiyo kwa karibu bilioni 60 nyingine - mitambo ambayo gharama yake ni chini ya milioni 25!

Kamati ya Shelukindo inasema hivi: “Serikali tayari imekwishafuta utaratibu wa kuwateuwa Makatibu Wakuu kuwa Wenyeviti wa Bodi za Wakurugenzi wa Taasisi au Wakala za Serikali (Executive Agencies) zilizo chini ya Wizara wanazoziongoza.

Kwa upande wa Watumishi wengine Waandamizi, Serikali bado inaona utaratibu huo uendelee katika baadhi ya Bodi ili kusaidia katika kusukuma na kutekeleza masuala yaliyo chini ya Wizara zao kwa Maslahi ya Taifa letu.”

Ni vema mashirika ya umma yasimamiwe na bodi huru, viongozi waandamizi waingie kwa ajili ya kutoa maelezo, taarifa au kupata maelekezo. Kuendelea kuwa na mtindo huu kunachangia sana kutokuwepo kusimamiana kunakotakiwa.

Kamati ya Shellukindo inasema: “Kamati imezingatia hatua zilizofikiwa na Serikali na inasisitiza kuwa wamiliki wa Richmond Development Company LLC wafikishwe mahakamani na Serikali itoe taarifa kwa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama.”

Mtu pekee aliyeshitakiwa katika aibu hii ya taifa, ameshitakiwa kwa kosa la kitoto na wahusika wengine wote (hata wamiliki) wako huru.

Kamati ya Shellukindo inasema: “Hatua ya kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri Mkuu pamoja na Mawaziri wawili waliowahi kuongoza Wizara ya Nishati na Madini kwa kutekeleza dhana nzima ya uwajibikaji katika suala hili linalohusu Zabuni kati ya TANESCO na Richmond development Company LLC”.

Kamati inashauri Bunge likubaliane na maelezo hayo kwa kuzingatia msingi huo wa uwajibikaji.

KULIMA:Serikali imekubali kuwa aliyekuwa Waziri Mkuu Bw. Edward Lowassa, Waziri Msabaha na Waziri Karamagi waliwajibika kwa suala la Richmond. Kwa maneno mengine, wabunge hawa hawawezi kamwe kulalamika walionewa kwani Bunge na serikali vimekubali kuwa walihusika katika suala la Richmond.

Lakini kama leo hii tunawasimamisha Mramba na Daniel Yona kwa maamuzi waliyoyafanya wakiwa madarakani na kusababisha hasara ya bilioni 11, inakuwaje leo hii hawa watatu wanaendelea kuwa huru kwa kusababisha hasara ya zaidi ya bilioni 40?

Kama duniani kuna haki, ama Mramba na Yona waachiwe au Lowassa, Karamagi na Msabaha waungane nao Kisutu. Vinginevyo, serikali inafanya usanii.

Samuel Sitta na Bunge wametimiza kazi yao, aliyeshindwa na Rais Kikwete anayekataa kuchukua hatua.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: