Serikali imefumbua macho na masikio?


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 04 May 2011

Printer-friendly version

WATU 84 wamejeruhiwa na kulazwa katika hospitali mbalimbali jijini Kampala, nchini Uganda. Kisa cha majeraha yao ni fujo zilizotokea nchini humo wiki iliyopita.

Chanzo cha fujo ni hali ngumu ya uchumi. Bei za mafuta zimepanda na gharama ya maisha imefikia katika kiwango ambacho wananchi wa kawaida hawawezi kukimudu.

Hivyo basi, kiongozi wa chama cha upinzani – Forum for Democratic Change (FDC), Dk. Kizza Besigye, akaamua kuitisha maandamano ya wananchi kwenda kazini kwa miguu kwa vile hawamudu gharama ya nauli ya mabasi.

Haikuwa kwenda kazini pekee. Wiki mbili zilizopita, Besigye mwenyewe alitembea kwa miguu kutoka nyumbani kwake Kasangati kwenda katika Kanisa la Gayaza, umbali wa karibu kilometa nne. Maelfu ya wananchi wakamuunga mkono.

Kilichofuata ni mabomu, risasi na bakora kwa wanaandamanaji kwa madai kuwa  wamefanya maandamano bila ya kibali!

Lakini kimsingi yale hayakuwa maandamano, bali wananchi waliamua kwenda kwenye shughuli zao kwa miguu. Hawamudu nauli za magari.

Wakati hali ikiwa hivyo nchini Uganda, nchini Kenya waziri mkuu, Raila Odinga, ameeleza serikali yake inafikiria kupunguza ukubwa wa matumizi yake.

Kaskazini mwa nchi hiyo ambako hali ya hewa ni nusu jangwa, wananchi wamefikia hatua ya kula mizoga ya wanyama wanaokufa kutokana na kushindwa kumudu ununuzi wa chakula.

Kwa ujumla, hali ya kiuchumi katika ukanda huu wa Afrika Mashariki si nzuri. Tanzania inaonekana kumepoa kulinganisha na Kenya na Uganda, ingawa sidhani kama hali hii itakuwa ya kudumu.

Bei za mafuta zinazidi kupanda. Bei za vyakula katika masoko mbalimbali zinaendelea kupanda. Wananchi wa kawaida; wakulima na wafanyakazi wanateseka kwa vile mustakabali wao unaonekana haueleweki.

Kwa kawaida ya serikali ya Tanzania, kama bei ya mafuta itazidi kupanda katika soko la dunia, bei hiyo itapanda hapa nchini. Bila ya umakini, naona upo uwezekano wa bei ya mafuta kwa lita moja kufikia Sh 3,000 kabla ya mwisho wa mwaka huu.

Jambo la kujiuliza ni kuwa itakuwaje kwa mwananchi wa kawaida wakati hali itakapofika hapo?

Akizungumza na waandishi wa habari wiki mbili zilizopita, Rais Yoweri Museveni wa Uganda, alisema matatizo yanayoikumba nchi yake kwa sasa yanasababishwa na ongezeko la bei ya mafuta kwenye soko la kimataifa.

Ukifika wakati ambapo bei ya mafuta hapa nchini itafika Sh. 3000 kwa lita moja, serikali yetu ni wazi kuwa itasingizia ongezeko hilohilo katika soko la kimataifa.

Na sababu hii haijawahi kutosha popote pale.

Kwa mujibu wa takwimu zilizopo sasa, serikali hujipatia kiasi cha Sh. 539 kwa kila lita moja ya mafuta yanayouzwa nchini.

Wakati serikali ya Jamhuri ya Muungano  inachukua kiasi hicho cha fedha, serikali nchini Kenya, inachukua Sh. 30 (Sh 514 za Tanzania).

Hiki ni kiasi kikubwa sana cha fedha na serikali zingetaka zingeweza kusikiliza kilio cha waagizaji mafuta na kupunguza kodi.

Kama kodi hizi za serikali zitapunguza, bei za mafuta zitashuka na kushuka kwake kunaweza kushusha bei za vyakula na bidhaa nyingine.

Inawezekana serikali ikapoteza kodi, lakini wananchi watapata nafuu.

Sioni sababu ya serikali kusubiri hadi wananchi waanze fujo kama ilivyotokea nchini Uganda, Tunisia na Haiti ili ichukue hatua za mapema. Ni muhimu kuzuia mambo kabla hayajawa makubwa.

Kuna mambo mengine madogo ambayo ni ya msingi katika kuhakikisha nchi yetu haiingii katika matatizo na ni muhimu kwa serikali kuyafanya.

Kwa mfano, kama wananchi wataamua kutembea kwenda kazini kwa kukosa nauli, serikali haitakuwa na sababu ya kuingia na kupiga watu kwa kutumia dola; hata kama matembezi hayo yatakuwa yana maudhui au yameanzishwa na watu wa upinzani.

Mambo kama hayo ndiyo yanayoamsha hasira za wananchi dhidi ya serikali yao. Kama tunakumbuka vizuri, mgogoro wa Tunisia ulianza baada ya kijana mwanafunzi aliyekosa ajira alipojichoma moto baada ya serikali kuharibu biashara zake za kimachinga.

Lakini pia naona hiki ni kipindi ambacho serikali ni lazima ifanye mambo yake ikizingatia hali ya maisha ya wananchi wake. Kama kuna jambo linaweza kufanyika kupunguza ukali wa maisha, lifanyike pasi na uoga.

Matumizi makubwa ya fedha kwa mambo yasiyo na umuhimu katika kipindi kigumu kama hiki ni muhimu pia yakazuiwa. Mojawapo ya mambo ambayo yamesababisha hasira ya wananchi wa Uganda ni hatua ya serikali ya nchi hiyo kukamilisha ununuzi wa ndege ya kifahari kwa Museveni.

Katika nchi hiyo ambayo wananchi wanakosa nauli ya kupanda mabasi, wengine hawana uhakika wa kupata mlo hata mmoja kwa siku, rais ananunuliwaje ndege ya kifahari?

Haya ndiyo mambo ambayo ni lazima serikali iyaangalie kwa makini katika wakati huu ambapo bara la Afrika linapita katika wakati wa majaribu.

Mara zote mimi ni mfuasi mkubwa wa mabadiliko. Na mara nyingi nimekuwa nikisisimshwa na matukio ya kishujaa yaliyotokea Tunisia, Misri na huko Syria hivi sasa.

Lakini, siamini kuwa mabadiliko yoyote ya kiuongozi au kimamlaka ni lazima yaendana na fujo, uharibifu wa mali na upotevu wa maisha ya watu.

Lakini mpira uko kwa serikali. Ni yenyewe ndiyo mwisho wa siku inayoamua uchezweje. Ikiamua vema, mpira utachezwa salama. Lakini ikiamua vibaya, athari zinajulikana kwa vile ziko kila mahali.

Hilo ndilo ninalotaka kulikwepa.

0718 81 48 75
0
No votes yet