Salva ikulu imebaki uchi


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 12 January 2011

Printer-friendly version
Wazo Mbadala
SALVATORY Rweyemamu

SALVATORY Rweyemamu, aliyekuwa mkurugenzi na mhariri mtendaji wa Habari Corporation Ltd (HCL), ni mtu wa kuhurumiwa sana. Amepata kazi ngumu.

Kama aliomba, hakujua uzito wake na kama aliteuliwa, basi aliyemteua amemkomoa kwani amempa kazi ya kufunika kwa viganja ikulu. Nia, isibaki uchi.

Kazi aliyopewa ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, inasaliti misingi aliyosimamia kwa muda mrefu wa utendaji wake kama mwandishi makini: kufichua uozo badala ya kuuficha.

Alipokuwa mhariri mtendaji wa HCL, magazeti ya Rai na Mtanzania yalikuwa yakiibua uozo serikalini.

Ni magazeti hayo yaliyosababisha Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Dk. Hassy Kitine ajiuzulu baada ya kudaiwa kuchotewa kifisadi Sh. 60 milioni. Ni mgazeti hayo yaliyofichua rushwa katika ununuzi wa rada na ndege ya rais.

Ni magazeti hayo yaliyolaani mauaji ya watu 21 yaliyofanywa na polisi wakati wa kuzima maandamano ya wanachama wa CUF waliokuwa wanalalamikia kuporwa ushindi wao Zanzibar, Januari 26 na 27 mwaka 2001.

Salva aliongoza harakati za kupinga kusudio la serikali ya CCM kumfukuza nchini aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya HCL, Jenerali Ulimwengu. Labda ile ilikuwa.

Salva wa leo ni tofauti. Anachukia vijana aliowalea wanapomweka peupe Rais Jakaya Kikwete kwamba ana mkono katika kampuni feki ya Dowans.

Salva leo anatetea uozo, tena kwa lugha ya kukirihisha, kufitinisha, kukejeli viongozi wa siasa. Anaunga mkono wafuasi na viongozi wa CHADEMA kudundwa kwa kuandamana kudai haki yao.

Katika kukanusha tuhuma zilizotolewa na Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, hivi karibuni, Salva alisema Dk. Slaa ni mzushi wa kupuuzwa, na ni mtu hatari.

Akataka wanahabari watafiti kujua mmiliki halali wa Dowans. Siku mbili baadaye, Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja akaibuka na majina ya eti wamiliki wa Dowans.

Kinachofichwa

Baada ya Bodi ya HCL kuuza hisa zake, aliyenunua ni Rostam Aziz, mbunge wa Igunga (CCM). Kwa hatua hiyo, Rostam aliamua kuuza hisa zake katika kampuni ya Mwananchi.

Wakurugenzi wote wa HCL walikwenda wapi? Salva na Dk. Gideon Shoo walianzisha kampuni ya ushauri wa mawasiliano ya G&S Media Consultants; Ulimwengu, Johnson Mbwambo na Shaaban Kanua walishirikiana na watu wengine kuanzisha kampuni inayomiliki gazeti la Raia Mwema.

Salva akapewa kibarua, kupitia G&S, kufanya ushawishi magazeti yasiiandike vibaya kampuni ya Richmond. Ndiye aliwapeleka Uwanja wa Ndege wanahabari kushuhudia na kupiga picha mitambo ya Richmond ilipoingia nchini kwa ajili ya kufua umeme wa dharura.

Alipohojiwa na Kamati Teule ya Bunge ya Dk. Harisson Mwakyembe, alivyoifahamu Richmond, Salva alisema alipelekwa na Rostam ambaye ni rafiki wa Rais Kikwete. Hao wote, Salva na Rostam, ni kati ya watu muhimu katika kinachoitwa mtandao wa ushindi wa Kikwete.

Rostam alikuja kuwa mweka hazina wa CCM baada ya uchaguzi mkuu. Kwa vile Richmond ilianzishwa kwa baraka za ikulu na kulikuwa na mipango ya kuigeuza Dowans, Salva akaajiriwa kuwa mpiga filimbi wa Hamelini ili kuhamisha akili za watu kama mapanya.

Ifahamike, kabla ya kuwa waziri, Ngeleja aliwahi kuwa mwanasheria wa Vodacom wakati Rostam alipokuwa mmoja wa wenye hisa. Hawa ndio wanachezea akili za watu kuficha wamiliki wa Richmond/Dowans.

Usanii huo ndio umetumika kuishtaki TANESCO mahakama ya kimataifa ya uluhishi wa migogoro ya kibiashara (ICC) na kushinda kiaina na sasa inataka ilipwe Sh. 185 bilioni. Walipoona wananchi wamechachamaa malipo yamepunguza hadi Sh. 94 bilioni.

Jiulize, kama ICC ilisema fidia ni Sh. 94 bilioni kwa nini walipandisha hadi Sh. 185 bilioni? Kwa nini Rostam amepewa mamlaka ya kisheria – Power of Attorney – kukinga mgawo huo wakati siku zote anadai hahusiki na Dowans? Kwa nini rais anayetuhumiwa yuko kimya wakati hadhi yake inachafuliwa?

Bunge limesema Richmond ni feki na Dowans ni feki, lakini ikulu imeng’ang’ania Dowans walipwe. Hata kama Salva atakejeli watu, ajue wazi Dowans imebeba anguko la kisiasa kwa Kikwete.

0
Your rating: None Average: 4 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: