Serikali haijaonyesha dhamira


Stanislaus Kirobo's picture

Na Stanislaus Kirobo - Imechapwa 19 May 2009

Printer-friendly version

KUFICHULIWA kwa mpango wa wabunge wa Tanzania kujiongezea mishahara na posho, kumeleta zogo kubwa. Mpango huo ukifanikiwa, mshahara wa mbunge kwa mwezi utafikia Sh. 12 milioni.

Malipo hayo ni mbali na posho za vikao pale bunge linapokutana na vikao vya kamati, pamoja na masurufu mengine ambayo wamekuwa wakipata.

Maoni ya wananchi yanaonyesha kupinga malipo hayo kwa kuona hayastahili kulingana na hali ya uchumi.

Wanasema haiwezekani serikali inayotoa sababu ya uchumi duni katika kusaidia miradi ya maendeleo ya wananchi, ilipe wabunge mamilioni ya shilingi. Kama hali ya uchumi si nzuri, basi na wabunge nao waihisi kama wanavyoihisi wananchi.

Lakini ukiacha mapato ya sasa ya wabunge ambayo ni halali kisheria na kikanuni – hata kama haitangazwi rasmi – kuna taarifa za kuwapo wabunge wadanganyifu.

Hawa huchukuwa posho kila siku za vikao licha ya kutoonekana bungeni. Wabunge hawa wanatumia wenzao kutia saini katika orodha ya wabunge waliohudhuria vikao ili walipwe posho ilhali hawapo bungeni.

Lakini kwa wale wanaosema Tanzania haijakomaa katika nyanja ya utawala bora, maadili ya viongozi na watumishi wa umma, uwajibikaji na uwazi, habari kutoka Uingereza zinaonyesha tatizo hilo limekithiri huko.

Hivi sasa kuna wabunge kadhaa wanaokabiliwa na kashfa za udanganyifu na kujinufaisha. Wanawasilisha madai ya uongo au ya viwango zaidi ya halali ili kulipwa fedha haramu.

Tayari Waziri wa Sheria, Shahid Malik amejiuzulu kwa kubainika analipiwa kodi ya nyumba zaidi ya kiwango halali.

Wabunge wengine wamo matatani kwa tuhuma za mfano huo. David Chaytor na Chris Bryant wote wa Chama cha Labour, Anthony Steen na Gerald Kaufman wa Conservative.

Waingereza wametaka wabunge wote hao washitakiwe haraka mahakamani na ikibidi wanyongwe kwa kufedhehesha taifa.

Ni kashfa iliyoshusha hadhi ya serikali ya Waziri Mkuu, Gordon Brown, wa Chama cha Labour. Ameahidi kufanywa uchunguzi wa kina na kukithibitika makosa washitakiwe.

Angalau Uingereza yenye wizara maalum ya Utawala Bora, serikali inajitahidi kuchukua hatua pakitokea tuhuma. Huko ni kuwajibika kwa serikali.

Tanzania tunayo wizara kama hii inayoshikwa na Sofia Simba. Tunayo Tume ya Maadili ya Viongozi na Watumishi wa Umma inayoongozwa na Jaji Stephen Ihema.

Utendaji na uwajibikaji wake unatia shaka kiasi cha kugunwa kwa yalivyo maoni ya umma. Kuna kigugumizi kizito zinapotokea tuhuma za kashfa zinazohusu wakubwa.

Waziri Sofia Simba hivi karibuni alitoa matamshi yaliyoshtua watu yakilenga kutetea watuhumiwa wakuu wa ufisadi.

Jaji Ihema naye analaumiwa na wafanyakazi wa chini yake kuhusu matumizi mabaya ya fedha za bajeti za Tume hiyo.

Katika hali kama hii, ya kukithiri kwa kashfa za ulaji na uzito wa taasisi husika kushughulikia tuhuma, Tanzania inaweza lini kuonyesha dhamira kwa vitendo ya kukomesha ufisadi angalau kwa kiwango kidogo tu?

0
No votes yet