Serikali chanzo cha migomo – JK


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 14 March 2012

Printer-friendly version

RAIS Jakaya Kikwete amethibitisha kwamba serikali yake ndiyo chanzo cha malalamiko na hatimaye migomo ya madaktari iliyogharimu maisha.

Katika hotuba yake kwa “wazee” wa jiji la Dar es Salaam, ukumbi wa Diamond Jubilee, juzi Jumatatu, rais alitoa maelezo juu ya historia ya migomo hiyo.

Ama kwa makusudi, kwa staili tu au kwa kupitiwa, rais alieleza jinsi madaktari walivyokosa malipo (posho) yao stahiki kwa kipindi kirefu na hatimaye kuanza kudai kwa njia ambayo alisema haikuwa nzuri.

Karibu na mwisho wa hotuba yake, rais hata hivyo, alikemea migomo ya madaktari akisema “…athari za mgomo wa daktari ni kifo…” na akawataka kuwa wavumilivu.

Hatua kwa hatua na kwa maelezo ya kupenya, rais alisema madaktari wanafunzi hupata asilimia 80 ya mshahara wa daktari aliyeajiriwa na serikali na kwamba “fedha hizo ni kila kitu kwao.”

Akielezea matumizi ya fedha ambazo madaktari walikuwa wanadai kabla ya mgomo, katika sauti iliyoonyesha upole, Rais Kikwete alisema fedha hizo zilikuwa kwa ajili ya “…nauli, chakula, nyumba….”

Kwa uthabiti, rais alikiri kuwa malipo ya madaktari yalicheleweshwa na kwamba hili lilitokea kwa kuwa hayamo katika “fungu” rasmi la mishahara ya wizara, bali fungu la “matumizi mengineyo.”

Alisema fedha za fungu la matumizi mengineyo huweza kutumika hata mahali pa dharura au popote pale ambapo kiasi kilichotengwa kimeisha na kueleza kuwa hivyo ndivyo ilivyotokea kwa malipo ya madaktari.

Madaktari wanafunzi, baada ya kudai malipo yao bila mafanikio, walifanya mgomo na kuungwa mkono na Chama cha Madaktari (MAT) na hata madaktari bingwa.

Wauguzi nao walitoa tamko la kutaka serikali imalize mgomo huo haraka la sivyo wataungana na madaktari katika mgomo.

Shinikizo la madaktari liliongezeka pale walipohamishwa kutoka Muhimbili kwenda hospitali za manispaa za Temeke, Ilala na Kinondoni na wengine kupelekwa hospitali ya jeshi ya Lugalo.

Mgomo huo uliochukua siku 17, kuanzia 24 Januari mwaka huu hadi 9 Februari, ulisababisha usumbufu, adha na hata vifo kwa wale waliokosa huduma kwa wakati.

Katika hili, rais alisema alisikitishwa na jinsi madaktari walivyopokea uhamisho huo, akisema wengi au wote waliuchukulia kuwa adhabu wakati ilikuwa nia njema ya serikali ya kutawanya huduma kwa vile walikuwa wengi kuliko walivyohitajika Muhimbili.

Alitoa mfano mmoja aliposema aliongea na daktari bingwa aliyemwambia kuwa yeye anahitaji madaktari wanafunzi wawili tu lakini alipelekewa zaidi ya aliohitaji.

Mgomo wa pili wa madaktari ulianza tarehe 7 mwezi huu, huku madaktari, pamoja na mambo mengine, wakishikilia lazima waziri wa afya na naibu wake waondolewe wizarani kwa kuwa hawana imani nao.

Madaktari walisema Dk. Hadji Mponda na naibu wake, Dk. Lucy Nkya, wamekuwa kikwazo kwa ufumbuzi wa matatizo ya Muhimbili na huduma za afya nchini; na matatizo yanayohusu maslahi yao kikazi.

Rais Kikwete aliingilia kati mgomo huo Ijumaa iliyopita kwa kukutana na madaktari; akitaka kujua undani wa madai yao kabla ya mgomo kusababisha madhara mapya kwa jamii.

Taarifa zinasema, katika kikao chake na madaktari, kilichofanyika ikulu Dar es Salaam, rais alionyesha kukubaliana na baadhi ya madai yao, lakini alikataa wazo la kufukuza kazi mawaziri wake.

Mtoa taarifa amenukuliwa akisema, “Wakati rais akiongea kwa staili yake ya ucheshi, aliwageuzia kibao madaktari na kusema, ‘Mmenitia kitanzi. Nitashindwa yale ninayotaka kufanya.’”

Akizungumza na wazee, rais alisema mabadiliko yanaweza kufanywa, akieleza kuwa hata waziri na naibu wake wanapogombana, huweza kuwasikiliza na kumpeleka huyu huku na yule kule.

Hata hivyo, wachunguzi wa mambo wanasema, Rais Kikwete yumo katika hatua ya kufanya mabadiliko ya baraza lake la mawaziri ambamo anaweza kuwabadilisha mawaziri wa afya.

Mazungumzo kati ya rais na madaktari yalifikia makubaliano ya madaktari kusitisha mgomo na kurejea kazini ili kumpa rais kile kilichoitwa “nafasi ya kutekeleza” madai yao.

Taarifa zinasema madaktari waliharakisha kukubaliana na rais kwa sababu mbalimbali. Kwanza, kulianza kujitokeza dalili za mgawanyiko miongoni mwao.

Pili, kulikuwa tayari na shauri katika Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) lililofunguliwa na serikali na amri ya mahakama ya kazi.

Tatu, kupatikana kwa taarifa kwamba “usalama wa taifa” ulikuwa ukisambaza “propaganda chafu” kwa umma dhidi ya madaktari.  

Naye Dk. Namala Mkopi, mwenyekiti wa MAT, alithibitishia MwanaHALISI kuwa jumuiya yao ilianza “kusambaratika” na hivyo wakautumia mkutano wao na rais “ili kujipanga upya.” 

“Ni kweli madaktari walianza kugawanyika. Kutokana na hali hiyo, nasi tukaona kuwa tukubali kumpa muda rais ili ashughulikie madai yetu na kutumia kipindi hiki kujipanga upya,” ameeleza.

Ni kwa kauli hii, wachunguzi wa mambo wanasema mgomo wa madaktari haujaisha, bali umeahirishwa ili kuona iwapo serikali itaheshimu ahadi zake.

Dk. Mkopi alikataa kuingia kwa undani katika makubaliano yao na rais. Badala yake alisema, “rais alikubali kuyafanyia kazi mambo mengi ambayo tunadai.”

Alipoulizwa iwapo wanamwamini Rais Kikwete, Dk. Mkopi alijibu kwa haraka, “Hatuna shaka na rais.”

Alipong’ang’anizwa kusema watachukua hatua gani iwapo rais hakutekeleza walichokubaliana, Dk. Mkopi alisema,  “Tusubiri tuone.” Alisema, “Usiwe na haraka, amesema tumpe muda. Tumempa. Tusubiri….”

Mazungumzo hayo yalishuhudiwa na Waziri wa Nchi Ofisia ya Rais, Mahusiano ya Jamii, Steven Wasira, Waziri wa Utawala Bora, Mathias Chikawe na Mwanasheria Mkuu wa serikali, Jaji Frederick Werema.

Wengine ni Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, Katibu Mkuu Utumishi, George Yambesi na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Peniel Lyimo. 

Ujumbe wa MAT ulioongozwa na rais wa jumuiya hiyo, Dk. Mkopi, uliwasili ikulu majira ya saa tano asubuhi na mkutano uliendelea hadi saa 11 jioni.

Katika hotuba yake kwa wazee, Rais Kikwete alirudia kauli yake kuwa anatarajia “migomo hii ndiyo ya mwisho.”

Alisema mabadiliko yanawezekana; lakini akahimiza madaktari wakubali kufanya majadiliano na siyo migomo aliyosema “ni kinyume cha sheria.”

0
No votes yet