Serikali ilete ajenda yake


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 13 May 2008

Printer-friendly version

SERIKALI ya awamu ya nne inayoongozwa na Rais Jakaya Kikwete, inaonekana imekuwa katika kifungo cha fikra kwa kipindi chote cha mwaka wa fedha wa 2007/08. Imeshindwa kujitoa katika ajenda iliyoasisiwa na wapinzani.

Ule moto uliowashwa na baadhi ya wabunge kuhusu Buzwagi; akaunti ya madeni ya nje (EPA); mkataba wa Richmond ungalipo. Ni moto ambao mawaziri waliupuuza wakikejeli kuwa ni kelele za watu wasiojua kinachoendelea maana serikali ilikuwa makini ikishughulikia mambo hayo.

Lakini pamoja na kusema suala la EPA kwa mfano lilikuwa likishughulikiwa, suala la mkataba wa Buzwagi, liligeuzwa kuwa mwiba kwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA), Zitto Kabwe baada ya hoja yake kudakwa na kugeuzwa na wingi wa wabunge wa CCM walioishia kumsimamisha vikao.

Kutoka hapo, mawaziri waliagizwa kuzunguka nchi kufafanua bajeti. Kuanzia Waziri Mkuu wakati ule, Edward Lowassa, hadi manaibu waziri, walizuru mikoani ili kuzima moto waliowasha wabunge wa upinzani kwa kusema serikali inalea ufisadi.

Mawaziri walivuna aibu kwa kuzomewa na wananchi katika ziara zilizoanza mara baada ya mkutano wa 10 wa Bunge uliojadili na kupitisha bajeti ya 2007/08.

Kwa maneno mengine, kazi ya kwanza waliyoifanya tangu bajeti hiyo ipitishwe, ni kwenda kukabili hasira za wananchi dhidi ya serikali yao kutokana na kuendekeza ufisadi na bajeti isiyopunguzia wananchi umasikini.

Kwa bahati mbaya, ajenda hii ya wapinzani, naomba kusisitiza, ya wapinzani, imekuwa ya kudumu tangu hapo wapinzani walipobuni na kuratibu kampeni dhidi ya ufisadi.

Walijaribu kutumia Bunge kuwasilisha tuhuma hizo, kama EPA kwa juhudi za Mbunge wa Karatu (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa aliyeandaa hoja binafsi lakini akafanyiwa mizengwe na kulazimika kuiondoa; na jinsi Kabwe alivyohujumiwa kuhusu Buzwagi, mwishowe wapinzani waliamua kushitakia umma.

Vita dhidi ya ufisadi ikaanzia hapo na kwa sasa ajenda hiyo imeingia kisawasawa vichwani mwa Watanzania. Imekuwa kubwa na nzito kiasi cha serikali kushindwa kufikiri nje ya ajenda hii. Ni ajenda hii iliyosambaratisha Baraza la Mawaziri baada ya Lowassa kujiuzulu akifuatiwa na mawaziri Nazir Karamagi na Dk. Ibrahim Msabaha walioondoka naye katika sakata la Richmond.

Lakini pia ni tuhuma za ufisadi katika ununuzi wa rada zilizomuondoa Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge, baada ya kukejeli sinikizo za kumtaka ang'atuke.

Kwa kutambua kuwa serikali imekwama, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Steven Wassira, akiwa Bahi, mkoani Dodoma, alithibitisha imani hii.

Alilalamikia vyombo vya habari kushikilia mambo hayo tu kama ndio habari pekee: Amekerwa na ajenda hii na hana la kufanya kuizuia.

Wassira hapendi magazeti yaandike habari za ufisadi, lakini alisahau kwamba serikali yenyewe haijaachana na ajenda hizohizo. Tangu bajeti ya 2007/08 ianze kutekelezwa, haijapata nafuu wala upenyo wa kutolazimika kujitetea.

Lakini ukiacha Buzwagi, EPA na Richmond pembeni, bado serikali inateswa na kashfa ya ununuzi wa rada iliyomuangusha Chenge; sasa inateswa na kashfa ya mkataba wa ukodishaji kazi ya kupakua na kupakia makontena bandarini Dar es Salaam, waliyopewa kampuni ya TICTS.

Hili likiwa halijaiva wala kujulikana mwisho, sakata la uuzaji nyumba za serikali limeibuliwa upya. Ni hoja ya upinzani pia waliyoitoa tangu zama za awamu ya tatu. Haya yameiandisha serikali ya Kikwete isijue mwelekeo wake hasa ni upi.

Hakuna ubishi serikali inateswa na mawaa yaliyofanywa awamu iliyoitangulia. Ukiacha Buzwagi na Richmond, uchafu wote huu pamoja na uoza wa mantiki ya sheria ya maadili ya viongozi, ni madudu yaliyotengenezwa na wenyewe.

Ni bahati mbaya au nzuri kwamba harufu ya uoza imekuwa kubwa kiasi cha kutowezekana tena kuifunika kwa staili aliyoitumia Rais Benjamin Mkapa. Ugonjwa umekuwa ni mkubwa zaidi, madhara kwa taifa yameongezeka na kikubwa zaidi, watu wamechoka wakiwamo wabunge wa CCM, na sasa wanatetea umma.

Kwa kutambua ufisadi unaitafuna nchi, wabunge hawa waliokuwa wamesalimu amri, wanaunga mkono juhudi za upinzani. Kumbuka habari ya Richmond bungeni na kauli ya Anne Kilango Malecela (Same Magharibi - CCM) kwamba hatakaa kimya kuwaachia akina Zitto wakiichachafya serikali wakati wao pia wanawajibika kuisahihisha serikali! Aliapa kupambana na ufisadi.

Ndio maana serikali na wabunge wake wamejikuta kuelekezwa kwenye ajenda ambayo kwanza hawakuipanga wao, lakini pili, hawajui mwisho wake.

Hatari inayojidhihirisha wazi ni kwamba kwa sababu ya makosa ya awamu iliyotangulia, na kwa sababu ya kukosekana ujasiri miongoni mwa wabunge wa 2000-2005, sasa awamu ya nne imegandishwa:

Haipangi tena ajenda zake kulingana na Ilani ya Uchaguzi ya CCM. Kazi sasa imekuwa ni kusaka tiba kuhusu tuhuma za ufisadi zinazoikabili.

Hadi sasa hakuna anayeweza kusema kwa yakini serikali itatoka na nini kuhusu azimio la Bunge juu ya mchakato tata wa mkataba wa Richmond wa kufua megawati 100 za umeme wa dharura; pia haijulikani kitakachotoka katika uchunguzi unaofanywa na timu ya Rais inayofuatilia wahusika wa wizi wa Sh. 133 bilioni za EPA.

Ilivyo, sasa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, hana awazalo isipokuwa kusimamia utekelezaji wa azimio hilo kuhusu ripoti ya Richmond huku akijua, anasubiriwa kueleza namna serikali ilivyoshughulikia mapendekezo ya Kamati Teule iliyochunguza sakata hilo.

Kama msaidizi mkuu wa Rais, hana ujanja isipokuwa kujihusisha kwa karibu zaidi na kurudisha fedha serikalini zilizoibwa kutoka EPA pamoja na kusaka wahusika wa makampuni 22 yaliyochotewa fedha hizo.

Katika hali hii, serikali imeganda au inazidi kuandamwa na hoja ya ufisadi. Ni halali kusema kuwa si waziri mmoja mmoja au kwa ujumla wao wanaoweza kueleza njia ya kuweka kiporo ajenda hii.

Mwaka mzima wa fedha unakwisha (Julai 2007 - Juni 2008) serikali inajihusisha na ajenda moja tu ya wapinzani, ufisadi. Je, huko twendako italeta ajenda yake au itaendelea kuswagwa na wabunge wa upinzani japo wachache bungeni?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: