Serikali ikiri kushindwa


Mwandishi Maalum's picture

Na Mwandishi Maalum - Imechapwa 12 May 2009

Printer-friendly version

KINYUME na majigambo ya serikali, kwamba kila mwaka serikali inatoa ruzuku ya fedha kugharamia Mpango Maalum wa Elimu ya Sekondari (MMES), mwaka 2008 serikali haikutoa fedha zozote kwa shule zake za sekondari ili kugharamia ada. 

Fedha ya MMES iko katika makundi mawili. Mosi, ni ya uendeshaji wa shule ambayo ni fidia ya ada. Hapa serikali ilikubali kubeba mzigo kwa kulipa nusu ya ada kwa kila mwanafunzi.

Hivyo, serikali inalipa Sh. 20,000 na mzazi analipa Sh. 20,000 kwa wanafunzi wa shule za kutwa. Kwa wale wanaosomea shule za bweni, serikali inalipa Sh. 35,000, mzazi analipa Sh. 35,000.

Inasikitisha kwamba serikali imewalaghai wananchi. Wazazi wanabanwa, wanalipa lakini serikali inakwepa kwa kisingizio cha hali ngumu ya uchumi, ufinyu wa bajeti na sababu nyinginezo.

Hata pale inapolipa, zinakuwa kidogo, chini ya kiwango kilichokubaliwa, kinachopaswa kupelekwa shuleni.

Pili, ni fedha zitolewazo kama ruzuku ya MMES, kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya vya kufundishia na kujifunzia.

Hapa ndipo penye tatizo. Hatuelewi serikali inatumia vigezo gani kutoa fedha hizi, kwani inaeleweka kwamba mahitaji ya shule na shule hutofautiana.

Mathalani, mnamo Februari 2009, serikali ilitoa kwa kila shule fedha za kununulia vifaa vya kufundishia na kujifunzia.

Shule yetu, ambayo ni ya kijijini, ina watoto 232 wa Kidato cha Kwanza. Ilipata Sh. 759,104. Baadaye, tumekuja kugundua kwamba kila shule ilipewa fedha hizi kulingana na idadi ya wanafunzi. Maana yake ni kwamba kila mwanafunzi alitengewa Sh.3,272.

Hii si haki kwa sababu, kwa namna yoyote ile, mfumo huu utazinyonya shule zote mpya (za Kata).

Shule hizi zina matatizo mengi. Hazina walimu, maabara wala vitabu; na nyingi ziko vijijini.

Haiwezekani hata kidogo ukatumia mfumo huu kuzipatia fedha shule hizi kama unavyozipatia shule kongwe, zinazojitosheleza kwa majengo, vitabu na vifaa vingine vya kujifunzia na kufundishia.

Ningependekeza ifuatavyo: Kwanza, mkazo uwe kwenye shule zote mpya za kata. Zipewe upendeleo maalum. Zitengewe mgawo mkubwa kuliko shule kongwe, ili ziweze kununua vifaa na kuboresha majengo ya shule.

Pili, kama serikali imeshindwa kutekeleza ahadi yake kwa wananchi, ya kugharamia nusu ya ada, iseme wazi, ili wazazi wajue na wajiandae kukabiliana na tatizo hilo moja kwa moja.

Lakini, kwanza ikubali kulipa madeni yote ya miaka miwili, ambayo haijatoa fedha zilizoahidiwa.

Tatu, wabunge waache tabia ya kuilinda na kuitetea serikali pale inapoboronga. Ni lazima waihoji, itoe maelezo kuhusu ziliko pesa ilizoahidi kutoa kwa ajili ya shule hizi.

Zipo taarifa kwamba shule za sekondari za vipaji maalum zinahudumiwa vizuri kuliko shule nyingine za elimu hiyo hiyo. Tena za serikali hiyo hiyo.

Kwa hiyo, kunapokuwa na taarifa zinazoonyesha kuwa baadhi ya shule zinapewa mafungu makubwa na nyingine zinapunjwa, huko ni kupanda mbegu za ubaguzi katika elimu.

Hakuna jambo baya na la hatari kama kuweka mizizi ya ubaguzi katika nchi, tena kwa jambo nyeti kama elimu. Jamii inaweza kusambaratiba kama ubaguzi kama huo utamea, kustawi na kupevuka.

0
No votes yet