Serikali haiwezi kupendwa kwa haya


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 11 January 2012

Printer-friendly version
Tuseme Ukweli

MTAWALA yeyote wa serikali na hata kiongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) akialikwa kutoa hotuba katika hafla yoyote ile, hata kipaimara utaona akitokwa jasho kusoma takwimu ili wasikilizaji waone maendeleo yaliyofikiwa nchini.

Atajitanua, atafuta jasho usoni, atasafisha miwani aone vizuri halafu atataja idadi ya shule, zahanati, visima vya maji, barabara na mwisho amani na utulivu. Watawala wetu, wanaamini takwimu hizo ni maendeleo yenyewe.

Utasikia; “Serikali ya CCM imefanya kazi kubwa sana. Hadi tarehe 30 Juni 2011 kulikuwa na jumla ya shule 4,266 za sekondari nchini. Kati ya hizo, shule 3,397 ni za serikali (3,308 mlizojenga ninyi wananchi, hizi ambazo wenzetu wanabeza, 89 shule kongwe za serikali) na 869 ni shule zisizo za serikali.

“Shule hizi sasa zinachukua wanafunzi zaidi ya milioni 1.6. Jamani sasa tuna vyuo vikuu 19 (vinane vya umma) na vyuo vikuu vishiriki 15 (vitatu vya umma),” atasisitiza.

Vilevile, atafafanua jinsi serikali ya CCM ilivyofanikiwa katika ujenzi wa zahanati, vituo vya afya na walivyopandisha na kuteua baadhi ya zahanati kuwa hospitali teule.

Takwimu hizi ndizo zilitumika kipindi cha maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru wa Tanganyika mwaka jana. Tangu baada ya uchaguzi mkuu wa 2010, CCM imekuwa ikitafuta kitu kinachoonekana au kinachoshikika kwa ajili ya kulazimisha wananchi watazame na kuona.

Halafu hujiridhisha kwa kaulimbiu ya “Tumethubutu, Tumeweza, na Tunasonga mbele.”

Lakini, yafuatayo ni mambo ambayo watawala hawajajiuliza: Kwa nini licha ya takwimu hizo kubwakubwa kuwahi kupatikana nchini ikilinganishwa na awamu tatu zilizopita, bado wananchi wanatazama ‘hawaoni’? Je, takwimu hizo zimechangia maendeleo yao?

Maana kama shule hizo zinatumika lakini hazitoi elimu bora, zahanati zipo hazina dawa na manesi, na majengo yaliyopo ya mabepari au mafisadi, hayo si maendeleo ya watu. Ni maendeleo ya vitu kama alivyotufundisha Mwalimu Julius Nyerere.

Kutokana na kukaidi mafundisho ya Mwalimu Nyerere watawala leo wanapata shida. Maana kama zimejengwa barabara za kuunganisha mikoa na wilaya, wajiulize kwa nini watu hawazioni?

Kama barabara na mitaa ya wilaya kuna lami, wajiulize kama wananchi hawaioni lami wanaona nini? Kama kuna ongezeko kubwa la zahanati tena zilizojengwa na wananchi wenyewe na vituo vya afya kuliko miaka iliyopita, kwanini wanabeza hayo?

Wajiulize kwa nini wananchi hawazioni shule wakati katika kata mbalimbali wenyewe wameshiriki kujenga, za msingi na za sekondari kuliko ilivyokuwa wakati nchi hii inapata uhuru?

Je, si kweli kwamba serikali imeongeza uwezo wa kulipa watumishi wake ikilinganishwa na miaka 15 iliyopita? Tatizo liko wapi?

Baada ya miaka 50 ya uhuru, wananchi wamegundua kuwa Tanzania inaweza kuwa inapata maendeleo makubwa ya vitu lakini si maendeleo ya watu. Vitu vyenyewe ni barabara, shule, zahanati, visima vya maji, mabwawa, nk, bado havijachangia maendeleo yao.

Mwalimu Nyerere katika kitabu chake cha “Uhuru na Maendeleo” amezungumzia tafsiri yake kuhusu uhuru na maendeleo na umuhimu wa uhuru katika maendeleo.

Anasema, “Tunapozungumzia habari za uhuru maana yetu nini hasa? Kwanza, kuna uhuru wa nchi; yaani uwezo wa wananchi wa Tanganyika kujipangia maisha yao, wakijitawala wenyewe bila ya kuingiliwa kati na mtu yeyote asiyekuwa Mtanzania.”

“Pili, kuna uhuru wa kutosumbuliwa na njaa, maradhi, na umasikini. Na tatu, kuna uhuru wa mtu binafsi; yaani haki yake ya kuishi akiheshimika sawa na wengine wote, uhuru wake wa kusema na uhuru wake wa kushiriki katika uamuzi wa mambo yote yanayogusa maisha yake, na uhuru wa kutokamatwa ovyo na kutiwa ndani kwa kuwa tu kamuudhi mkubwa, japo kuwa hakuvunja sheria yoyote….”

Na kuhusu maendeleo, Mwalimu alifundisha, “Maana ukweli ni kwamba maendeleo maana yake ni maendeleo ya watu. Mabarabara, majumba, kuongeza mazao, na vitu vingine vya aina hii, si maendeleo; ni vyombo vya maendeleo.

“Barabara mpya inampanulia mtu uhuru wake kama ataitumia kwa kusafiri. Kuongeza majengo ya shule ni maendeleo kama majengo hayo yanaweza kutumika, na yanatumika kuongeza ujuzi na elimu ya watu… Maendeleo yasiyokuwa maendeleo ya watu yanaweza kuwapendeza wataalamu wa historia mwaka 3000; lakini kwetu sisi hayana maana kwani hayahusiani na maisha ya kesho tunayoyajenga….”

Takwimu za serikali zinaonyesha kuwa japokuwa ni kweli uchumi unakua, ukuaji huo hautafsiriki faida yake kwa uchumi wa watu; uchumi unakua lakini umaskini unaongezeka.

Baada ya miaka 50 ya uhuru, watawala wanajifutua kufurahia majengo mengi mapya marefu katika miji ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na Mbeya, wakidai ni maendeleo.

Wananchi hawana cha kufurahia. Shule zipo lakini hazina walimu na waliopo wanajuta; zahanati zipo lakini hazina dawa, vifaa na manesi; wanazuiwa kutumia mkaa wakati gharama za umeme na mafuta ya taa ziko juu.

Wananchi wanaopigwa takwimu hizi wanashuhudia kila siku manyanyaso na kukosekana usawa katika kipato na demokrasia. Wanahisi watawala walifeli darasa elekezi la Mwalimu Nyerere ambaye alionya juu ya athari kubwa za kukamata watu ovyo na kuwatia ndani kwa kuwa tu wametumia uhuru wao kukosoa viongozi wao.

Wananchi wanashuhudia watawala wanavyokiuka haki za binadamu, kupiga wapinzani na kuwafungulia kesi kuzima mageuzi.

Wanashuhudia kukosekana kwa uvumilivu wa kusikiliza hoja kutoka kwa watu wasiowashabikia; chama tawala kilichokuwa kinapewa darasa elekezi kimebobea kwa kuzomea wapinzani.

Wakati hakuna juhudi za kuyaongezea thamani mazao ya wananchi ili yapate bei nzuri, watawala wamerundikia posho wabunge. Halafu wamesalimu amri kwa mafisadi na wawekezaji laghai na wezi.

Lakini katika kitabu cha “Binadamu na Maendeleo,” Mwalimu Nyerere alisema kama haki imefungiwa ndani au mlango uko wazi nusu, basi nguvu itumike kuufungua uwe wazi watu wafaidi haki na demokrasia.

"Ikiwa mlango utakuwa umefungwa, juhudi zifanywe ili kuufungua; ikiwa uko wazi nusu na nusu umefungwa, nguvu itumike kuusukuma hadi ufunguke wote. Hata hivyo isiwe kwa gharama ya waliomo ndani." Nukuu hii ipo katika hotuba ya “Utengamano na Mabadiliko Barani Afrika” aliyoisoma Chuo Kikuu cha Toronto, Canada, 2 Oktoba 1969.

Katika kipindi hiki ambacho watu wana uelewa mpana kuhusu haki zao za msingi na za kikatiba, watawala wasipobadilika kifikra wakadhani dawa ya kuzima upinzani ni kuwanyamazisha ili wasikosoe watawala, watambue wanachochea hasira za kudai kwa nguvu mageuzi, demokrasia, haki na uhuru wa watu. Na huko ndiko twendako.

0789 383 979, jmangul@yahoo.com
0
No votes yet