Serikali iache ubabe


editor's picture

Na editor - Imechapwa 17 February 2010

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

KAULI ya Jaji Mkuu, Augustino Ramadhani kuhusiana na mgombea binafsi katika uchaguzi mkuu ujao, inawabebesha watawala fedheha.

Fedheha haitoki kwa jaji au mahakama. Inatoka kwa watawala na kwenda kwa watawala. Ni wao wamevunja Katiba ya nchi.

Alichofanya Jaji Ramadhani ni kuwakumbusha watawala kuwa kuna hukumu ya mahakama kuu inayosema “mgombea binafsi” ni halali katika uchaguzi ujao.

Sasa Watanzania wanafahamu kuwa serikali iliyoko madarakani chini ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), imethibitishwa isivyofuata utawala wa sheria kwa kitendo chake cha kulitumia bunge kupora haki ya raia kugombea uongozi bila ya kuwakilisha chama cha siasa.

Mahakama iliruhusu mgombea binafsi asimame kwenye uchaguzi kwa kuwa haki hiyo imetolewa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Bali serikali ilionyesha ubabe juu ya sheria na misingi ya demokrasia; ikapeleka muswada bungeni – kwa namna ya kukengeusha uamuzi halali wa mahakama – na kufanikiwa kuzuia kilichoruhusiwa kisheria.

Kilichofanywa na serikali ni uvunjaji Katiba na kubeza mantiki ya mgawanyo wa madaraka ambao unaelekeza mihimili ya dola kufanya kazi kwa kuheshimiana na siyo mmoja kutumia mwingine kukidhi matakwa yake, tena yaliyo haramu.

Ni ukorofi wa serikali kujitia hamnazo na kupora haki iliyohalalishwa na Katiba ya nchi na kuhimizwa na Mahakama, chombo mahsusi kilichopewa jukumu na Katiba hiyohiyo la kusimamia utoaji wa haki.

Wala ilichofanya serikali si ukorofi tu, bali pia dharau kubwa. Imedharau mahakama; imedharau viongozi wa mahakama; imedharau Watanzania na ikadharau utawala wa sheria.

Katika kukandamiza haki ya Mtanzania asiyeamini katika kutafuta uongozi kupitia chama cha siasa, serikali imekosea maana sasa umma utaamini kumbe viongozi wake katika utawala hawathamini misingi ya demokrasia.

Serikali imethibitisha inavyojiona iko juu ya sheria na kwamba haiwajibiki kufuata sheria zinazozitungwa.

Haijatoa hoja ya msingi ya kutaka Mtanzania asifaidi haki anayopewa na Katiba. Huu ni mtihani mgumu unaoikabili wakati ikisubiriwa kuwasilisha hoja zake mbele ya jopo la majaji wa Mahakama ya Rufaa.

Kwa mwenendo huo mchafu, inatia shaka kwamba hakutafika siku CCM ikakubali kilio cha umma cha kutaka katiba mpya waliyoiridhia kwa kushiriki kuiandaa. Tusifike huko.

Tunahimiza na kuitaka serikali iache ukorofi mbele ya haki za wananchi. Iache kupeleka mikono na mabavu yake na kuchezea haki zilizohalalishwa kikatiba.

0
No votes yet