Sasa naitwa Ridhwani - Kikwete Nyaronyo Kicheere


Nyaronyo Kicheere's picture

Na Nyaronyo Kicheere - Imechapwa 13 July 2011

Printer-friendly version
Ridhwani Kikwete

NIMEGUNDUA kwamba watu hawafanikiwi kwa bahati tu, bali hupata bahati na mafanikio kulingana na majina wanayopewa au majina wanayojichagulia.

Ukipewa jina baya usishangae ukipata balaa. Mathalani ukiitwa Kamanda utakuwa kamanda kweli maishani mwako. Ukipewa au kujiita Tajiri huwezi kuwa maskini maishani mwako. Na ukiitwa Msomi utajitahidi kusoma angalau kufika chuo kikuu.

Nami nimeamua kuitwa Ridhwani-Kikwete Nyaronyo Kicheere ili nipate bahati kama Ridhwani Kikwete na niishi kama anavyoishi Ridhwani Kikwete. Kwa maneno mengine Uridhwani Kikwete ni cheo au nafasi kwangu mie.

Nimechagua Uridhwani Kikwete na siyo Ujanuari Makamba, Umakongoro Nyerere, Ubeno Malisa, au Unape Nnauye kwa sababu maalumu. Sababu ya mali. Unapokuwa Ridhwani Kikwete unakuwa na bahati ya jina na mali.

Kwanza kabisa unapokuwa Ridhwani Kikwete unapata bahati ya kuwa mahali sahihi kwa wakati mwafaka. Unapata taarifa za matukio na matarajio ya kufanyika mambo mapema kuliko wengine kwa sababu unakuwa jirani zaidi na wakubwa watoa maamuzi.

Watu wenye uwezo na bahati zao wanajipendekeza na kujipitishapitisha kwako ili wawe jirani na duru za siasa na watoa maamuzi. Kwa hiyo, unapokuwa Ridhwani Kikwete na unasoma sheria usishange kuitwa na makampuni mbalimbali ya sheria kukuomba ukafanyie mafunzo kwa vitendo. Bahati ilioje.

Kwa hiyo, unapokuwa Ridhwani Kikwete, si ajabu ukawepo mahali kwenye kampuni ya wanasheria inayounda kampuni ya kitapeli itakayopata bahati ya kuchota mabilioni ya shilingi ndani ya benki ya umma.

Si wote wanaopata bahati ya kuwapo mahali zinapoundwa kampuni kama za Deep Green ambazo baadaye huchota mabilioni BoT. Hii ni bahati kubwa kwani lazima utaammbulia tu chochote angalau kidogo. Ndiyo maana nimeamua kuitwa Ridhwani-Kikwete Nyaronyo Kicheere.

Pili, unapokuwa Ridhwani Kikwete unakuwa rafiki wa wenye mali na ambao watashirikiana nawe kutafuta mali. Si ajabu, kwa hiyo, ukiwa Ridhwani Kikwete ukapata mali nyingi kama vile kampuni kubwa ya malori yanayosafiri Zambia, Malawi, Rwanda, Burundi na hata Kongo ya Kabila.

Majuzi nikiwa na rafiki yangu wa Dar es Salaam ambaye ni dereva wa malori ya mafuta, yale ‘masemi tela’ niliambiwa kuwa bosi wao aliwatembelea. Nilipouliza bosi wao ni nani, jibu lilikuwa rahisi sana. “Ni Ridhwani Kikwete, kwani wewe hujui?”

Akaendelea, “Wewe ulidhani bosi ni yule Mchaga, yule Mchaga ni boya tu. Mwenye mali pale ni Ridhwani Kikwete bwana. Yule mtoto ni tajiri wa kutupwa.” Mimi sikuwa na la kujibu kwa sababu huyo Mchaga anayesemwa simfahamu ingawaje nafahamu hayo malori yana mwenyewe ila sikujua mwenyewe aweza kuwa Ridhwani.

Hoja ni kwamba kama kweli Ridhwani kapata kampuni hiyo ya malori au kama kweli kapata malori kadhaa ambayo yanafanya biashara kupitia kampuni hiyo ya malori basi ni kwa kuwa yeye ni Ridhwani Kikwete. Bila hivyo asingeweza kuwa na malori hayo kwa umri wake. Ndiyo bahati hiyo ya Uridhwani Kikwete ninayoiwania mimi.

Tatu, unapokuwa Ridhwani Kikwete unakuwa na ruhusa au kibali cha kuingilia uchaguzi wa klabu ya mpira uipendayo kama vile Yanga. Nasikia uongozi wa sasa wa Yanga uliwekwa madarakani au ulichaguliwa kwa shinikizo la Ridhwani.

Niliwahi kuona hati ya madai iliyoandaliwa kupelekwa mahakamani kupinga uchaguzi wa klabu ya Yanga uliopita kwa madai kwamba uliingiliwa na Ridhwani Kikwete kwa kutoa hotuba iliyomdhalilisha mpinzani mmojawapo naye kwa hasira akajitoa. Shauri hilo halikufika popote kwa kuhofia au kuheshimu jina la Ridhwani Kikwete.

Sasa kwa vile mimi ni shabiki wa Simba, nikishakuwa Ridhwani-Kikwete Nyaronyo Kicheere nitakuwa na haki na bahati ya kuingilia uchaguzi wa Simba na kutoa hotuba ya kumkandia Ismail Aden Rage ili ajitoe na kumwachia mgombea ninayempenda mimi.

Kwa sababu ya jina langu la Ridhwani-Kikwete Nyaronyo Kicheere sitahojiwa wala kushitakiwa popote kama vile ambavyo malalamiko ya wagombea waliojitoa kwenye uchaguzi wa Yanga kwa sababu ya vituko vya Ridhwani hayakupelekwa popote.

Si hilo tu, jambo la nne, unapokuwa Ridhwani Kikwete unakuwa na haki na bahati ya kuingilia uchaguzi wa viongozi ndani ya umoja wa vijana wa chama chenu. Nasikia uchaguzi wa viongozi wa sasa wa Umoja wa Vijana wa chama tawala uliathiriwa na shinikizo la Ridhwani.

Mie sikuwapo lakini waliokuwapo na watu wenye kujua mambo wananiambia kuwa Ridhwani aliingilia kampeni na uchaguzi huo na kuhakikisha watu aliowataka yeye wamechaguliwa. Wengine wamesema hata kuondolewa mwenyekiti wa UVCCM Hamad Masauni Yusufu wa Zanzibar kulishinikizwa na Ridhwani.

Nani asiyependa bahati kama hiyo ya kuingilia chaguzi ziwe za vilabu vya mpira au ndani ya umoja wa vijana na usifanywe chochote kwa sababu ya jina lako la Ridhwani Kikwete? Hilo ndilo jina ninalolitaka mimi.

Na tano, unapokuwa Ridhwani Kikwete unakuwa na haki na bahati ya kuhudhuria vikao vya chama chenu na kutoa kashfa kwa viongozi walio madarakani au wastaafu na usifanywe chochote na wazazi wako, chama chenu wala kuhojiwa na Jamhuri.

Hata kauli potofu kama “rais ajae hatatoka kanda ya kaskazini” haiwezi kukemewa kama imetolewa na mwenye jina la Ridhwani Kikwete. Maana yake ni kwamba unapokuwa Ridhwani Kikwete unapata bahati ya kuambiwa safari hii rais ajae atatoka kanda gani miaka minne kabla ya uchaguzi! Nani asiyependa bahati hii?

Kwa sababu hizo zote, mimi Nyaronyo Mwita Kicheere wa Tungi, Kigamboni Dar es Salaam nimeamua kubadili jina na kuitwa Ridhwani-Kikwete Nyaronyo Kicheere.

Ili kutekeleza azma hiyo nimewasiliana na wakili wangu Juma Thomas, ambaye ameandaa waraka ambao nitaupeleka kwa Msajili wa nyaraka pale ghorofa ya pili ya jengo la Wizara ya Ardhi Magogoni Dar es Salaam nikimtaka asajili jina langu jipya. Waraka nilioandaa ni kama ifuatavyo:

“Kwa hati hii, mimi niliyetia saini yangu hapa chini, ambaye awali nilifahamika kwa majina ya Nyaronyo Mwita Kicheere, Nyaronyo Kicheere na Nyaronyo M. Kicheere, leo hii nayakana na kuyaacha kabisa majina hayo na kuanzia leo kuanza kuitwa, kufahamika na kutumia jina la Ridhwani-Kikwete Nyaronyo Kicheere; na kutokana na kubadilika jina langu, natoa tamko kwamba nitatumia mara zote na siku zote katika nyaraka zote, hati zote na maagizo yote kwa maandishi katika mashitaka, madai na mienendo na katika shughuli na manunuzi na katika hafla zozote zile nitatumia jina langu la Ridhwani-Kikweete Nyaronyo Kicheere.

Na sasa nawaamuru na kuwaomba watu wote kunifahamu na kuniita kwa jina langu la Ridhwani – Kikwete Nyaronyo Kicheeere, nami nayaacha na kuyakana majina yangu ya awali ya Nyaronyo Mwita Kicheere, Nyaronyo Kicheere na Nyaronyo M. Kicheere kuanzia leo Jumatano 13 Juni 2011.

0
Your rating: None Average: 4.7 (3 votes)
Soma zaidi kuhusu: