Serikali hii kama ya walevi


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 29 February 2012

Printer-friendly version

TAREHE 12 Februari 2004, mjini Dodoma, Mzee wa “Uwazi na Ukweli,” Benjamin Mkapa alipohutubia Bunge alivunja watu mbavu.

Mkapa alitoa hadithi ya walevi wawili waliokutana njiani usiku wa mbalamwezi na wakaanza kubishana kama walichokuwa wanakiona ni mwezi au jua.

Alisema, “...Walevi wawili walikuwa wanatembea usiku. Mmoja akaangalia juu, akamwambia mwenziwe, ‘Usiku wa leo ni mzuri kweli. Hebu ona mwezi ulivyopendeza!’ Mwenzake akasimama, akapepesuka kidogo, kisha akajibu, ‘Wewe vipi, umelewa nini? Huo si mwezi, hilo ni jua.’

“Wakabishana kwa muda mpaka walipomwona mtu wa tatu akipita karibu yao. Kumbe naye mlevi. Wakamuuliza, ‘Samahani bwana. Hebu tusaidie. Lile ni jua au mwezi?’ Mlevi wa tatu akasimama, akafinya macho, kisha akajibu, ‘Sijui bwana, mimi ni mgeni hapa!”’ Wabunge na wasikilizaji wakaangua kicheko.

Majibu ya mlevi wa tatu yanafanana sana na aliyotoa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hadji Mponda kuhusu sakata la ugonjwa wa Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe.

Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, amedai mara mbili kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi Dk. Harrison Mwakyembe kalishwa sumu. Hii ina maana katika ugonjwa wa Mwakyembe kuna jinai.

Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha akaliagiza Jeshi la Polisi lichunguze jinai hiyo. Baada ya kufuatilia nyaraka kadhaa, nyingine wakidai zimetoka wizara ya Dk. Mponda, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba akatangaza kwamba Mwakyembe hakulishwa sumu; kwa hiyo Waziri Sitta mwongo.

Siku iliyofuata Dk. Mponda akamruka DCI Manumba akidai hajui na hana ripoti ya ugonjwa wa Mwakyembe wizarani kwake.

Je, ni kweli ripoti hiyo haiko wizarani? Kama ni kweli basi Manumba kasema uongo. Taarifa ya Dk. Mponda imempa nguvu Mwakyembe na analishangaa Jeshi la Polisi kutoa taarifa hiyo.

Kama Dk. Mponda yuko sahihi, Manumba kapata wapi ripoti inayogonganisha watendaji serikalini? Je, analinda wahalifu anaowajua kama wa rada, Richmond, EPA, Meremeta na Kagoda?

Basi, ili kuondoa kiwingu cha sakata hili ripoti ichapwe. Hatuombei, lakini ikiwa Mwakyembe atazidiwa akaaga dunia katika mazingira haya, mchawi nambari wani atakuwa serikali.

Waziri mmoja anasisitiza Mwakyembe kalishwa sumu lakini ofisa mwandamizi anasema hakulishwa sumu huku waziri mwingine akisema hahusiki na taarifa alizotoa ofisa huyo.

Ikiwa kweli Mponda amesema ya kutoka ‘rohoni’ mwake, anamaanisha DCI Manumba amedanganya. Sasa kama Manumba kasema uongo, hao wadogo zake, yaani wafanyakazi wa chini wamesingizia wangapi?

Wadogo zake Manumba wamekanusha ukweli mara ngapi? Tukio hili si linathibitisha madai ya wafungwa wengi nchini kwamba wamebambikiwa kesi? Vyombo hivi vinatumikia wahalifu (mafisadi), na hii ndiyo ajenda ya siri katika sakata la Mwakyembe.

Kumbuka, Takukuru iliwahi kusema kuwa hakukuwa na rushwa katika zabuni ya Richmond; Takukuru hao hao bila aibu wakajitokeza kuvuruga vita ya ufisadi eti aliyekutwa na “ngawira” kiasi cha shilingi bilioni katika benki ya ughaibuni kafutiwa kesi wakati wakijua haikuwa kweli.

Takukuru wanaruhusu rushwa, wapelelezi wanaruhusu uhalifu – Sitta anasema kuna mazingira ya sumu; DCI anasema hakuna sumu; Mponda anakaa katikati akidai hajui kitu.

Majibu ya kilevi ndiyo yaliwagonganisha vigogo katika sakata la posho, hivi karibuni. Hakika hiki ni kielelezo kuwa serikali inaugua ugonjwa usiotibika na unakaribia kuiangamiza.

0658 3838 979
0
No votes yet