Serikali haiwataki, chama hakiwasaidii


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 23 March 2011

Printer-friendly version
Wazo Mbadala

BAADHI ya mnaosoma hapa mtakuwa mliona msafara mzito wa mawaziri kwenda Manyara kupitia luninga zenu au kusikia redioni.

Wengine mtakuwa mlisoma magazetini au kuwaona kwa macho wakiwa Manyara kwa mwekezaji.

Mawaziri watano waliendesha mashangingi yao kwa kasi ili ‘kuhani msiba wa mwekezaji,’ hapana, kumpa pole na kuona uwezekano wa serikali kufidia hasara aliyoipata baada ya mazao katika mashamba yake kufyekwa na mali kuharibiwa.

Matatizo haya yangeweza kuepukwa lakini serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imeyalea kwa vile sera ya siri ya serikali ni kufukarisha wazawa kwa kuwanyang’anya maeneo yao na kuwawezesha wawekezaji.

Mathalani, malalamiko ya wananchi wa eneo la Magugu, Babati mkoani Manyara ni ya muda mrefu. Wameomba mipaka inayogawa eneo la mwekezaji na kijiji iwekwe wazi, hawakusikilizwa.

Njia pekee ambayo wananchi hao waliichagua ili kuutuma ujumbe wao kwa serikali ni ghasia. Wakaharibu ekari 400 za miwa kwa kufyeka na wakachoma moto matrekta manne ya mwekezaji.

Makala hii haina lengo la kutetea uharibifu huu, lakini ni ukweli usiopingika kuwa serikali inanyanyasa na kuonea wananchi mpaka kuwafikisha mahali pa kuamua kutumia nguvu zao kupinga dhulma.

Kwa nini serikali ilikaa kimya pale wananchi walipoomba mipaka ya umiliki ardhi eneo hili ipitiwe upya? Kwa nini imemwacha mwekezaji anyanyase wananchi?

Serikali inapata faida gani wananchi wanapolialia kila siku? Na ilitaka wakulima hao wavumilie hadi lini?

Hebu turudi nyuma. Chimbuko la matatizo yote haya ni sera ya uwekezaji. Serikali ilikaribisha wawekezaji bila ya kutafuta maeneo mbadala, ikawapeleka kwenye maeneo ya wakulima, wafugaji na wachimbaji wadogo wa madini.

Mwaka 1996, kwa kivuli cha uwekezaji, serikali ilitumia mabavu kuwaondoa wachimbaji wadogo eneo la Bulyanhulu, wilaya ya Kahama, mkoani Shinyanga ili kumpisha mwekezaji ambaye ni Kahama Mining (sasa Barrick).

Wakazi wale wanalia na kuilaani serikali yao hadi leo wakikumbuka unyama, polisi waliposimamia magreda ya mwekezaji kuwafukia hai watoto wao na kupora eneo la kilimo bila ya kuwafidia kwa angalau kifuta machozi.

Mwaka huo pia serikali ilifurusha maelfu ya wachimbaji wadogo wa dhahabu katika migodi ya North Mara na Nzega.

Mamia ya walioporwa maeneo ya kujipatia riziki kwa kuchimba madini na kuendesha shughuli za kilimo wameachwa wakihangaika, wakiombaomba na kuwa vibaka na malaya.

Serikali ikahamia katika mashamba ambako kila kona aliko mwekezaji, wananchi wameporwa maeneo yao mazuri ya kilimo na malisho na kuachwa wakihangaika.

Tabia ya serikali kutotaka kutatua migogoro ndiyo kiini cha mapambano na vurugu za mara kwa mara katika maeneo waliko wawekezaji wote.

Vilevile ndiyo kiini cha wengi kuichukia serikali kwamba haina msaada kwao ila inajali zaidi maslahi ya wawekezaji na mafisadi.

Vurugu kama hizo zilitokea Kilombero, Mbarali na sasa huenda zikazuka kijiji cha Mbango, Rungwe Mashariki ambako kampuni inayojenga nguzo za umeme inakata kukokoa kwa ajili ya kupisha nguzo hizo bila ya kulipa fidia wananchi.

Serikali haikerwi na umaskini wa wananchi wake, maana kila siku inapora maeneo na kuyagawa kwa wawekezaji au kuachia mbweha na fisi kama inavyotokea kwenye pori la Kazimzumbwi. Baada ya wananchi kuhamishwa, serikali inampa eneo mwekezaji.

Inasikitisha kuona mawaziri wanakimbiza mashangingi hadi kwa mwekezaji kumpa matumaini ya fidia wakati maelfu ya wananchi waliosababishiwa umaskini na serikali inawaacha wakilia.

Mawaziri hao hawajui malalamiko ya wakazi wa vijiji vinavyozunguka migodi ya Bulyanhulu, North Mara na Nzega? Je, wamechukua juhudi zozote za kukutana na wananchi wanaozunguka shamba la mwekezaji kupata maoni yao?

Usaliti huu ndio unazidi kuchafua heshima ya serikali ya CCM. Unaweka mustakbali wa chama katika kona. Wananchi wanaona serikali haiwataki, chama hakiwasaidii, sasa maelfu wanasaka maisha bora na tumaini jipya nje ya serikali ya CCM.

0789 383 979, 0753 626 751
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: