Salva akwepa hoja, akimbilia matusi


Mtega Mustapha's picture

Na Mtega Mustapha - Imechapwa 12 January 2011

Printer-friendly version

Na Mtega Mustapha

IKULU ya Dar es Salaam imejiumauma, imejikanyaga na kwa lugha rahisi, imeshindwa kutoa majibu kwa tuhuma zilizotolewa hivi karibuni na Dk. Willibrod Slaa juu ya uhusika wa Rais Jakaya Kikwete katika kampuni feki ya Dowans.

Hali hii inatokana na wanaomsaidia Rais kushindwa kutambua kuwa ikulu ni taasisi ya umma ambayo inatakiwa kutoa maelezeo ya kina pasipo jazba kila inapotokea haja ya kufanya hivyo.

Wananchi kwa ujumla wao au kupitia wawakilishi na viongozi wao au mtu mmoja kwa upekee, wana haki ya kikatiba kupata maelezo ya kina juu ya utendaji wa viongozi wa ikulu, ambao ndio wasimamizi wa viongozi wengine wote.

Dk. Slaa alipowasilisha tuhuma dhidi ya msimamizi mkuu wa raslimali ya nchi, waliotoa majibu walitakiwa kutafakari; kupima kama fikra za Slaa zinawakilisha mawazo na hisia za wengi wa wapiga kura au ni za kwake na chama chake tu.

Hapo, wangeweza kutoa jibu linalofaa.

Hukumu ya Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICC) inayotaka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) liilipe kampuni ya Dowans Sh. 185 bilioni au Sh. 94 bilioni si jambo dogo kwa Watanzania ambao wamepandishiwa gharama za umeme katika mazingira ya kutatanisha.

Hukumu hiyo si jambo dogo kwa Watanzania wanaopata huduma duni ya umeme kwa kuwa shirika limeelemewa na madeni huku likibebeshwa mzigo wa kutekeleza mikataba ya kifisadi kama huu uliowaleta Richmond na Dowans. Ikulu haikutoa majibu kuonyesha ukweli ni upi.

Tuliambiwa na Bunge kuwa Richmond ni kampuni hewa, na mrithi wake Dowans naye ni hewa. Sasa nani analipwa pesa katika kampuni ambayo ni hewa! Sielewi ni kiasi gani waliomjibu Dk. Slaa walipima uelewa wa wananchi kuhusu ukweli huu kabla ya kuamua kujibu kwa lugha ya kashfa.

Baada ya kupatikana taarifa kwamba TANESCO inatakiwa kulipa Sh. 185 bilioni (kabla ya kupunguza hadi Sh. 94 bilioni), wananchi wengi weledi walitaka kujua inakuaje?

Walianza kuhoji inawezekanaje shirika ambalo tayari lihoi, kumudu deni wasilolisababisha? Ikumbukwe kuwa aliyekuwa Mkurugenzi mkuu wa TANESCO, Dk. Idris Rashid aliwahi kutaka kujiuzulu ila alibembelezwa na rais arudi.

Kitendo cha Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Salva Rweyemamu kutoa majibu kwa Dk. Slaa yaliyojaa kashfa, kebehi na pengine yanayokaribia kuwa matusi, kwa, kinaonyesha namna watendaji wa taasisi hiyo wasivyojua dhima yao kwa jamii waliowateua kutawala.

Kwa mtazamo wowote ule ambao Ikulu au watendaji wake binafsi wanaweza kuwanao dhidi ya Dk. Slaa, watambue kuwa majibu watakayomtolea hayampatii faida yeye binafsi bali wananchi wote wanaotaka kujua ukweli kuhusu sakata la Dowans.

Walitakiwa kupima ni kwa kiasi gani tuhuma alizotoa Dk. Slaa zinawezekana ni sauti ya wapiga kura.

Katika somo la utoaji wa hoja kwa wanasiasa, tamko hili dhidi ya Dk. Slaa limekosa hoja ya msingi kwani badala ya kujibu hoja, Salva ameamua kutukana- argumentum ad hominem.

Hii ni kasoro katika kujenga hoja - logical fallacy – kwani unadhani kwa kumtukana mjumbe badala ya kujibu hoja zake, unaweza ukamtisha na kumnyamazisha kumbe unajijengea mazingira ya kuwaonyesha watu kuwa umehusika na kwa sababu huna namna ya kujitetea unaamua kumtishia kwa matusi yule anayekushitaki. Pia unatumia kipigo, kashfa au mashataka mahakamani.

Inawezekana Dk. Slaa alikosa, iwapo kweli alikosa, au kushindwa kujenga hoja yenye maelezo na ushahidi wa kutosha kuwaridhisha Watanzania na Ikulu.

Jukumu la Ikulu lilikuwa kutoa maelezo ya kina juu ya sakata la Dowans na kujitahidi kumwonyesha kila Mtanzania kuwa Rais Kikwete hahusiki kama mshirika, lakini kama kiongozi wa nchi, alitakiwa kuwawajibisha wahusika.

Unapokuwa kiongozi, ukatuhumiwa, ukaanza kujibu wapigakura kwa matusi, unatoa msisitizo kuwa ni kweli unahusika na kashfa unayotuhumiwa. Si hivyo, itakuwa unawaogopa wahusika hasa kwa sababu za urafiki nao, uanachama katika chama chenu au ufadhili wa kifedha wanaoutoa kwenu.

Wasaidizi wa Ikulu wajue si mara ya kwanza Dk. Slaa kumtuhumu Kikwete. Alifanya hivyo Septemba 2007 alipomtaja Kikwete katika orodha ya watafuna nchi – List of Shame.

Baada ya Rais kutajwatajwa, kina Salva walipaswa  kumsafisha kwa kutoa maelezo ya kina ya namna asivyohusika lakini wakitoa maelezo ya nani wanahusika halisi na hatua gani wamechukuliwa.

Utaona kuwa kwa kukosekana mfumo mzuri wa utoaji taarifa, kila waziri alijisikia kuzungumza na wakazungumza kila mmoja alivyotaka na Rais ambaye ndiye msemaji mkuu wa serikali hakuweza kutoa tamko kuwatoa hofu wananchi.

Tunaambiwa TANESCO inaongeza kodi, katika kipindi ambacho imeamriwa kuilipa Dowans mabilioni ya shilingi na dola 50,000 za Marekani kwa Richmond. Ni nani anawatolea ufafanuzi wa yote haya?

Lakini majibu yale ya Salva pia yanaonyesha taswira halisi ya watu walioikalia ofisi. Kuwa hawana uwezo wa taaluma ya kusimamia mahusiano kati ya serikali na wapiga kura.

Wakati wajibu wa washauri wa rais ni kujenga mahusiano bora na wananchi, wataalamu hawa wanataka kumwona rais kuwa ni mtu asiyefaa kulaumiwa – above reproach!

Si kweli hata kidogo. Katiba inaruhusu au inatoa haki za msingi za kila mwanadamu kuzungumza hisia zake ilimradi kwa kufanya hivyo haathiri amani. Kama mtu anaona anaonewa, basi aombe jukwaa la kuzungumza ili kupinga aliyetuhumu kwa njia ileile isiyovuruga amani.

Haiwezekani kuwa umetuhumiwa kwa lugha ya amani, unaamka kutishia kumfunga, kumtukana mtuhumu, na kumbeza kwa kejeli za namna hiyo. Huko ni mtu kupungukiwa na mantiki.

Kwa lugha hii, Salva amethibitisha kuwa Rais anahusika ndiyo maana amekimbilia kujibu hoja za Dk. Slaa kwa matusi kama kinga. Na huko ni kuidhalilisha ikulu.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: