Serikali ijiondoe kwenye lawama


editor's picture

Na editor - Imechapwa 13 October 2010

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

MWAKA jana serikali iliwalazimisha wamiliki wote wa simu za mkononi kusajili namba za simu zao, kwa maelezo kwamba huo ni utaratibu mpya wa kudhibiti matumizi mabaya na uhalifu.

Taarifa ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) iliyosimamia usajili wa namba za simu kwa ushirikiano na kampuni za simu; Zain, Vodacom, tiGO, Zantel na TTCL, ilisema utaratibu huo una lengo la kurahisisha ufuatiliaji wa matukio ya kihalifu, matusi na mipango ya uvunjifu wa amani inayofanywa kwa kutumia simu.

Kwa kuwa, hilo lilikuwa agizo la serikali na kwamba yeyote ambaye angeshindwa kutekeleza katika muda uliopangwa angefungiwa namba yake; kila mtumiaji aliitikia wito huo.

Lakini miezi michache tangu zoezi hilo likamilike kwa ufanisi, katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani, makampuni ya simu—kwa kujua au kutojua—yameruhusu taarifa chafu kusambazwa nchi nzima kupitia mitandao hiyo.

Baadhi ya taarifa hizo zimekuwa za kuhamasisha watu kuwapigia wagombea wanaowapenda na kutowapigia wasiowapenda.

Lakini katika siku za hivi karibuni simu hizo zimekuwa zikipitisha taarifa za uchochezi, kashfa na zenye lengo ya kuchafua sifa na hadhi ya wagombea wengine.

Mbali ya kuchafua hadhi ya wagombea hasa wa ngazi ya urais, taarifa hizo zimejaa uchochezi, vitisho, upotoshaji wa hali ya juu ambao unavumiliwa na mamlaka husika.

Kwa kuwa uhalifu uliotajwa ni pamoja na kutukana, kupanga wizi na hujuma; kutoa vitisho, upotoshaji na kashfa, serikali, TCRA, na makampuni ya simu yaeleze kwa nini hawajazuia mpaka sasa.

Kama serikali, TCRA na makampuni ya simu watasema hawana uwezo kuzuia, kuulikuwa na faida gani kusajili namba hizo? Kwa nini walitumia mabilioni ya shilingi kama hawawezi kubaini uchochezi huu? Je, wanaweza kutuambia namba hizo ni za kina nani?

Ikiwa hakutakuwa na ufafanuzi juu ya kashfa, vitisho, uchochezi na hujuma za kisiasa zinazofanywa kupitia simu za mkononi, serikali, pamoja na makampuni ya simu na TCRA watabeba lawama moja kwa moja.

Watabeba lawama kuwa wao ndio waliofadhili uhalifu huu, uchochezi na kashfa kwa malengo ya kisiasa; hivyo basi wawaeleze Watanzania nini kimetokea? Kama si wao wajisafishe kwa kueleza kulikoni nchi imefikia hapo.

0
No votes yet