Serikali ikikiri kushindwa 'ipumzike'


Ndimara Tegambwage's picture

Na Ndimara Tegambwage - Imechapwa 28 October 2009

Printer-friendly version
Rais Jakaya Kikwete

SERIKALI imesema isilaumiwe kwa ukame au vifo vya mifugo nchini. Rais Jakaya Kikwete amesema, "Wapo …wanaoichukia serikali kutokana na ukame; jamani hata sisi tunaomba Mungu hali iwe nzuri…"

Ni kauli za aina hii ambazo vijana wa mjini hupenda kuita, “funga kazi.” Tatizo la vijana hao ni kwamba hawaoni kuwa kazi haijafanyika. Ukweli ni kwamba hizo ni kauli za mwisho wa mwanzo wa kukata tamaa.

Tujadili. Kisiasa, kauli ya rais ilitolewa muda na mahali pasipofaa. Ilitolewa katika kijiji cha Olbalbal wilayani Ngorongoro. Taarifa za awali zilikuwa zimeeleza kuwa rais yuko likizo ndogo katika mbuga za wanyama za Ngorongoro.

Ngorongoro ni moja ya wilaya ambazo zimekumbwa na ukame wa aina yake. Mifugo inakufa. Mizoga imetapakaa huku na kule. Wafugaji hawana maji. Niliwahi kuandika kuwa hata wao wanaweza kuitwa “mizoga inayotembea.”

Ni huko rais alikwenda kufanya mapumziko. Nasema siyo sahihi kisiasa kwa kuwa rais kaenda “kujinyolosa” baada ya mahangaiko; pale – jirani tu – hata kama kwa umbali wa kilometa 80; lakini ndani ya wilaya hiyohiyo ambamo maafa ndiyo maisha.

Kama siyo kwa diplomasia – ule unafiki wa kicheko na mgonganisho wa bilauri za mvinyo huku watu wakiteketea – na hilo hufunzwa vyuoni – basi rais angekemewa.

Sasa rais amewahi. Amewaambia wananchi wanaoishi katika wilaya ambamo uoza wa Loliondo umefunika harufu kali ya ubani, kuwa hana la kufanya kuhusu ukame na vifo vya mifugo yao. 

Kwamba wafuge kisasa; kwamba yeye ana ng’ombe 600 lakini hahitaji kuzungukazunguka nao kutafuta malisho; kwamba wajifunze kutoka wafugaji wa Uganda; kwamba hata serikali inaomba mvua zije.

Ukitaka waweza kuita hayo kuwa ni kejeli. Ukitaka waweza kuita kauli za kutojali kilio cha wafugaji. Ukitaka pia waweza kuita mizaha kwenye msiba. Mkuu wa nchi akisema hayo, wanasiasa wa viwango vya Yusuph Makamba watasema nini?

Uko wapi mpango wa serikali wa kushirikisha wananchi – wafugaji – katika kutatua matatizo yao? Kwa mfano, uongozi wa wilaya au mkoa kukaa na wafugaji; kujadili jinsi ya kuchanga ng’ombe, kuwauza, kupata fedha za kununulia mabomba ili kuvuta maji kutoka mbali. Uko wapi?

Uko wapi mpango wa serikali wa kutafuta vilipo vyanzo vya maji wilaya nzima; kuvilea, kuvihifadhi na kujenga malambo yenye uwezo mkubwa wa kulinda maisha ya mifugo na wafugaji?

Kama kuna mfano mzuri Uganda, wafugaji wa huko walianza vipi? Walitoka usingizini wakajikuta wameanza kufuga kisasa; au kuna waelekezaji – wataalam wenye moyo wa kutumikia jamii – ambao waliacha umangimeza; wakajitosha kwenye maeneo ya wafugaji na kuanza kushawishi, kufundisha na kuonyesha mifano?

Wafugaji wa wilaya ya Ngorongoro siyo ombaomba. Hutozwa kodi, yao na ya mifugo. Wanahitaji utaalam wa wale wanaojali na wasiosingizia Mungu kwa kila janga, pamoja na janga la ukame. Wanahitaji uongozi wenye akili na unaowathamini.

Umbali uliopo kutoka yalipo maji hadi walipo wafugaji na mifugo yao inayokufa, hauzidi kilometa 80. Pengine ni kilometa tano. Pengine kilometa 15. pengine kilometa 40.

Vilevile kuna maji yaliyofungiwa na wanaoitwa wawekezaji – wale waliojipa uwezo wa ki-Mungu wa kuamua huyu na mifugo yake hata wafe, potelea mbali, lakini hawawezi kuchota maji kwenye kisima kilichoko wilaya ya Ngorongoro, mkoa wa Arusha, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ushenzi uliopitiliza.

Wanaoitwa viongozi wa wilaya wamefumba au wamefumbwa midomo. Viongozi wa mikoa yenye ukame wamejikinga nyuma ya pazia la “sheria.” Waziri wa mifugo anahangaika kukanusha ukweli usiokanushika. Leo rais anasema hana la kufanya labda kumwomba Mungu.

Picha za mizoga ya mifugo – ng’ombe, mbuzi na kondoo, ni ushahidi wa serikali isiyotenda. Sauti za wafugaji, zinazotetereka na kupotelea mbugani bila kusikilizwa na watawala, ni ushahidi wa ukatili unaoendeshwa na wale wanaoishia kutukana, kukejeli na kufukuza wafugaji kutoka makazi yao.

Rais ana ardhi. Ana maji. Ana fedha za kutunzia bustani za vyakula vya mifugo. Ana fedha za kununulia dawa. Ana maji ya kunywesha mifugo na kumwagilia bustani za vyakula vyake. Ana madaraka – maji hayakatiki. Yakikatika akikohoa yanarudishwa. Haombi Mungu mvua inyeshe ili mifugo isife.

Rais alipewa ushauri na wataalam. Anakofugia paliandaliwa na wataalam. Panakaguliwa na wataalam; na ng’ombe ni ng’ombe tu; awe wa rais au wa Masaai.

Lakini mfugaji, mwenye elimu ya asili tu ya kujishughulisha na mifugo; kwa mfano kujua dawa za miti shamba za kuiponya na mahali pa kuilaza; anahitaji kufikiwa na mbinu za kisasa ili afuge kama rais au kama Jakaya Kikwete.

Wafugaji wengine, pamoja na kuishi mbali na miji, na hiyo ni faida kwao, wana ng’ombe wengi kuliko rais. Wengine wana hata zaidi ya 2,000. Kuwapa wananchi hawa wazo la kuchangia kupatikana kwa maji katika maeneo yao, hakuwezi kuwa mzigo. Watahiari. Lakini hakuna uongozi wa kufanya hivyo.

Hili ni la kuwashirikisha – wao na utajiri wao wa mifugo. Haliwaondolei haki yao ya kufaidi matunda ya kodi walipazo. Hapa ndipo tungetaka kuona watawala wakiwajibika kwa walipakodi na siyo kuwaambia wamwombe Mungu ili mvua inyeshe.

Dunia nzima inatambua kazi ya kodi na mapato ya nchi kwa ujumla. Mfano wa Libya huwa unanijia mara kwa mara. Ni Kanali Muamar Ghadaffi, kiongozi wa nchi hiyo aliyesukuma maji kwa njia ya mabomba kwa umbali wa zaidi ya kilometa 1,700 ndani ya jangwa la nchi hiyo.

Watu wakanywa maji. Wakaonga. Wakafua. Wakatunza bustani ndani ya jangwa. Jangwa likakoma kuwa jangwa pale maji yalipotiririkia. Tanzania hakuna jangwa.

Rais Kikwete amekoleza kilio cha wananchi wafugaji wa wilaya ya Ngorongoro. Alikwenda kupumzikia kwao wakati wao hawana mapumziko. Wengi wanalala nje. Wamechomewa nyumba na maboma ya mifugo.

Rais alikwenda kupumzikia kwa wale ambao wanaswagwa na watawala wilayani kwa msaada wa “wageni” waliokabidhiwa vipande vya ardhi ya nchi hii kwa ajili ya kuua raslimali wanyama.

Kubwa kuliko yote ni kwamba rais amewaambia wakazi wa Ngorongoro kuwa wachague Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika uchaguzi wa serikali za mitaa, kwa kuwa ndicho chenye “uhakika wa kuwaletea maendeleo.”

Uko wapi uwezo alioahidi rais? Uuliyeyuka palepale aliposema hana uwezo wa kumaliza ukame na kusitisha vifo vya mifugo katika nchi yenye mito mikubwa isiyokauka; maziwa makubwa, marefu, yenye kina kirefu; na maeneo mengi yenye unyevu kunakoweza kuchimbwa mabwawa na malambo kwa ajili ya huduma kwa watu na mifugo yao.

0
No votes yet