Serikali ilete umeme


editor's picture

Na editor - Imechapwa 01 November 2009

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

MAENEO ya nchi yanayotumia umeme wa gridi ya taifa yapo nusu giza. Kwa wiki tatu, nishati hii muhimu kwa maendeleo ya mwanadamu na mazingira yake, inatolewa kwa mgao.

Shirika husika – TANESCO – limeanzisha mgao kutokana na vyanzo vyake vya uzalishaji kupungua uwezo.

Sababu wanasema kiwango cha maji, yanayotegemewa zaidi kwa uzalishaji umeme, kimeshuka mno hivi karibuni hivyo kudhoofisha uwezo wa mitambo kufanya kazi vizuri.

Tunaambiwa kuna upungufu wa megawati 150 za umeme wa kutosheleza mahitaji halisi katika maeneo ambayo TANESCO wanayahudumia.

Wakati inakera TANESCO kuhudumia asilimia chini ya 15 tu ya nchi, inatisha wenyewe pamoja na serikali kuendelea kutoa maelezo kuhusu tatizo kama vile wameshtukizwa.

Mgao upo wakati menejimenti ilishaeleza matatizo yanayowakabili na hatua zinazotakiwa. Walitoa hata onyo kuwa iwapo hawatasaidiwa, “nchi itaingia gizani.”

Tunasema kukosekana umeme wa kutosha nchini ni fedheha kubwa. Inasikitisha kwamba TANESCO inashindwa kuhudumia wateja wake. Hata kabla ya mgao, umeme umekuwa ukipatikana kwa matatizo makubwa.

Menejimenti wanajua. Wizara inayosimamia shirika hili, wanayajua matatizo. Hatuna shaka yoyote Rais Jakaya Kikwete, anayajua.

Hoja yetu inaanzia hapa. Kwamba wananchi hawajaona uwajibikaji makini wa serikali katika suala hili. Ni maneno tu na ubabaishaji.

TANESCO ina uwezo wa kuhudumia asilimia ndogo mno ya Watanzania lakini hata hao hawahudumiwi ipasavyo. Ni malumbano tu.

Hakuna sababu ya viongozi wa serikali kuendelea kusema. Wananchi wanataka umeme ili watekeleze harakati za kujikomboa kiuchumi na kuisaidia nchi yao kuendelea.

Wamechoka maneno na maelezo; wanataka umeme tu. Nchi haiwezi kwenda kwa utamaduni walioanzisha viongozi wa kutunishiana misuli.

Hapana. Ni “Umeme; Umeme; Umeme.” Basi. Vingine vifuate. Lakini umeme haupatikani kimatarajio, basi zije hatua haraka.

Tunataka rais aitishe uchunguzi wa kitaalamu, ikibidi hata wa kimataifa. Watazame tatizo ni kitu gani hasa. Watafute chimbuko la utendaji usio tija wa TANESCO.

Akili zetu haziwezi kufikiria maendeleo iwapo hatuna umeme wa uhakika. Hakuna elimu bora, afya bora, maji safi na salama, makazi bora, chakula bora, makuzi bora ya watoto na vijana; bila ya umeme wa uhakika.

Hata serikali inajidanganya kuongeza kutunga sera na sheria na kutamka kaulimbiu kama “Kilimo Kwanza.”

Yote hayo – ambayo kufanikiwa kwake kunahitaji mipango na teknolojia – yatabaki ndoto bila ya umeme wa uhakika.

Sasa tukishindwa kuwezesha umeme wa uhakika na unaotosheleza mahitaji kuwepo nchini, tusikasirike wengine wanapozidi kuisukumiza Tanzania nchani mwa mataifa masikini.

0
No votes yet