Sakaya: Tumetendewa unyama Urambo


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 22 June 2011

Printer-friendly version
Ndani ya Jamii
MAGDALENA Sakaya, Mbunge wa  Viti Maalumu (CUF)

MAGDALENA Sakaya, Mbunge wa Viti Maalumu (CUF) kutoka mkoa wa Tabora ameonja kadhia kubwa katika harakati za kuwasaidia wananchi wake kupata ufumbuzi wa matatizo yanayowakabili.

Alikamatwa na polisi, akabambikiwa makosa, akatiwa mahabusu katika Gereza la Urambo kuanzia Mei 28 hadi Juni 7, mwaka huu.

Humo alishuhudia ukatili wa hali ya juu kutoka kwa polisi ambao kimsingi wanapaswa kuwa watu wa kulinda amani. Alichokishuhudia katika siku kumi za mateso kimebadili kabisa mtazamo wake kuhusu vyombo vya dola na utekelezaji wa misingi ya utawala bora, haki na sheria hapa nchini.

“Nimejionea mwenyewe hali ambayo wananchi walioko mahabusu na magerezani wanaishi. Wanaishi katika maeneo ambayo hata ng’ombe watapata taabu kuishi,” anasema Magdalena katika mahojiano na gazeti hili mwishoni mwa wiki iliyopita.

Anaongeza, “Katika siku yangu ya kwanza (Mei 28) katika mahabusu ya Polisi, niliwekwa katika chumba kimoja na wanaume. Hakukuwapo na choo na watu walitakiwa kujisaidia kwenye mifuko, mbele za watu nikiwamo mimi.

“Chumba kizima kilikuwa na harufu. Hakuna magodoro na watu wanalala sakafuni. Nzi na wadudu wa aina zote wanazunguka tu katika vyumba. Kumbuka maisha hayo anaishi mahabusu ambaye bado hata hajatiwa hatiani. Huu ni utawala wa kikatili sana.”
Magdalena pamoja na wananchi 10 walikamatwa Mei 28 mwaka huu kwa madai ya kuchochea vurugu wakati wa sakata la kukamata mifugo ya wafugaji wa Urambo wanaodaiwa kufanya shughuli zao katika eneo la hifadhi ya taifa.

Tayari serikali imefungua kesi dhidi ya mbunge huyo na wenzake katika Mahakama ya Wilaya ya Urambo wakidaiwa kusababisha mkusanyiko, kuwapiga polisi kwa mawe, kutaka kunyang’anya silaha, kujeruhi polisi na kukataa kutoa taarifa polisi.

Kati ya mambo ambayo Magdalena hataweza kusahau ni siku ambayo waliomba ruhusa kwa polisi awaruhusu waende kula nje ya mahabusu hayo. Badala ya kujibiwa ndiyo au hapana, askari waliyemomba ruhusa alihoji kwa dharau; “Hivi hamjafa tu? Tunataka kwenda kuwazika!”

Kilichosababisha Magdalena na wenzake hao waombe ruhusa ni kwa vile walishindwa kula ndani ya mahabusu hiyo inayonuka kwa siku nzima ya kwanza.

“Katika siku ya pili, tukiwa tumeishiwa nguvu kabisa mimi na wenzangu, kwa sababu ya njaa na uchovu, tulimwomba askari aturuhusu tutoke nje ya mahabusu tule. Ndipo akatujibu, ‘hamjafa tu? Tunataka kwenda kuwazika.’ Hebu fikiria mtu anatoa jibu kama hilo, je kuna utawala wa sheria hapo?” anahoji.

Akisimulia tukio la kukamatwa kwao Magdalena anasema siku nne kabla ya kukamatwa, alipata taarifa wakati akihudhuria vikao vya kamati za Bunge jijini Dar es Salaam kuwa mifugo mingi ya wananchi inakamatwa na serikali wilayani Urambo.

“Nikampigia simu Mkuu wa Wilaya ya Urambo (Anna Magova) na kumuuliza kulikoni? Yeye akaniambia hana taarifa kwa vile yuko Tabora Mjini kwenye vikao. Ila akaniambia atanipigia baadaye kunipa taarifa rasmi.

“Na kweli akanipigia simu baadaye na kunithibitishia kuwa ni kweli mifugo imekamatwa. Nikamwambia si tulikubaliana mwaka jana kuwa wafugaji wasisumbuliwe hadi suluhu ya kudumu itakapopatikana? Imekuwaje tena? Mkuu wa Wilaya akaniambia nisimfundishe kazi kwani uamuzi umeshafikiwa. Ndipo nikaamua kwenda mwenyewe.

“Nilipofika Urambo, mimi na ujumbe wangu kutoka makao makuu ya chama (CUF) na wilaya ya Urambo, tulikwenda moja kwa moja kwenye Kata ya Usinge ambako wafugaji wengi walinyang’anywa mifugo yao.

“Wananchi waliposikia tumefika wakaja kutuletea malalamiko yao na sisi tukawa na kazi kubwa ya kutuliza. Wakati tukiwatuliza, mara likaja gari la polisi likiwa limejaa polisi, wakaniuliza kwa nini nafanya mkutano wa hadhara bila ya kibali?

“Nikawaambia sijaitisha mkutano wowote wa hadhara. Ni wananchi tu ndio walikuwa wananipa malalamiko yao. Ndipo tukakubaliana kuwa niende kwenye makao makuu ya kata ili nizungumze na viongozi wa serikali ya kijiji, polisi na wawakilishi wa wananchi kutafuta suluhu.

“Huko kwenye ofisi ya kata ndiko mifugo yote iliyochukuliwa na serikali ilikuwa imewekwa. Kwa hiyo tulipofika tukaambiwa ofisi imefungwa. Wakati tukihojiana kwa nini ofisi ya serikali imefungwa, polisi wakaja tena, safari hii kwa shari.

“Wakatutaka tuondoke la sivyo watatupiga risasi. Nikasema kwa nini mnataka kutumia nguvu wakati sisi tunataka suluhisho la amani? Ikapigwa risasi ya kwanza ikapita mbali. Ikapigwa ya pili ikapita karibu yangu. Karibu sana na ndipo watu walipoanza kushtuka.

“Kesi niliyofunguliwa inaendelea. Lakini watu waliopigwa na polisi hadi kutaka kuzimia ndiyo haohao waliofunguliwa kesi ya kutaka kupiga polisi. Ukimuona huyo mtu anayeshitakiwa kwa kupiga polisi utaona huruma.

“Kuna mwenzetu mmoja alipigwa sana na polisi na akawa katika hali mbaya. Ni mwanamume lakini alilia mpaka na mimi nikaanza kutokwa na machozi. Tulipopelekwa polisi naye akapelekwa badala ya hospitali. Usiku mzima alikuwa akilia kwa maumivu. Lakini askari walikuwa wakimdhihaki. Leo kafunguliwa kesi ya kupiga polisi.

“Kichekesho kilikuwa kwenye dhamana. Nilinyimwa dhamana eti kwa sababu ningeachwa ningesababisha uvunjifu wa amani. Lakini makosa yote niliyoshitakiwa hayaangukii katika makosa ambayo mtu ananyimwa dhamana.

“Hakimu akataka wadhamini wangu waje na hati za nyumba. Sasa kijijini kule utapata watu wangapi wenye nyumba zenye hati? Hata wakili wangu (Twaha Taslima) alijenga hoja kwa hakimu kuwa hata yeye hana hati ya nyumba yake iliyoko Dar es Salaam.

“Na tangu lini watu wakatakiwa kutoa hati za nyumba wakati utaratibu ni kupata wadhamini na uthibitisho wa barua kutoka kwa wenyeviti wa vijiji? Zote hizo zilikuwa njama za kunikomoa mimi, wenzangu na CUF kwa ujumla. Nchi hii haina kabisa utawala bora,” anasema.

Sakaya anatoa wito kwa serikali kufanya maamuzi ya busara na mapema kwenye kutatua migogoro ya wananchi wanaoishi kwenye maeneo yanayopakana na hifadhi kwa vile yanaweza kuzua maafa makubwa katika siku za mbele.

Anasema tatizo la ardhi linazidi kuwa kubwa kila kukicha na kama serikali itaendelea kupuuzia tatizo hilo, ipo siku nchi itaingia katika maafa makubwa ya ardhi baina ya wananchi na serikali yao.

Mbunge huyo ametoa tuhuma kwa baadhi ya viongozi na wanasiasa wa Urambo kuwa wanatumia nafasi zao kuchukua fedha kutoka kwa wafugaji wakidai kuwa watawasaidia wasifukuzwe.

“Serikali na wanasiasa (akiwataja majina) wanafaidika na hali hii ya sasa. Wanatumia nafasi zao kuomba hongo kutoka kwa wafugaji. Huu ni unyanyasaji na ni lazima ukomeshwe. Serikali ni lazima ifanye maamuzi ya haraka, anasema.

0718 81 48 75
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: