Sera nzuri, mikakati mibovu


Flora Mhagama's picture

Na Flora Mhagama - Imechapwa 17 November 2010

Printer-friendly version

KILA linapozungumzwa suala la umaskini nchini, watu hukimbilia kutoa maelezo, majibu, tafsiri na mikakati tofauti kuhusu kuondoa umaskini.

Hiyo ndiyo sababu imekuwepo misamiati na matamko mengi kama Kilimo cha Kufa na Kupona, Maji ni Uhai, Chakula ni Afya na sasa Kilimo Kwanza.

Matamko yanakuja na kupita lakini umaskini uko pale pale.Kwanza ni umaskini wa mtu mmoja mmoja na pili umaskini wa taifa. 

Ieleweke, umaskini ni hali inayomfanya binadamu aishi maisha ya kukosa mahitaji muhimu, kama chakula, maji safi, maliwato, huduma za afya, makazi, elimu pamoja na uwezekano wa kupata habari. 

Kuhusu nchi, umaskini unapimwa kwa kuangalia idadi ya watu na kipato cha taifa hisika. Benki ya Dunia (WB) imeweka viwango vya kuonyesha umaskini. 

WB imeeleza kwamba maskini ni mtu anayeishi chini ya dola mbili na maskini wa kutupwa ni yule anayeishi chini ya dola moja. Maana hii inatumika kwa nchi zinazoendelea kama Tanzania.

Tanzania imekuwa na sera mbalimbali zinazohusiana na mkakati za kupunguza umaskini tangu uhuru mpaka leo. Mkakati mkubwa wa kuondoa umaskini ulikuwa ule wa miaka mitano, 1960 – 1964. Baada ya hapo zilifuata sera nyingine za kijamii likiwemo Azimio la Arusha la mwaka 1967.

Miaka ya 1970 Tanzania iliingia kwenye mtikisiko wa uchumi na hapo serikali ikashindwa kutoa vizuri huduma za jamii hali iliyochangia maisha ya wananchi kuwa magumu. 

Mtikisiko wa uchumi wa kipindi hicho pia ulichangiwa na vita vya Kagera vya mwaka 1978 na 1979. 

Katika miaka ya 1980 kulikuwa na jitihada mbalimbali za kuondoka umaskini. Miaka ya 1990 uchumi ulianza kuimarika na hapo serikali ilianza kuangalia jinsi ya kuimarisha huduma za jamii. 

Pia iliweza kujiwekea mikakati mbalimbali na sera za kupunguza umaskini kama Mkukuta, Mkurabita na sera nyingine nyingi. Mwaka 2009 serikali imekuja na kitu kinaitwa Kilimo Kwanza, lakini umaskini unaendelea kukua badala ya kupungua.

Tangu miaka ya 1970 tunajua Kilimo ni uti wa mgongo wa taifa hili. 

Ni kweli kilimo kinachangia kukua kwa pato la taifa, kinatengeneza ajira, kinategemewa na idadi kubwa ya watu hasa waishio vijijini kama kazi inyowapatia kipato. Lakini kilimo kimekuwa kikikua kwa kasi ndogo ikilinganishwa na shughuli nyingine za kiuchumi. 

Kwa mfano, kumekuwa na jitihada nyingi toka mwaka 2001 za kukuza kilimo. Uzalishaji umekua hadi kufikia asilimia 5.1 katika kipindi cha 2001–2005 ikilinganishwa na asilimia 3.6 kuanzia 1995 na 2000.

Hii ni tofauti kabisa na upande wa madini ambao unaonyesha kuwa uzalishaji unakua kwa kasi. Kwa mfano, mwaka 2001 hadi 2005 sekta ya madini imekua hadi kufikia asilimia 15.4.

Japokuwa sekta ya madini inaonekana imekua hakuna mchango mkubwa katika kukua kwa uchumi wa nchi kwa sababu wawekezaji wameachiwa kuondoka na kiasi kikubwa ikilinganishwa na kinachobaki nchini.

Kukua kwa uchumi ni kwa takwimu za serikali lakini hakuna maendeleo ya kiuchumi; umaskini wa kipato cha watu bado mkubwa.

Hivyo kuna umuhimu kwa serikali kuweka msisitizo katika kilimo ambacho kinachangia moja kwa moja katika pato la taifa na maendeleo ya wananchi. 

Juhudi zinahitajika ili kuimarisha ustawi, na maendeleo ya kiuchumi ya wananchi. Ili amani iendelee kuwepo lazima kuwe na hali nzuri ya kimaisha kwa watu. 

Umaskini unasababisha vitendo vya uhalifu kuzidi, umaskini unapozidi watu wanaweza kufanya jambo lolote kwani watakata tamaa na watakosa tumaini.

Umaskini unapozidi utawala wa sheria huwa shakani kwa sababu maskini watakosa haki ya kuzungumza, sauti zao hazisikilizwi; sauti za maskini hazina nguvu, maskini wanapozungumza sauti zao hazina nguvu ya kuleta mabadiliko. 

Serikali ijue umaskini unachangia kuleta mporomoko wa maadili. Kwa sababu ya umaskini watu wanakata tamaa na kuishi maisha kinyume na utamaduni wa Mtanzania.

Hivyo basi kuna umuhimu wa kuangalia vizuri sera na mikakati ya uchumi katika nchi ili iweze kupunguza makali ya umaskini wa wananchi, ili wawtu waweze kuendelea, kuwa na amani na utulivu uliopo.

Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere aliliona suala la umaskini kuwa moja ya matatizo makubwa. Kwanza alibainisha na kutambua kasha akawashirikisha wananchi katika vita ya kuondoa umaskini. 

Alisema, “Tuna maadui wakuu watatu ambao ni umaskini, maradhi na ujinga”—maadui hao wamejikita na ameongezeka adui wa tatu ufisadi uliotengenezwa na kulelewa na serikali.

<p> Mwandishi wa makala haya amejitambulisha kuwa ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma 0762861583&nbsp;</p>
0
No votes yet