Sera ya Kitabu kimoja: Daraja la maarifa finyu


Rutashubanyuma Nestory's picture

Na Rutashubanyuma ... - Imechapwa 25 February 2009

Printer-friendly version

SERA ya “kitabu kimoja” kwa ajili ya kufundishia shuleni inasukumwa na viongozi wachache walioko makao makuu ya Wizara ya Elimu.

Lengo lao ni kuteka nyara maamuzi yaliyokuwa yanafanywa na walimu wakuu katika kuchagua vitabu vinavyofaa kufundishia.

Hili la kitabu kimoja ni mfano wa matatizo ya taifa ambalo linalea ugonjwa wa kuwalundikia madaraka warasimu wachache.

Walimu wakuu walioko mikoani wanaelewa vizuri matatizo yanayowasibu wao na wateja wao na hivyo huwa kwenye nafasi nzuri ya kubuni mikakati bukheri ya kudhibiti matatizo hayo.

Kumekuwa na mawazo kuwa vitabu vingi vinawavuruga wanafunzi hivyo kama wizara ikipitisha sera ya kitabu kimoja basi matatizo kama hayo yatakuwa yamedhibitiwa.

Hiyo ni “danganya toto” kwa kuwa hakuna kitabu cha aina yoyote kinachoweza kuutendea haki mtaala wa kipindi chochote.

Kila kitabu ni sawa na ile riwaya ya “Vipofu sita” waliokuwa wanampapasa tembo na kulingana na eneo ambalo wasioona wamegusa, basi kila mmoja alitoa hisia zake juu ya maumbile ya tembo.

Aliyegusa mguu wa tembo alidai kwa nguvu zote kuwa tembo ni sawa na mchi wa kinu wa kutwangia. Yule aliyebahatika kugusa sikio alipayuka kuwa tembo ni sawa na ungo. Aliyemshika mkia aligangamala kuwa tembo ni sawa na nyoka.

Hoja ya sera ya kitabu kimoja inapwaya kwa sababu ya dhana yake potofu kuwa yupo mtunzi wa kitabu ambaye atakamilisha matakwa ya mtaala wote.

Mtunzi wa namna hiyo hajazaliwa na kila mwandishi anachojaribu kufanya ni kuchokonoa tu hamu ya wanafunzi ili wajiendeleze wenyewe kielimu; lakini hawezi kwa kitabu kimoja kuwapa wanafunzi ujuzi wote uliopo kwenye mtaala.

Hivyo, kuwawekea mipaka wanafunzi wetu katika kujiendeleza kupitia “sera ya kitabu kimoja” ni kuwadumaza kimaarifa. Viwango vya kimataifa vya kujiendeleza vinatutaka sote, angalau kwa mwezi, tuwe tunasoma wastani wa vitabu viwili kwenye mkondo wowote tuupendao.

Sasa mwanafunzi ambaye kazi yake ni moja tu, nayo ni kusoma, kubinywa na kitabu kimoja kwa mwaka mzima kwa somo moja; na kama anasoma masomo saba basi ni vitabu saba kwa mwaka; hapo tunamjengea daraja la ujuzi finyu ambao kamwe hautamkomboa.

Kinachotakiwa ni wizara kuandaa orodha ya vitabu visivyopungua kumi kwa kila somo kama sera ya mwongozo na kuwapa uhuru walimu wakuu kuchagua katika mwongozo huo, ni vitabu vipi vitafaa mazingira ya maeneo yao.

Vilevile katika zoezi la kuchagua vitabu vya kufundishia, sharti walimu wakuu washirikishwe kikamilifu badala ya kulazimishwa kutumia vitabu ambavyo wao, kama wadau wa Sekta ya Elimu, pengine wanaona vina hitilafu kadha wa kadhaa.

Hili ni muhimu kwani kosa moja likifanywa wizarani katika kuchagua vitabu vya kufundishia, basi litaathiri vibaya nchi nzima.

Zipo hoja kuwa vitabu vingi vinachangia katika matokeo mabaya. Hoja hizi si za kweli. Matokeo mabaya kwenye mitihani yanachangiwa sana na aina ya maswali yanayoulizwa na kwa kiwango gani yamezingatia hali halisi ya mazingira ambayo wanafunzi wetu wanaishi.

Aidha, mitihani haitokani na vitabu bali mitaala. Watunzi wa mitihani wanapaswa kutunga maswali yanayosisimua udadisi badala ya kuchochea kukariri.

Na hili halipingiki kwa kuwa vitabu vingi, licha ya kuchochea utamaduni wa kusoma, vitatoa uelewa mpana zaidi na vitazalisha watunzi lukuki na ushindani utalea ubora.

0
No votes yet