Serikali haitaki Katiba Mpya


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 06 April 2011

Printer-friendly version

KATIKA gazeti hili, toleo Na. 223 la 5 Januari 2011, tulichapisha uchambuzi wa Ndimara Tegambwage chini ya kichwa: “Rais Kikwete hataki Katiba Mpya.” Ndivyo imetokea katika muswada wa serikali wa “Sheria ya Marejeo ya Katiba” wa Mwaka 2011. Tunarudia makala hii kutokana na umuhimu wake.

RAIS Jakaya Kikwete hajasema kuwa anakubaliana na hoja ya kuwa na katiba mpya. Hajasema!

Kama anasema amesema, basi hajaelewa wanaodai katiba mpya wanataka nini; au ametamka maneno “katiba mpya,” lakini siyo kwamba anakubaliana na matakwa ya kuandika katiba mpya.

Ambaye bado ana mashaka na kile kinachoelezwa hapa, kuhusu tume ambayo rais ataunda ili kukusanya maoni, basi asome haya yafuatayo ambayo yametoka kinywani mwa Jakaya Mrisho Kikwete.

Amesema, “…kuanzisha mchakato wa kuitazama upya katiba ya nchi yetu kwa lengo la kuihuisha ili hatimaye tuwe na katiba inayoendana na taifa lenye umri wa nusu karne.”

Jakaya Mrisho Kikwete huyohuyo anasema, “…baada ya kukamilisha kukusanya maoni, Tume itatoa mapendekezo yake yatakayofikishwa kwenye vyombo stahiki vya kikatiba kwa kufanyiwa uamuzi.”

Anaongeza, “Baada ya makubaliano kufikiwa, taifa letu litapata Katiba mpya kwa siku itakayoamuliwa ianze kutumika.”

Kwa kauli hii, iko wapi kazi ya kuandika katiba mpya? Haipo. Hatuioni. Tunachoona ni maneno yaliyotumika kwa muda mrefu na kuchoka, kama “mchakato.” Ni ukuti-ukuti.

Twende taratibu. Itaonekana kuwa rais hakuwa amejiandaa kusemea suala la katiba. Mvumo wa madai ya kuwa na katiba mpya ndio utakuwa umemsukuma ajitokeze 31 Desemba 2010 bila maandalizi mwafaka.

Kasi ya hoja za katiba mpya; msisitizo wa viongozi wa chama chake – wa sasa na wastaafu; mabingwa wa sheria na katiba, wanasiasa na wanaharakati, ndio walimsukuma aseme alichosema.

Uzuri wa Kikwete ni kwamba wakati mwingine hukiri ukweli; ama kwa kusema waziwazi au kwa vitendo. Juzi alizungumzia “mchakato” lakini akaonyesha kuwa hajafanya lolote isipokuwa nia ya kuwa na mchakato. Basi.

Rais alitaka kuzima kauli zilizokuwa zinaendelea kutoka mithili ya ndimi za moto. Ni Mzee Peter Kisumo, mdhamini wa CCM aliyempa nguvu wiki iliyopita.

Kisumo alisema CCM isione woga wala aibu “kuongoza mchakato wa katiba mpya.” Hivyo, bila kuwa na mchakato; bila maandalizi yoyote, rais akaishia kutoa ahadi. Hilo nalo linahitaji ujasiri. Ni kizibo.

Hata hivyo, rais hakuzungumzia kuandika katiba mpya, bali “kuhuisha” – kuipa uhai katiba iliyopo ili iendane na mazingira yake “na taifa lenye umri wa nusu karne” – miaka 50. Upya wa katiba uko wapi?

Rais anasema tume yake ikikamilisha kazi atakayoipa, itatoa mapendekezo yake. Turudi nyuma kidogo. Jaji Francis Nyalali (1992) alitoa mapendekezo ya tume yake. Serikali ilidonoa yale ambayo iliona  yanaisaidia. Mengine ikayazika.

Jaji Kisanga alitoa mapendekezo ya tume yake. Rais akachukua yale aliyohitaji; bali rais mstaafu Benjamin Mkapa alikuwa mkali kwa jaji akisema ameingilia hata eneo ambalo hakuambiwa. Mapendekezo mengine yakazikwa.

Katika mazingira ya sasa, Jakaya Kikwete atateua mtu anayemtaka, wenzake katika tume na kazi watakazofanya. Wakimaliza kazi watatoa mapendekezo. Rais atachukua yale ambayo anahitaji. Mengine atayaacha yazikwe na historia. Mchezo wa ukuti-ukuti.

Rais anazungumzia “vyombo stahiki vya katiba” ambako mapendekezo yatafikishwa. Hataji vyombo hivyo. Yawezekana anafikiri kuwa wananchi wote wanajua vyombo hivyo? Wanajua jinsi vinavyofanyakazi? Wanajua jinsi maamuzi yake yanavyoathiriwa na anayeteua tume?

Rais anasema makubaliano yatafikiwa ndani ya “vyombo” hivyo stahiki na taifa kupata “katiba mpya” na lini ianze kufanya kazi.

Kwa mtiririko wa maelezo haya, utaona kuwa rais na serikali yake hawajajiandaa kujibu hoja za wananchi juu ya katiba wala kukubaliana na umuhimu wa kuandika katiba mpya.

Rais anajaribu kurahisisha maelezo yake, aliyotoa kwa Kiswahili, kwa kutumia Kiingereza. Anasema ataunda Constitutional Review Commission.

Hii tunaweza kuita Tume  ya kuangalia, kufikiri, kutafakari na, au kupitia upya katiba. Siyo kuandika katiba mpya. Kuna tofauti kubwa kati ya kupitia kwa lengo la “kuhuisha” na kuandika katiba mpya.

Bali lugha ya mpindo-mpindo ya Rais Kikwete ina madhara makubwa. Inaduwaza baadhi ya wananchi na kuwaaminisha kuwa rais amelainika.

Kwa kulenga au bila kulenga, lugha hii inapandikiza shaka miongoni mwa wananchi. Wale ambao watakuwa wamesadiki kuwa rais amekubaliana na madai ya katiba, basi wataona wanaoendelea kudai kuandika katiba mpya kuwa ni, ama wapuuzi au wakorofi.

Lakini pia lugha hii inalegeza misuli, na hata kupumbaza baadhi ya wanasiasa wa upinzani ambao wameanza kupaparika kwa vineno dhaifu kwamba walichotaka ndicho rais amekubali.

Katika mazingira haya, hasa iwapo wananchi hawatapata maarifa zaidi juu ya umuhimu wa katiba mpya, Rais Kikwete na CCM watapata jukwaa kubwa la kisiasa.

Kwanza, watachelewesha hata kile wanachoita “mchakato” wa kufanya wanachotaka hadi wakati mwafaka kwao kwenda katika uchaguzi.

Pili, watatumia karata ya katiba katika chaguzi zao, kwani watapita wakiwaambia wananchi kuwa wapinzani walitaka katiba tukawapa; sasa wameshindwa kuitumia au kuitambua.

Chama Cha Mapinduzi kama kilivyo na viongozi wake, hakina nia wala uwezo wa kukubaliana na hoja ya kuandika katiba mpya inayozingatia haki na matakwa ya wananchi.

Hii ni kwa sababu chama hiki kimezaliwa, kukulia na sasa kinazeekea kwenye matumizi ya katiba iliyosheheni vikwazo na pengine kuhalalisha ukandamizaji, ambayo kuondolewa kwake ndio utakuwa mwisho wake.

Chama Cha Mapinduzi kimetawala, katika maeneo mengi, kwa kutegemea mitaji miwili mikuu: ujinga – ukosefu wa maarifa na ujuzi wa mambo mbalimbali – na umasikini.

Mtaji mwingine mkubwa ni ubabe ulioshonwa ndani ya katiba ya sasa ambayo wananchi wanataka iwekwe pembeni; iandikwe katiba mpya. Katika mazingira haya, huwezi kutegemea kiongozi wa CCM kuandika katiba mpya.

Utakachoona ni Rais Kikwete akichukulia suala la katiba kama lake binafsi au la chama chake peke yake; na bado anataka “kupitia katiba” na siyo kuwa na katiba mpya.

Kauli ya Kikwete haina tofauti na ile ya wateule wake – Celina Kombani na Jaji Frederick Werema. Ataendelea kuwa nao; na kama kuna ambaye bado anaamini kuwa waliropoka kwa kusema hawataki katiba mpya, sharti abadili msimamo.

Kazi ya kuendelea kuelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kuwa na katiba mpya, ndio sasa ipambe moto.

Lakini kama mwanasiasa mmoja alivyoniambia, kwa mazoea ya CCM, ama walazimishwe kukubali kuandika katiba mpya au kwanza waondolewe madarakani.

Ambaye bado ana shaka na hili, asubiri kuona mpango wa Rais Kikwete.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: