Salma Kikwete kortini


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 15 September 2010

Printer-friendly version
Salma Kikwete

SALMA Kikwete, mke wa rais anayemaliza muda wake Jakaya Mrisho Kikwete, aweza kuburuzwa mahakamani kujibu matumizi mabaya ya mali ya umma, MwanaHALISI limeelezwa.

Wakili Mabere Marando alieleza mjini Dar es Salaam jana kuwa amekuwa akipokea maombi ya watu binafsi, vikundi na asasi, vikimwomba afungue kesi dhidi ya Mama Salma kwa “matumizi mabaya ya mali ya umma.”

Mama Salma anadaiwa kutumia magari na “usafiri mwingine” wa serikali, kuzunguka nchi nzima kumpigia kampeni mume wake kwa kilichoitwa “mgongo wa kodi za wananchi.”

Wakili Marando amesema atamwandikia notisi Mwanasheria Mkuu wa serikali (AG), wakati wowote sasa, juu ya nia ya wateja wake kufungua kesi dhidi ya Salma kama sheria inavyoruhusu.

Katika kesi hiyo, Marando amesema, ataunganisha pia serikali ambayo imekuwa kimya wakati raslimali za taifa zikitumiwa nje ya utaratibu.

“Ninapanga kumburuza Salma na serikali mahakamani. Ni suala la utaratibu tu. Tutataka serikali ieleze ni kiasi gani ametumia kwa muda wote na tutaomba mahakama itamke, pale itakapomwona na hatia, kwamba fedha zote hizo zirejeshwe serikalini,” ameeleza Marando.

Alipoulizwa iwapo haihitajiki notisi ya muda mrefu kwa kesi kufunguliwa, Marando alisema anajua inahitajika notisi ya siku 90, “…lakini hili siyo suala la leo na kesho tu. Tutaweza kuendelea na kesi hata baada ya uchaguzi.”

Kauli ya Marando inaendana na taarifa za ufuatiliaji ziara za Mama Salma nchi nzima kwa kipindi cha kabla na baada ya kuanza kwa kampeni za uchaguzi wa madiwani, wabunge na rais.

Taarifa zinasema kikosi cha wafuatiliaji ambacho kimetia nanga hivi sasa mjini Musoma, juzi Jumatatu kiliendelea kunukuu nyendo za mke wa rais katika kampeni za uchaguzi za mume wake.
“Tunachukua taarifa zote za matukio, mahojiano, kupiga picha za mapokezi, mikutano na kurekodi hotuba ambazo zinatolewa katika mikutano ya ndani na ya wazi,” ameeleza mmoja wa wafuatiliaji.

Hii itakuwa kesi ya kwanza na ya aina yake kumkabili mke wa rais tangu kupatikana kwa uhuru.

Mpango wa kumshitaki First Lady kwa kumuunganisha na serikali unakuja muda mfupi baada ya mke wa Rais wa Zambia, Thandiwe Banda kuswekwa mahakamani kwa mashitaka ya aina hiyohiyo.

Mama Banda anatuhumiwa kutumia helikopta na magari ya umma kumpigia kampeni mumewe huku akigawa pesa ambazo vyanzo vyake havijaweza kuthibitishwa.

Mmoja wa wafuatiliaji wa ziara za Mama Salma amelieleza MwanaHALISI, juzi Jumatatu kuwa kuna tofauti ndogo kati ya mashitaka dhidi ya mke wa Banda na yale dhidi ya mke wa Kikwete.

Akitoa mfano, mfuatiliaji huyo amesema Mama Salma aliwasili mjini Musoma kwa ndege ya serikali, Septemba 12, Jumapili iliyopita akiwa na mlinzi wake na baadhi ya wahudumu.

Ndege hiyo ya aina ya Fokker yenye namba ya usajili 5H – TGF ni mali ya serikali. Ilikuwa na jumla ya abiria wapatao 10 ingawa ina uwezo wa kubeba abiria 48 hadi 50.

“Alikuja na ndege ya serikali. Dreva wake analipwa na serikali. Alipokewa na viongozi wa serikali. Msafara wake mkoani ulijaa magari ya serikali pia. Hayo ndiyo baadhi ya matumizi mabaya ya fedha na raslimali za umma,” ameeleza mfuatiliaji.

Miongoni mwa waliotajwa kumpokea Mama Salma, wakiwa na usafiri wa serikali, ni Mkuu wa Polisi wa Mkoa Robert Boaz, mkuu wa usalama wa mkoa na mkuu wa wilaya ya Musoma, Geoffrey Ngatuni.

Magari yaliyokuwa kwenye msafara ni pamoja na yale ya magereza, usalama wa taifa, OCD, RSO na DSO, wakati yeye, Salma alipanda katika gari aina ya VX – v8 Land Cruiser T206 BJY.

“Katika maeneo mengi tayari tumethibitisha matumizi ya rasliamli za serikali isivyohalali. Katika hili la Musoma, tunataka kuthibitisha iwapo ndege hiyo ya serikali iligharamiwa,” ameeleza mfuatiliaji.

Amesema wanachofanya ni kufuatilia ufujaji ambao unaingiza taifa katika umasikini na kuziba fursa za mamilioni ya wananchi kupata elimu, makazi bora, chakula na afya njema.

Mfuatiliaji amesema kinachosikitisha ni kwamba aliyebebwa kwa fedha za umma, kupokelewa na waajiriwa wa serikali, magari ya serikali na muda wa umma, hana ujumbe wa umma bali wake binafsi na mume wake.

Katika mikutano mingi, hasa kabla na baada ya kampeni kuanza, ujumbe wa Mama Salma umekuwa kumpeni za mume wake.

“Chukua mfano wa hapa Musoma. Alipofika Jumapili alikwenda Mwibara, wilayani Bunda. Jana (Jumatatu) alikuwa hapa. Ujumbe ni uleule - kampeni za mumewe,” ameeleza.

Mfuatiliaji amesema ujumbe wa Mama Salma ni kuchagua CCM na Kikwete; kuvunja makundi na kuwa wamoja; na kuhubiri kile anachoita “madhara ya kuchagua vyama vya upinzani.”

“Katika hali hii anatumia fedha za umma kujenga familia yake binafsi. Je, walipakodi wasio wanachama wa CCM au wasiotaka kumchagua Kikwete mwaka huu, wanafaidika vipi? Wameliwa,” anaeleza kwa sauti ya uchungu.

Gazeti lilishindwa kumpata Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Ndege za Serikali, kueleza iwapo ndege aliyotumia Mama Salma ilikuwa imekodishwa au ni bwerere.

Ofisa mmoja wa cheo cha Dispatcher wa mamlaka hiyo aliyejulikana kwa jina moja la Makuru, hata kabla ya kuulizwa swali hilo, alipogundua anayeuliza ni mwandishi wa habari, alikataa kusema lolote akidai kuwa siyo msemaji wa mamlaka.

Kwa kauli yake, Mama Salma aliwaambia wasikilizaji wake mjiniMusoma kuwa lengo la ziara yake ni kuhamasisha viongozi wa CCM kujenga umoja, kuvunja makundi, kupita kwa wananchi kuwaomba wachague CCM na Kikwete.

Alisema kama ni rushwa ilianza enzi za TANU na kwamba “Jakaya kajitahidi kwani nyumba haijengwi siku moja…wanawake watazidi kupewa mikopo…CCM ina wenyewe na itazidi kupeta.”

Kufikishwa kwa Salma mahakamani kunaweza kuleta mtizamo mpya kuhusu nafasi ya wake wa marais na majukumu yao.

Aidha, asasi za kijamii ambazo wake wa marais wanaunda mara baada ya waume zao kuingia madarakani, nazo zinaendelea kutiliwa shaka kwa madai kuwa zinakuzwa na kuneemeshwa na “urais.”

Alipoulizwa ni lini hasa ataweza kupeleka notisi ya kufungulia mashitaka Salma na serikali, Wakili Marando alijibu, “Unauliza lini? Nasema wakati wowote. Hata kesho. Hili siyo suala la kukawiza.”

Mgombea urais wa CHADEMA, Willibrod Slaa, alilaani, wiki mbili zilizopita, kile alichoita Salma kutumia raslimali za taifa kwa faida ya familia yao.

Alikuwa akitaja gharama za usafiri na matunzo kwa waliomo katika misafara yao ambayo ni ya kifamilia zaidi kuliko taifa.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: