Sera ya elimu bure inawezekana


Dk. Kitila Mkumbo's picture

Na Dk. Kitila Mkumbo - Imechapwa 13 October 2010

Printer-friendly version
Gumzo
Dk. Willibrod Slaa, mgombea Urais wa CHADEMA

KUNA wanaotilia shaka sera ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ya kutoa elimu bure, kuanzia ngazi ya chekechea.

Hao wanaogozwa na mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Kikwete, meneja kampeni wa chama hicho, Abdulrahman Kinana na spika wa zamani Samwel Sitta.

Wanasema nchi maskini kama Tanzania, haiwezi kutoa elimu bure. Nawambia inawezekana.

Mwaka 1995 wapinzani waliahidi kufuta kodi ya kichwa – CCM waliita kodi ya maendeleo – iliyoleta adha kubwa kwa wananchi hadi wengine kujificha porini wakikimbia kukamatwa na mgambo.

Serikali ilisema haiwezekani kuendesha serikali bila kodi hiyo. Lakini baada ya shinikizo kutoka ndani na nje ya bunge, serikali iliifuta.

Mwaka 2000 wapinzani walikuja na sera ya kufuta ada katika shule za msingi kama njia ya kuwawezesha watoto wengi kuingia shuleni.

Kama kawaida yao, CCM walicharuka tena wakidai kuwa “wapinzani wanaota.” Hata hivyo, baada ya uchaguzi wa 2000 ada katika shule za msingi ilifutwa; wakabakiza kinachoitwa leo: michango.”

Wapinzani wa elimu ya bure wametumia hoja dhaifu, kwamba kwa kufanya hivyo, serikali itashindwa kutekeleza majukumu yake mengine ya msingi.

CHADEMA inapoongelea elimu ya bure inamaanisha kufuta ada zote wanazotozwa wazazi katika shule za sekondari.

Tayari wanafunzi wa shule za msingi hawalipi ada na kwa hivyo kinadharia elimu ya msingi inatolewa bure Tanzania.

Hivyo basi, kila mwanafunzi wa shule ya sekondari anatakiwa kulipa Sh. 20,000 kwa shule za kutwa na Sh. 70,000 kwa shule za bweni.

Kwa mujibu wa takwimu za serikali mwaka 2010, idadi ya wanafunzi wa shule za sekondari za serikali walikuwa 1,401,330.

Katika shule zaidi ya 2,000 nchi nzima, shule za bweni zipo 170 zenye wanafunzi wasiozidi 120,000.

Hii inamaanisha kuwa kwa mwaka serikali inakusanya takribani Sh. 25.6 bilioni ikiwa ni ada kutoka kwa wanafunzi wa kutwa na takribani Sh. 8.4 bilioni kutoka kwa wanafunzi wa bweni.

Kwa hivyo, serikali inapata Sh. 34 bilioni ikiwa ni mapato yatokanayo na ada ya wanafunzi katika shule za serikali. Hii ndiyo fedha ambayo serikali itaikosa kwa kutekeleza sera ya elimu bure.

Kama serikali itafuta michango mingine yote ambayo wazazi wenye watoto katika shule za sekondari wanalipa, italazimika kuongeza bajeti yake kwa shule za sekondari kwa kiwango cha Sh. 40 bilioni.

Hii ndiyo kusema kuwa gharama ya kutoa elimu bure, kwa maana ya kumuondelea mzazi mzigo wa ada na michango mingine, ni Sh. 100 bilioni kwa mwaka.

Kuhusu kupanua wigo wa mapato ya kodi, CHADEMA wameweka mkazo katika maeneo mawili:

Moja, kupunguza misamaha ya kodi isiyo na tija na pili kuongeza vyanzo vya kodi ambavyo vimeanishwa vizuri katika bajeti mbadala zilizowasilishwa na kambi ya upinzani bungeni.

Wataalam wa kodi wameshauri kwa miaka mingi kuwa misamaha ya kodi isizidi asilimia moja ya pato la taifa au asilimia 10 ya makusanyo yote ya kodi.

Wanasema punguzo la kodi kwa kiwango hiki halitaathiri mazingira ya uwekezaji nchini. Lakini serikali imepuuza ushauri huu. Matokeo yake mapato mengi ya serikali yamepotea.

Kwa mfano, mwaka 2008/2009 serikali ilisamehe asilimia 2.7 ya pato la taifa – sawa na Sh. 731.3 bilioni.

Kama ingefuata ushauri wa wataalam wa kodi ingesamehe kiasi kisichozidi Sh. 270. 8 bilioni na hivyo kuokoa zaidi ya Sh. 500 bilioni.

Hivyo basi, kupunguza misamaha ya kodi pekee, kutaokoa mara tano (Sh. 500 bilioni) ya fedha ambazo zinatosha kugharamia masomo ya wanafunzi wote nchini.

CHADEMA kitatekeleza ushauri wa wataalam na kuhakikisha kuwa misamaha ya kodi haizidi kiwango cha asilimia moja ya pato la taifa. Hili limewekwa ndani ya ilani ya chama na dhamira ya viongozi.

Pili, CHADEMA imeahidi kubana matumizi ya serikali kwa kuachana na anasa.

Moja ya maeneo ambayo wamelenga kuokoa fedha ni eneo la posho.

Kwa mujibu wa vitabu vya bajeti, katika mwaka wa fedha wa 2008/09, serikali ilitenga Sh. 506 bilioni ili kulipa posho wafanyakazi wake.

Kiasi hiki cha fedha ni sawa na mishahara ya walimu 109,000, au zaidi ya theluthi mbili ya walimu wote nchini.

Katika mwaka wa fedha wa 2009/10, kiwango kilichotengwa kwa ajili ya posho kilikuwa sawa na asilimia 59 ya mishahara yote ya wafanyakazi wa serikali.

Sehemu kubwa ya posho hizi ni zile zinazolipwa kwa viongozi na maafisa katika taasisi za serikali na haziwahusu watendaji wanaofanya kazi katika mazingira magumu huko vijijini.

Katika ilani yake, CHADEMA imeahidi kupunguza kiwango cha posho hadi kufikia asilimia 15 ya mishahara wanayolipwa wafanyakazi wa serikali.

Msingi wa kukuza uwezo wa serikali kuhudumia wananchi umejengwa katika kubana matumizi ya serikali na kupanua wigo wa ukusanyaji mapato.

Katika hili, CHADEMA itapunguza ukubwa wa serikali kutoka mawaziri na manaibu mawaziri zaidi ya 40 waliopo sasa hadi 20.

Hii itasaidia kupunguza gharama za kuendesha serikali kwa zaidi ya nusu ya gharama za sasa.

Kwa hatua hii, kiwango cha posho serikalini kitapungua kutoka Sh. 506 bilioni za sasa hadi Sh. 126 bilioni.

Hapa serikali itakuwa imeokoa Sh. 380 bilioni ambazo zitatumika kwa ajili ya miradi ya maendeleo, ikiwamo uboreshaji wa shule za msingi sekondari na huduma nyingine za jamii.

Kwa hatua mbili tu za kupunguza misamaha ya kodi na kupunguza posho zisizo na tija kwa viongozi na maafisa wa serikali, serikali itaokoa Sh. 880 bilioni.

Hii ni mifano miwili kati ya mingi ambayo serikali makini ya CHADEMA inaahidi katika kutumia vizuri fedha za walipakodi kwa ajili ya maendeleo na kuboresha utoaji huduma za jamii, ikiwemo kutoa elimu bure.

CHADEMA haijakokotoa fedha zitakazookolewa kwa kupunguza ukubwa wa baraza la mawaziri na kufuta nafasi za wakuu wa wilaya.

Aidha, haijkokotoa fedha zitakazopatikana kwa kutokomeza ufisadi serikalini na zitakazopatikana kwa kuimarisha mikataba ya madini.

Kwa hiyo, utaona kuwa kwa kutumia mifano michache niliyoitoa hapo juu, tatizo sio ukosefu wa fedha katika kutoa elimu bure na huduma nyingine za jamii.

Tatizo ni ukosefu wa utashi wa kisiasa, ukosefu wa upeo, uadilifu na umakini.

Mwandishi wa makala hii ni mhadhiri katika Idara ya Saikolojia ya Elimu na Taaluma za Mitaala, Chuo Kikuu cha Dar es Salaa. na mjumbe wa Kamati Kuu (CC) ya CHADEMA. Anapatikana kwa simu:. 0754 301908, imeili: kitilam@yahoo.com
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: