Serikali haiendi bila bakora


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 15 February 2012

Printer-friendly version
Mtazamo

SERIKALI ya Chama cha Mapinduzi (CCM) haina kawaida ya kudamka usingizini kusikiliza malalamiko ya wananchi hadi iambiwe kwa lugha ya maandamano au ichapwe bakora kama punda.

Punda, mnyama anayetumiwa na wafugaji kwa shughuli za kubeba mizigo, kuvuta mikokoteni na kuvuta jembe la plau, huwa hawezi kutembea haraka afikishe mzigo au akamilishe kazi mpaka acharazwe bakora.

Hilo ndiyo chimbuko la methali ya punda haendi bila mijeledi. Vipi serikali ya CCM?

Siku zote serikali inalalamikiwa na raia waliovunjiwa nyumba bila fidia, waliohamishwa kwa fidia ndogo, waliostaafu bila malipo (Afrika Mashariki), lakini haitatui.

Serikali inapewa malalamiko ya mishahara midogo ya wafanyakazi hususan wa sekta ya huduma kama afya na elimu, lakini inakaa kimya.

Wanafunzi wa vyuo vikuu wamelalamika sana juu ya kucheleweshewa posho za kujikimu, kumbe baadhi ya maofisa wa Bodi ya Mikopo wameziingiza kwenye miradi yao, lakini serikali inawafukuza masomo.

Madaktari walipotangaza kuwasiliana na serikali kwa lugha yenye madhara serikali ikafanya jeuri. Wabunge wa CCM wazandiki na waliofunikwa kwenye kwapa la woga eti wakajitokeza kulaani.

Jambo la ajabu wabunge haohao wanaochonga sana kulaani mgomo wa madaktari, wao walisusa kukutana na Rais Jakaya Kikwete ili kujadili kwanini ameridhia sheria ya marekebisho ya katiba ifanyiwe marekebisho hata kabla ya kuanza kutumika, tena kwa kuingiza mapendekezo ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Hawa hawajitambui. Kama wao walimgomea Rais Kikwete, akakutana na kamati tu, wanatofauti gani na CHADEMA waliomsusa Kikwete siku ya ufunguzi wa Bunge mwaka juzi? Kama huu si unafiki na uzandiki ni nini?

Mgomo ni mgomo na lengo huwa kuwasilisha ujumbe kwa mamlaka husika kupinga au kushinikiza kusikilizwa shida. Wabunge wa CCM walipopanga kutoonana na Rais Kikwete walilenga kumwambia hawakuridhishwa na mwafaka kati yake na CHADEMA.

Mzee wa Upako naye ana maneno? Eti madaktari ni wauaji. Jamani!

Mgomo wa madaktari ulipoanza katika hospitali zote za rufaa nchini, serikali iliwaambia wanachodai hawawezi kupata eti serikali haina fedha. Siku iliyofuata serikali ikatishia nyau kuwafukuza. Madhara ya uamuzi huo kila mmoja ameyaona.

Madaktari, mbali ya kuwasilisha madai yao ya posho na mishahara walikusudia kuwafumbua macho wananchi kuhusu ufisadi mkubwa katika zabuni ya nguo za wafanyakazi, lakini serikali ikaziba masikio kwa vile wanaotuhumiwa ni wateule wa rais.

Eti vazi jeupe na nadhifu analovaa daktari linaloweza kupatikana kwa bei ya chini ya Sh. 100,000 kigogo wa serikali ameiuzia serikali yake kwa Sh. 500,000 halafu serikali inamtetea. Bila mgomo ule, wananchi wangejua vipi ufisadi huu? Kwanini fisadi huyu analindwa?

Kipindi chote serikali imekuwa ikidai haina fedha za kulipa posho za nyongeza, lakini ghafla ikawaangukia na kuzipandisha.

Madaktari bingwa wamepandishiwa kutoka Sh. 10,000 hadi Sh. 25,000; madaktari wa kawaida kutoka Sh. 10,000 hadi Sh. 20,000; wengine kutoka Sh. 3000 hadi Sh. Sh. 5,000; na kutoka Sh. 5,000 hadi Sh.15,000; pia watapewa nyumba na mikopo ya magari.

Halafu serikali inaangalia uwezekano wa kupandisha mishahara kutoka Sh. 700,000 hadi Sh. 3.5 milioni kwa mwezi. Bila ya mgomo wasingeongezewa.

Hakika mgomo unalipa ndiyo maana walimu wanabipu kushinikiza walipwe malimbikizo yao haraka.

Lakini tabia ya serikali kusubiri migomo ndipo isikilize shida za wananchi mbali ya kujenga matabaka, ni hatari kwa usalama wake.

0
No votes yet