Sendeka, Sendeka kigeugeu


Mwandishi Maalum's picture

Na Mwandishi Maalum - Imechapwa 15 February 2012

Printer-friendly version

MBUNGE wa Simanjiro (CCM), Christopher ole Sendeka ana ndimi mbili na sura mbili.

Tarehe 15 Novemba, mwaka jana, katika bunge mjini Dodoma, Sendeka alishambulia wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na kusema “hawajui wajibu wao.”

Alikuwa akichangia muswada wa Sheria ya Kuunda Tume ya Kukusanya Maoni Juu ya Katiba Mpya.

Wakati huo wabunge wa CHADEMA walikuwa wamesusia mjadala kwa maelezo kuwa ulikuwa na mapungufu mengi.

Lakini Alhamisi iliyopita, Sendeka yuleyule aliimwagia CHADEMA sifa kedekede na hasa mbunge wake wa jimbo la Singida Mashariki, Tundu Lissu.

Alisema uelewa mkubwa wa masuala ya sheria alionao Lissu, ndio ulichangia, kwa kiwango kikubwa, kurejeshwa kwa sheria hiyo bungeni hata kabla ya kuanza kutumika.

Kauli hii ya Sendeka ina maana ya kujikanyaga; ni kula kile ambacho awali alitema, tena kwa kauli kali na sauti ya juu, kuwa ni kibaya, kichafu na najisi.

Ili kuthibitisha sura mbili za Sendeka, tunukuu kumbukumbu mbili za bunge (Hansard); wakati akijadili muswada huo, 15 Novemba mwaka jana na ile ya Alhamisi iliyopita.

Aliyosema Novemba

“Mheshimiwa spika, … taifa letu linapata fursa nyingine na ya pekee ya kuandika upya katiba yake…yako mambo ambayo hayana mbadala.

Amani katika nchi yetu haina mbadala; umoja wa kitaifa hauna mbadala, uwepo wa Watanzania na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hauna mbadala... (makofi).

Nilitarajia sana wabunge wa Bunge hili wangekuwa wa kwanza kutambua hili, maana nje ya Tanzania hakuna bunge la Tanzania.

Nje ya Tanzania unaweza kuwa na bunge la Tanganyika, unaweza kuwa na bunge la Zanzibar, mnaweza mkapasuka mkaenda vipande mkawa na bunge la Simanjiro, bunge la Singida, bunge la Manyara, lakini si bunge la Tanzania.

Kama Bunge la Tanzania mnapaswa kuanzisha mchakato utakaowapa Watanzania katiba mpya na si vinginevyo (makofi).

Mheshimiwa Spika, nasema hili kwa sababu watu wanataka kuharibu historia. Kwa mara ya kwanza nimemsikia msomi na mtalaam wa sheria kama anavyojiita na kama anavyotambulika, Bwana Tundu Lissu akiwalaghai na kuwadhihaki Watanzania na kudhihaki historia ya taifa letu…(makofi).

Katika hotuba yake ukurasa wa 17, Lissu anasema Mwalimu Julius Nyerere alimomonyoa uhuru wa Zanzibar kwa kuongeza orodha ya mambo ya Muungano kwenye katiba ya Muungano.

Nataka nimwombe mwanasheria huyu na mbunge mwenzetu, arudi tena darasani; ni kwa sababu, hajui sheria. Hafahamu sheria na hajui anachokisema na kukisimamia.

Hakuna namna unaweza ukamomonyoa madaraka na uhuru wa Zanzibar ndani ya Bunge hili kwa sababu ni lazima upate theluthi mbili ya Wazanzibari walioko kwenye Bunge.

Kumtuhumu Nyerere kwamba alimomonyoa uhuru wa Zanzibar, ni kumtukana Mwalimu, ni kulitukana taifa hili, ni kubeza historia ya Tanzania. Mtu huyu anapaswa kupuuzwa kwa kiwango ambacho hakina mfano (makofi).

Mheshimiwa spika, nataka nirudi tena kukumbusha historia ya taifa letu na historia ya nchi yetu…

Katika kubadilisha katiba ya Jamhuri ya Muungano, ni lazima utambue uwepo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) na uwepo wa nchi iliyokuwa inaitwa Zanzibar na uwepo wa nchi iliyokuwa inaitwa Tanganyika (makofi).

Huwezi kubadilisha katiba na kuandika katiba upya, bila wabia hawa wawili wa Muungano kuwashirikisha. Wote hawa wawili, wanakuwa na haki sawa ya kujadili juu ya umoja wao na mustakabali wa taifa lao.

Katika hili, ninamuomba tena Lissu apate tuition na sisi tuko tayari kwa ajili ya darasa hilo bila kulipwa (makofi…).”

Hiyo ndiyo sura moja ya Sendeka. Sura ya pili hii hapa. Alhamisi iliyopita, wakati akichangia katika marekebisho ya sheria hiyohiyo ambayo haijaanza kutumika, alibadili kauli.

Aliyosema Alhamisi

“Mheshimiwa spika, … kupitia bunge lako tukufu naomba kipekee nimpongeze sana Mheshimiwa Freeman Aikaeli Mbowe, mwenyekiti wa taifa wa CHADEMA, katibu mkuu, Dk. Willibrod Slaa na viongozi wa vyama vingine kwa kupeleka maoni yao kwa mheshimiwa rais (makofi).

…lakini kipekee namshukuru sana rafiki yangu mpendwa, mwanaharakati mwenzangu wa zamani, mheshimiwa Tundu Lissu, kwa hotuba yake nzuri na ya kihistoria. (makofi)

Mimi yule (Tundu Lissu) namheshimu sana kwa sababu upeo wake ni mkubwa sana katika masuala ya sheria, lakini katika msimamo wa mambo ya msingi, mheshimiwa Lissu huwezi kumdharau. Unaweza ukatofautiana naye kwenye mambo mengine (makofi).

Nirejee tena kusema, mheshimiwa Tundu Lissu nakushukuru sana kwa hotuba yako nzuri kwa niaba ya kambi ya upinzani, kwa dhati ya moyo wangu kabisa (makofi).

Kwa hiyo, nataka niseme ninaunga mkono hoja.  Lakini nitawaomba sana wabunge wenzangu bila kujali chama cha siasa mtuunge mkono katika mabadiliko haya madogo ambayo yanakusudiwa kufanywa (makofi).”

Hiyo ndiyo sura ya pili ya Sendeka na tofauti na ile ya kwanza. Hapa anahema. Anajuta. Anapalilia. Anafumbuka macho. Kama anaomba radhi. Huyu ndiye Sendeka wa Novemba 2011 na Sendeka wa Alhamisi wiki iliyopita.

Mabadiliko haya si kama ambavyo Sendeka ameeleza, bali ni matokeo ya ubabaishaji na ufisadi wa fikra uliojikita ndani ya serikali, CCM na baadhi ya wabunge wake.

Mbunge Sendeka ni mmoja wa wabunge wa CCM ambaye kwa sura ya nje amejipambanua kama mtetezi wa wanyonge na mpinzani wa ufisadi ndani ya chama chake.

Lakini ni huyuhuyu pia ambaye rekodi ya matendo yake haijipambanui kama kweli ni mtetezi wa vitendo, bali mwigizaji mahiri wa sauti ya wanasiasa mashuhuri wa taifa letu kama Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na aliyekuwa waziri mkuu, Edward Sokoine.

Tumeshuhudia Sendeka akijiunga na mafisadi kuwasakama watetezi wa haki za wanyonge hapa nchini kwa vile tu wahusika si wanachama wa chama chake.

Tumeshuhudia akihiari au kulazimishwa kwenda katika majimbo yanayogombewa na mafisadi ili kuwanadi, kwa sababu tu wanatoka CCM.

Muda wote, Sendeka ameshindwa kuelewa kuwa ndani ya CCM wamo mafisadi na wasio mafisadi; hivyo anahitaji kuweka msimamo – kupambana na ufisadi hata kama unafanywa na chama chake au mwanachama mwenzake.

Kinachoonekana wazi kwa msimamo wake tata wa sasa, ni kuwa pale anapopaza sauti kupinga ufisadi anaongozwa na chuki binafsi dhidi ya watu fulani.

Mwalimu Nyerere, ambaye Sendeka anapenda kutumia sauti yake katika kutimiza malengo yake, ni kiongozi aliyekuwa amejipambanua vema.

Aliwaadhibu, kuwafunga, kuwafukuza kazi na kuwapinga hadharani, wanachama wa chama chake waliopitishwa kugombea uongozi baada ya kujiridhisha kuwa hawakuwa na sifa.

Bali siyo rahisi kusema Sendeka anatumiwa. Hii ni kwa kuwa ana uwezo wa kujituma. Au tuseme wakati mwingine anajituma vibaya na anaweza kujimaliza kwa povu kama sabuni?

0
Your rating: None Average: 1 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: