Serikali ibebe lawama za ucheleweshwaji kesi


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 10 February 2010

Printer-friendly version
Mtazamo

WAKUU wa Mahakama nchini wamekuwa wakilalamika mara kwa mara kwamba shughuli za taasisi hii mhimili wa dola zimekuwa zikizoroteshwa kwa sababu ya bajeti finyu.

Tatizo la mahakama kupatiwa fedha zisizotosheleza mahitaji ya kibajeti kila limekuwa sugu kwani siku zote viongozi wake wamekuwa wakililalamikia nab ado serikali haijasaidia ufumbuzi.

Ulipoibuka mjadala wa taasisi gani hasa inahusika zaidi katika kusababisha ucheleweshaji wa kesi za jinai, Jaji Kiongozi, Fakih Jundu alisema shughuli za mahakama zinakwama kutokana na mahakama kutopatiwa fedha za kutosha ambazo zingeiwezesha kutimiza majukumu yake.

Jaji Jundu alisema ili kuwezesha shughuli za mahakama kufanyika kwa ufanisi, mkoa mmoja tu unahitaji Sh. 50 bilioni kwa mwaka. Hata hivyo, alisema ni Sh. 23 bilioni tu hutolewa na serikali.

Kwa wastani, Jaji Jundu anasema imekuwa kwa maombi ya fedha yanayopelekwa serikalini, serikali hutoa chini ya nusu ya mahitaji halisi.

Kukosekana kwa fedha za kutosha kuna maana kwamba mahakama haitaweza kununua vifaa andishi (stationaries) vya kutosha, haitaweza kuhudumia watumishi wake vizuri, haitaweza kupeleka majaji wa rufaa kwenye kanda kwa ajili ya usikilizaji wa rufaa mbalimbali.

Mahakama itashindwa kutengeneza majengo yake yakiwemo yale yanayotumika kusikilizia kesi. Na haya ni majengo ya mahakama kuanzia za mwanzo, mahakama za wilaya, mahakama za mahakimu wakazi na mahakama kuu.

Ni jambo la kusikitisha kuona kwamba kila siku wakuu wa Mahakama wanalalamikia tatizo hilohilo. Inasikitisha zaidi kwamba pamoja na matatizo yanayoikabili taasisi hii yanayokuzwa na kutopatiwa fedha za kutosha kuendesha shughuli zake, mwisho wa siku ni taasisi hiihii ndiyo inayojikuta ikilaumiwa.

Mahakama inalaumiwa na wananchi kwa kuchelewesha kesi kiasi cha kusababisha magereza kujaa mahabusu na wafungwa wanaosubiri rufaa zao.

Lakini tayari hata viongozi wa serikali wanasikika wakiitaja mahakama kuwa ndiyo inayochangia zaidi tatizo la ucheleweshaji wa kesi. Hapa lipo tatizo. Kwamba huenda serikali inafanya makusudi kutoipatia mahakama fedha inazohitaji kuendesha shughuli zake.

Inawezekana serikali haipendi kazi ya mahakama. Labda kwa sababu hata yenyewe inaumia kwa kupoteza kesi nyingi zikiwemo za madai na kujikuta ikilazimika kulipa mabilioni ya shilingi kwa wale wanaoishinda mahakamani.

Hata hivyo, bado hiyo si sababu ya serikali kugomea mahakama. Serikali ina wajibu wa kutekeleza kwa sababu ndiyo inayokusanya mapato, ndiyo inayogawa mapato. Na mambo haya ni kwa mujibu wa katiba ya nchi.

Ni serikali inayopaswa kikatiba kugawa mafungu ya fedha kwa taasisi zake. Lakini ni serikali inayotakiwa kuhakikisha kazi za mihimili mingine ya dola zinatekelezwa kwa ufanisi. Hiyo itatokea iwapo inazigawia fedha kama zinavyoomba.

Wananchi wamechoka kusikia simulizi za eti serikali haina fedha za kutosha maana uchumi bado mchanga. Hizi ni kauli za visingizio tu ambavyo havina tija yoyote zaidi ya kudhoofisha utendaji wa serikali yenyewe na taasisi zake pamoja na taasisi mihimili kama ilivyo.

Haiwezekani Mahakama iendelee kuishi kwa kutegemea huruma ya serikali. Maelfu ya wananchi wakiwemo wengi wenye uwezo wa kufanya kazi za kuzalisha mali na kusaidia uchumi wa familia zao na wa taifa, wanaumia magerezani kwa sababu mahakama inanyimwa fedha na serikali. Haikubaliki.

Kauli ya Rais Jakaya Kikwete kwamba anatambua matatizo yanayoikabili mahakama, inafurahisha. Lakini haitoshi kwa sababu kilio cha wakuu wa mahakama si cha leo naye amekuwa katika safu ya juu ya uongozi kwa muda mrefu akiwa waziri.

Mahakama inahitaji bajeti yake isiyomtegemea mtu yeyote. Ichukuliwe kama ilivyo kuwa ni taasisi mhimili na inastahili kuamua mambo yake kwa vile viongozi wake wanavyoona.

Ninaamini Jaji Mkuu, Augustino Ramadhani atatumia nafasi hiyo kuwasilisha mahitaji kamili ya kibajeti ya taasisi anayoongoza ili hatua ofisi ya rais ichukuwe hatua zifaazo katika muda muafaka.

0
No votes yet