Serikali hii inatesa na kuua raia


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 18 July 2012

Printer-friendly version
Tafakuri
Dk. Steven Ulimboka

“TUMDHURU Dk. Steven Ulimboka ili serikali ipate nini,” ni utetezi mwepesi wa Serikali juu kutuhumiwa kuhusika kwake na kutekwa na kisha kupigwa nusu ya kufa kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya Madaktari, Steven Ulimboka, ambaye sasa anatibiwa nje ya nchi.

Uetezi huo umetolewa kama njiaa ama ya kupinga au kukwepa madai ya kuundwa tume huru ya kuchunguza ukatili na ufedhuli aliofanyiwa Dk. Ulimboka.

Kauli hii imetolewa mara mbili na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akikataa wazo la kuundwa kwa tume huru, lakini pia imetolewa mara moja na Rais Jakaya Kikwete.

Wote wamejitetea kuwa hawaoni mantiki wala uwezekano wowote wa serikali kuhusika na ufedhuli dhidi ya Dk. Ulimboka.

Nimesema kuwa huu ni utetezi mwepesi kwa sababu nyingi, lakini kubwa zaidi ni kwamba inayotuhumiwa hapa ni serikali, na wanaojitetea ni viongozi wake wakiisemea serikali hiyo hiyo.

Rais Kikwete amekwenda mbali zaidi kusema serikali yake haijatuma mtu kwenda kumteka na kumdhuru Dk. Ulimboka.

Lakini zaidi akasema kuwa Dk. Ulimboka alikuwa kiungo muhimu kati ya madaktari na serikali katika mazungumzo ya madai ya madaktari; kwa maana hiyo haoni ni kwa jinsi gani serikali ipange ufedhuli huo na mtu waliyekuwa wanawasiliana naye vizuri.

Pinda amesisitiza mara mbili ndani Bunge kwamba “haingii akilini serikali kwa nini ipange kumdhuru Dk. Ulimboka ili ipate nini… tena wakati ilikuwa na uamuzi wa mahakama uliokuwa unaisaidia.”

Viongozi hawa, siyo tu kwamba wamejitahidi kuiweka serikali juu ya tuhuma zozote kuhusiana na ufedhuli aliyofanyiwa Dk. Ulimboka, bali pia imejenga picha kwamba siyo utamaduni wake wala watendaji wake kuwafanyia raia wake ufedhuli.

Inawezekana kabisa Rais Kikwete na Waziri Mkuu Pinda wako sahihi, kwamba serikali haihusiki na ukatili huu aliofanyiwa Dk. Ulimboka, lakini usahihi huo hauwezi kuthibitishwa na yenyewe au vyombo vyake tu ambavyo vinatiliwa shaka katika kadhia hii mbaya.

Kwa maana hiyo, ili kukata mzizi wa fitina na kujiondoa kwenye lawama, halikuwa suala la kufikiria mara mbili katika kutafuta ukweli wa jambo hili ambalo linachafua sifa ya serikali iliyoko madarakani.

Serikali ingeridhia tu kukubali kuundwa kwa tume huru ambayo ingejumuisha watu wa makundi mbalimbali katika jamii, kwani mbali ya kuonyesha kuwa haina inachoficha, pia ingekuwa inatekeleza kwa uwazi kabisa dhana nzima ya utawala bora.

Serikali katika kadhia hii ni mtuhumiwa, sasa kuliagiza tu Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi inajenga hisia na hitimisho lisilotikisika kuwa serikali inataka kufunika kombe ili mwanaharamu apite.

Serikali hii ilipoingia madarakani, mwaka 2006 iliamua kuunda tume huru iliyoongozwa na Jaji Musa Kipenka kuchunguza mauaji ya wafanyabiashara wa Mahenge waliouawa na polisi kwa ukatili mkubwa wenye sura inayoelekea kufanana na ufedhuli huu aliofanyiwa Dk. Ulimboka.

Tujikumbushe machache katika matukio ya kinyama yanayofanywa dhidi ya raia na ama vyombo vya dola au watumishi wa umma, kwa kisingizio cha kutekeleza wajibu wao.

Itakumbukwa kwamba wakati wa utawala wa awamu ya tatu, aliyekuwa Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Luteni Jenerali Imran Kombe, Juni 30, 1996 aliuawa kinyama na askari polisi.

Polisi walitekeleza unyama huo licha ya ukweli kwamba walimjua, walimsikia akijieleza, walimwona akiwa amejisalimisha, na kwa uhakika alikuwa hana lolote alilokuwa anafanya lililowapa polisi wale uhalali wa kuumua kama mnyama.

Kwa mfano, Koplo Juma Mswa na Konstebo Mataba Matiku ambao mwaka 1998 walihukumiwa kifo na mahakama kuu na kisha rufani zao mahakama ya rufani kutupwa kwa kumuua Kombe, waliachiwa huru chini ya msamaha wa rais.

Ikulu ya sasa ilitoa taarifa mwaka huu ikipinga kuwa siyo Rais Kikwete aliyetoa msamaha huo, ila alipoingia madarakani Desemba mwaka 2005 alikuta maamuzi ya msamaha huo umekwisha kufanywa.

Serikali inatengeneza ugomvi ili ionekane suala ni nani alitoa msamaha, wakati hoja ni kwamba ugomvi hapa siyo nani alitoa msamaha, ila ni kwa nini ulitolewa. Serikali ndiyo ilitoa, bila kujali ni nani, ni utawala ule ule wa chama kile kile.

Lakini cha kustaajabisha hata pale serikali iliposhindwa hata kesi ya madai ya mjane wa Kombe, na kulipa Sh. milion 300 kwa uzembe wa watumishi wake, serikali hiyo hiyo ilikuwa na ujasiri wa kuwaachia kwa huruma ya rais wauaji wa Kombe.

Yapo mauaji mengi mno ambayo yamefanywa na polisi kwa staili ya kutisha mno. Julai 2009 polisi walifanya mauaji wilayani Kyela, mkoani Mbeya. Tume iliundwa na taarifa kuwasilishwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kwa ajili ya hatua zaidi.

Hakuna kilichofanywa dhidi ya polisi waliohusika. Kati ya Machi na Julai mwaka 2009 raia sita waliuawa kikatili na polisi, lakini jeshi hilo lilishindwa kuchukua hatua dhidi ya askari wake waliohusika na mauaji hayo ya kinyama.

Machi Mosi mwaka 2009, polisi mkoani Arusha waliwaua kinyama vijana wawili, kwa kuwapiga risasi Ewald Mtui (36) na Shadrack Motika (22) ambao walituhumiwa kuwa walihusika na matukio ya ujambazi.

Tukio la kuuawa vijana hao wawili liliibua kelele na mjadala kwenye vyombo vya habari na kusababisha aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Isdore Shirima kuunda timu ambayo ilichunguza tukio hilo na kubaini kuwa waliouawa hawakuwa majambazi na waliuawa kwa makosa.

Machi 24 mwaka 2009 Polisi jijini Dar es Salaam walimuua kinyama dereva teksi Lazaro Mwapi, 23, kwa kumpiga risasi. Mauaji yaliyotekelezwa na ofisa wa polisi kutoka kikosi cha Askari wa Dharura (99) Koplo Adelbert Donald Sangu.

Kijana huyo aliuawa kwa risasi wakati akiendesha teksi yake na kukutana na polisi hao waliokuwa wamevalia kiraia maeneo ya Kimara Stop Over. Alitii amri ya kusimama, lakini akakataa kufungua madirisha na ndipo polisi hao walipovunja kioo cha mlango wa mbele na kummiminia risasi.

Julai 15, 2009 Polisi wa kituo cha Stakishari jijini Dar es Salaam, walimpiga hadi kufa mfanyabiashara Tuga Rashidi (31), wakimtuhumu kuwa ni jambazi; Juni 2009 polisi walimuua mfanyabiashara Frank Mwachembe, katika mji mdogo wa Tunduma, Mbeya;  Julai 2009, kijana Lucas Mwaipopo (20), mkazi wa Kyela mkoani Mbeya aliuawa na polisi ambaye alifia mikononi polisi saa chache tu baada ya kumkamata.

Matukio haya machache nmifano tu, yapo mengi yanayoonyesha kuwa kuna ushahidi wa kutosha kwamba vyombo vya dola vinashiriki katika mauaji ya raia.

Matukio haya yanafanya utetezi unaotolewa na serikali juu ya kutokuhusika kwake na ufedhuli aliofanyiwa Dk. Ulimboka kukosa nguvu kwa sababu historia ni mwalimu mzuri sana.

Ni katika ukweli wa namna hii inakuwa vigumu serikali kuaminika, kwanza kwa kutaka kufunika kombe kwa kuendesha uchunguzi yenyewe wakati ni mtuhumiwa mkubwa juu ya kadhia hii. Lakini pia kwa kuibuka na utetezi kuwa haihusiki huku ikikataa kuchunguzwa kwa suala hilo na vyombo huru, inazidi kuzama katika tope chafu linalonuka.

0
No votes yet