Sawa, uchaguzi Zanzibar uahirishwe


Ndimara Tegambwage's picture

Na Ndimara Tegambwage - Imechapwa 27 January 2010

Printer-friendly version
Gumzo

MAAFA makubwa yaja Zanzibar. Hii ni iwapo watawala – Bara na Visiwani – watakuwa vichwa ngumu na kupuuzia ushauri wanaopewa.

Kengele imelia. Ujumbe wake ni kwamba tayari hali ni mbaya kwa mujibu wa mazingira ya uchaguzi na kwamba kwa Zanzibar kuingia uchaguzi mkuu mwaka huu, itakuwa inatafuta maafa badala ya neema.

Ni hivi: Uchaguzi uahirishwe. Hoja kuu za kuandaa mazingira muwafaka zitafakariwe vizuri na kutekelezwa. Ndipo uitishwe uchaguzi mkuu.

Hapa hoja siyo kuongeza muda wa utawala wa Rais Amani Karume. Rais Karume anajua vema kuwa muda wake kikatiba umeisha. Hoja ni kusogeza mbele tarehe ya uchaguzi ili kutoa mwanya kwa marekebisho na kuandaa uwanja linganifu kwa uchaguzi wa haki.

Ushauri wa kuahirisha uchaguzi hadi hali iwekwe sawa Zanzibar hauletwi na watu kutoka nje ya nchi. Unaletwa na wakazi wa Pemba na Unguja. Hawa ndio wanajua matokeo ya chaguzi zilizopita Zanzibar na kinachofuata kila baada ya uchaguzi.

Wanaotoa ushauri ndio wanajua kinachoendelea Visiwani. Mwaka 2005, Seif Shariff Hamad aliambiwa siyo mkazi wa Pemba. Sheha (mtendaji wa Kata) alimwambia mgombea urais (Seif) kuwa hata akitangaziwa habari za kifo inasikika wakisema “popote alipo.”

Kama siyo kwa nafasi yake, juhudi kubwa na hata kukata rufaa kwa ngazi mbalimbali, mgombea urais asingepata fursa ya kupiga kura katika nchi yake.

Wangapi wasio na uzito kisiasa na kijamii katika Pemba na Unguja kama ule wa Seif ambao walinyimwa haki ya kujiandikisha kuwa wakaazi na hivyo kushindwa kuzuiwa kupiga kura? Watakuwa wengi tu.

Mwaka huohuo, Haji Mussa Jahazi Kitole, ambaye alikuwa amegombea urais kipindi kilichopita kupitia chama cha Jahazi, alikataliwa hati ya ukaazi. Ilikuwa baada ya minyukano ya muda mrefu, ndipo alifanikiwa kuandikishwa.

Wangapi wasio na kifua na king’ang’anizi cha Kitole ambao walinyakuliwa haki yao ya kuchagua viongozi wanaowataka? Watakuwa wengi tu.

Chukua mifano mingine ifuatayo inayodhihirisha ubabe wa masheha na ukimya wa watawala ngazi za juu katika kunyonga haki ya mwananchi ya kuchagua kiongozi anayemtaka.

Fikiria hili. Mwananchi ambaye amekataliwa hati ya ukaazi anabomoa nyumba yake. Anachomoa mlango. Anaubeba hadi kwa sheha. Anaonyesha ushahidi wa ukaazi.

Katika miaka ya nyuma, kila mlango wa nyumba – wa mbele au nyuma – uliwekwa kibati chenye namba ya nyumba ya mtaa au eneo. Hivyo wale ambao walikataliwa kuwa siyo wakaazi, walipeleka milango kuonyesha kuwa wao ni wakaazi na nyumba zao zina namba za mitaa husika.

Adha kubwa. Jeuri ya masheha. Rukhusa za watawala ngazi ya juu. Zoezi la kuvizia kila kura inayoonekana itakwenda kwa watawala na kuziba na hata kuua kila kura inayoonekana inaweza kwenda kwa wapinzani.

Kuna masimulizi Unguja kwamba mwenye duka; tena la siku nyingi, alikataliwa na sheha kuwa siyo mkaazi. Sheha aliyemkana mwenye duka ndiye alikuwa anakopa mchele dukani hapo kwa miaka yote ya uhai wa duka hilo.

Hili siyo tu kwamba lilileta kero mtaani, lakini lilionekana pia kuwa kashfa kubwa kwa utawala wa eneo hilo na kwa ngazi ya wilaya hata taifa ambao walikuwa wanafumbia macho vitendo vya unyang’anyi wa haki ya mtu binafsi.

Hebu angalia sheha huyu. Anataka kuoa. Anamtuma mzee mmoja jirani, mwandani, kwenda kufanya posa. Wakati wa kujiandikisha kupata hati ya ukaazi, sheha anamwambia aliyemposea mke kuwa hatambui ukaazi wake.

Chukua mfano wa imam anayeswalisha msikitini Tomondo, Unguja kila siku – asubuhi, mchana na jioni. Sheha wa eneo hilo huswali humo na hukutana na imam huyo wakati wote.

Siku ya kuandikisha wakaazi Sheha anamwambia imam kuwa hamfahamu kuwa ni mkazi wa Unguja. Anamkatalia hati ya ukaazi hadi minyukano ya muda mrefu.

Wangapi wamenyimwa au kunyang’anywa ukaazi hadi wapiganie kwa nguvu zao zote? Wangapi wameshindwa kupambana? Wangapi wamekata tamaa? Wangapi wameamua kupuuzia kujiandikisha mradi hawajahamishwa majumbani mwao? Bila shaka ni wengi.

Mfumo huu wa usajili umekuwa ukitumika kuwanyima au kuwanyakua wananchi haki yao ya kupiga kura.

Katika mazingira ya Zanzibar, ambako idadi ya wapigakura ni ndogo, kura moja ina thamani kubwa. Kwa hiyo wizi, unyang’anyi au hila za kupoteza haki ya mtu, ni kosa lisilostahili kusameheka.

Visiwani, kwa makusudi au kwa bahati mbaya, sheha amejitwisha au ametwishwa madaraka makubwa na maamuzi yaliyopitiliza kiasi cha kumfanya atoe maamuzi ambayo hata rais hawezi kuyatoa akanyamaziwa.

Kwenye hili la wizi na ujambazi wa kisiasa kwa njia ya kunyang’anya wananchi haki ya ukaazi, ongeza mwenendo wa serikali kwa miaka yote tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini.

Kuna ushahidi kwamba katika uchaguzi wa kwanza wa 1995, chama cha upinzani – Chama cha Wananchi (CUF) kilishinda. CCM ililalamika. Wataalam ndani ya CCM wakawakemea wenzao walioangua kilio.

Waliwaambia wanyamaze. Wakanyamaza. Wakateuliwa wataalam wa “kuangalia upya” kura na wataalam wakatangaza baadaye kuwa CCM ndiyo mshindi. Upinzani ukakaa kimya.

Mwaka wa uchaguzi uliofuata ulikuwa wa mazingaombwe ya aina yake. Kura zimepigwa. Askari, kwa maagizo ya watawala, wakavamia vituo. Wakachukua masanduku ya kura. Wakayaficha. Siku 14 baadaye ndipo inatangazwa kuwa CCM imeshinda. Upinzani ukalalamika na hatimaye kukaa kimya.

Uchaguzi uliofuata, askari wakatandazwa Visiwani. Vitisho kila mahali. Juu ya vitisho wakaongeza mbinu chafu za siku zote. Kwingine watawala wakazuia upinzani kufanya kampeni kwa madai kuwa “wananchi wameishaamua wanamtaka nani.”

Huu ndio ubakaji hasa wa haki za wananchi. Katika Afrika, isipokuwa chini ya tawala za kijeshi, hilo lilitendeka Tanzania peke yake na hadi sasa hakuna kwingine ambako wamevunja rekodi ya serikali ya CCM ya kuua haki ya raia. Wamebakia “Nambari Wani” katika uhalifu usiomithiulika.

Mbali na yote hayo, kuna Tume ya Uchaguzi ambayo chini yake watawala wametenda wapendavyo. Ni tume ya rais. Inatarajiwa kufanya kwa mujibu wa mapenzi ya rais na wenzake. Inahitaji mabadiliko makubwa.

Makubaliano yaitwayo “muafaka” yamefanywa mara tatu. Mara zote serikali imeshindwa kuyatekeleza. Badala yake imeyatumia kama njia ya kupumulia baada ya kukabwa koo kwa muda mrefu.

Hekima iliyowatembelea wahusika hivi sasa haipaswi kuachwa ipotelee katika ulafi wa kisiasa wa mtu binafsi au chama.

Sheria na Katiba ya Zanzibar, vyote vinahitaji marekebisho ili kutoa mwanya kwa uhuru na haki ya Mzanzibari. Hata watawala wanajua kuwa Wazanzibari wamekuwa wavumilivu na uvumilivu una mwisho.

Unapojitokeza upenyo wa kuleta mabadiliko; inapotokea akili na hekima vikawatembelea watawala, angalau mara chache na hata kwa muda mfupi, hapana budi kuchukua hatua za kurekebisha yale ambayo, kwa muda mrefu, yamekuwa kikwazo kikubwa kwa haki na ustawi wa watu na jamii nzima.

Leo kuna hoja ya kuahirisha uchaguzi mkuu Zanzibar hadi hali ya kisiasa na kiutawala iwekwe sawa. Hili linaweza kuchukua muda maalum kama itakavyopangwa na wadau.

Hili lisionyeshwe kuwa ni kutaka kumpa Rais Karume muda zaidi wa kutawala Zanzibar. Lakini kiini cha kuchanganya kuahirishwa kwa uchaguzi na kuongezwa kwa muda wa utawala wa rais wa sasa, kimetokana na mbinu za kufanya kazi za viongozi wa CUF na CCM Zanzibar.

Hakuna andishi au tamko la wazi na moja kwa amoja lililotolewa na Seif na Karume kueleza kipi kinahitajika. Majadiliano yao yamefanyika agizani na kilichojadiliwa na kukubaliwa kikawa gizani.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya aina ya Tanzania, na kwa juhudi za CCM Bara kuzima “uhuru” unaonukia, walichoona kuwa ni habari ni rais kuongezewa muda wa kutawala.

Hili limetokana na kutokuwepo taarifa mwanana za CUF na CCM Zanzibar juu ya hoja kuu ya kuahirisha uchaguzi hadi yawepo mazingira mazuri kwa maana ya huru na haki.

Bahati hubisha hodi mara moja. Ama unafungua sasa au basi! Na hiyo ndiyo hali iliyoko Zanzibar. Karume amepata fursa ya kuandika historia ya kushiriki mabadiliko ya kuleta uhuru na haki kwa mpigakura na mwananchi wa Zanzibar. Nafasi hii haiji tena.

Ama Baraza la Wawakilishi lichague mtu wa kusimamia mabadiliko yanayohitajiwa kutoka miongoni mwa wanachama wa CCM au CUF; au ateuliwe mtu nje kabisa ya vyama hivi; au Rais Karume asimamie hatua hii, hoja kuu ni kuahirisha uchaguzi wa Oktoba mwaka huu Visiwani.

Kwa uhalifu uliokwishafanywa kupitia Daftari la Wapigakura; kwa njama na mbinu ambazo zimetumika kwa miaka yote; na kwa nia njema ya kurejesha uhuru na haki ya mpigakura Zanzibar, kuna kila sababu ya kuahirisha uchaguzi.

Hatua hii ina funzo kubwa kwa Watanzania. Siku zote, na hivi sasa, viongozi wa CCM Bara na baadhi visiwani wameishi kwa woga kwamba kufanikiwa kwa CUF Zanzibar ndio kifo cha CCM Visiwani na baadaye Tanganyika.

Uhai wa raia – kwa maana ya uhuru na haki zao za kijamii – ni muhimu kuliko “uhai wa chama” unaotegemea ubabe na hata dhuluma ili chama kijirejeshe madarakani kila uchaguzi mkuu.

Zanzibar yaweza kuleta heshima kwa taifa zima. Maslahi binafsi ya CCM yaweza kuwekwa kando na maslahi ya wananchi kuwekwa mbele.

Juhudi zozote za kuzima utashi wa Wazanzibari wa kuahirisha uchaguzi na kuasisi mfumo sahihi wa uchaguzi, zitazamisha Tanzania katika kashfa; kwani ni nchi hii iliyowahi kusifika kwa kupigania haki za watu za kujiamulia mambo yao bila vikwazo.

Bali kupuuza juhudi za sasa, za kujenga mazingira bora ya uchaguzi, kunaweza kuleta maafa makubwa kwa Zanzibar na Tanzania nzima. Hili lisije leo. Lisije kesho.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: