Serikali ‘inawasiliana’ na marehemu


Ndimara Tegambwage's picture

Na Ndimara Tegambwage - Imechapwa 29 February 2012

Printer-friendly version

SERIKALI imeanza utaratibu wa kuwasiliana na waliokufa. Mara hii imeanza na walimu wanaodai mafao yao.

Anayebisha amuulize marehemu. Jina lake ni Richard Mutakulembelwa. Alifariki miaka 14 iliyopita; lakini bado serikali inamwandikia barua.

Soma barua ambayo serikali – wizara yake ya elimu na mafunzo ya ufundi – ilimwandikia mwezi uliopita (Januari) ikiwa imesainiwa na T. Kagumisa kwa niaba ya Katibu Mkuu.

Katika barua hiyo Richard anaelekezwa taratizu za kufuatilia malipo yake kwa mujibu wa madai ya malimbikizo, marekebisho ya mshahara au mapunjo baada ya kupandishwa ngazi.

Kwa maelfu ya walimu wanaodai serikali, basi kifo siyo mwisho wa kudai mafao yao au mwisho wa mawasiliano na wizara yao.

Specioza Kamala (57), mke wa Richard ndiye ameonja uchungu wa aina yake. Tangu baada ya kifo cha mumewe, amekuwa akifuatilia malipo yake bila mafanikio.

“Nimeandika barua. Nimekwenda hadi wizarani Dar es Salaam. Nimepewa ahadi, ahadi, ahadi. Hatimaye nimeona wanatuma barua kwa marehemu mume wangu,” anasimulia.

“Sasa mimi sijui jinsi ya kuifikisha kwake,” anaeleza Specioza kwa sauti inayonyauka na kupotea katikati ya mchuruziko wa machozi.

Richard anayetoka kijiji cha Musibuka, Kiziba, alikuwa mwalimu katika Shule ya Sekondari Kahororo iliyoko Manispaa ya Bukoba.

Alifariki tarehe 19 Agosti 1998 katika hospitali ya Muhimbili alikokuwa akipatiwa matibabu.

Kwa mujibu wa Specioza, kabla ya kukumbwa na mauti, Richard alikuwa akidai mapunjo kwenye mshahara wake, alikuwa hajalipwa mshahara wa mwezi mmoja, alikuwa akidai marekebisho kwenye mshahara.

Kwenye madai hayo ndipo yakaongezeka yale ya nauli na gharama za kusafirisha mizigo ya marehemu.

“Jumla zikawa karibu Sh. 500,000. Wakati huo ni fedha nyingi sana kwa familia yetu,” anaeleza Specioza.

Sasa wizara inamwandikia Richard Mutakulembelwa kumweleza jinsi ya kujaza fomu na kuituma kwa Katibu Mkuu, akiambatanisha nakala ya barua ya kupandishwa na kukubali cheo; na salary slip – hati ya malipo ya karibuni kuonyesha alikuwa akilipwa mshahara.

Richard aliacha mjane na watoto watano. Justa, Audax, Edwin, Godwin na Godwill.

Specioza anayetoka kijiji cha Kantare, Bwanjai, Kiziba anasema hatatulia hadi amepata ufumbuzi wa suala hilo.

Swali: Unadhani kwanini wizara imemwandikia marehemu mume wako?

Jibu: Nadhani watu hawa siyo makini au kuna wapya ambao hawajui yaliyotokea.

Swali: Si kuna mafaili. Wanaweza kusfuatilia kilichotokea?

Jibu: Hapo sijui.

Swali: Hata mkuu wa shule Kahororo hajui mwalimu aliyekuwa anafundisha pale?

Jibu: Naye aliniambia hakuwa na taarifa juu ya yaliyotokea.

Swali: Una matumaini ya kulipwa fedha hizo?

Jibu: Ndiyo. Situlii mpaka nizipate.

Swali: Lakini leo hii kiasi hicho ni kidogo sana…

Jibu: Hichohicho. Nikipate. Ni haki yetu… (Specioza anapatikana kwa simu: 0754 636077).

Wangapi waandikiwe barua wakiwa marehemu ndipo walimu wasimame kidete kudai chao wakiwa hai?

0713 614 872, ndimara@yahoo.com
0
No votes yet