Serikali imejigeuza kondoo wa kafara


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 10 August 2011

Printer-friendly version
Tafakuri

BABA wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alipata kusema, “Ni lazima serikali iwatishe walarushwa. Alikuwa anasimulia kisa cha raia mmoja wa Ugiriki aliyekuwa anatamba mitaani kuwa ameiweka serikali yake mfukoni.

Alisema alimshughulikia mtu huyo na mwishowe alimfukuza nchini baada ya kuombwa sana na kiongozi mmoja wa dini. Uamuzi wa kumshughulikia Mgiriki huyo aliyetamba ameiweka serikali mfukoni ulilenga kuonyesha serikali ipo, haichezewi, ina nguvu na ina uwezo wa kutenda tena kwa makali ya kutosha.

Mwalimu alisema haya alipokuwa akielezea hali ya kuzidi kuyumba kwa serikali, wakati huo utawala wa awamu ya pili ukielekea ukingoni. Alikuwa akijenga hoja ya kupata viongozi wa awamu ya tatu, ambao wangekuwa wachapakazi, waadilifu na ambao watajua kwa hakika vyeo watakavyopewa ni dhamana na kwamba wakati wote watavitumia kutekeleza matakwa ya sheria, kanuni na taratibu za kuendesha nchi.

Nimekumbua maneno ya Nyerere baada ya kuona jeuri ya wamiliki wa vituo vya mafuta. Ni jeuri kweli kweli. Yaani ametokea mfanyabiashara mmoja ambaye ameshiba faida ya kuuza mafuta nchini kiasi cha kuanza kuipa serikali onyo (ultimatum) ya saa 24 kwamba kama haitafanya hivi na vile, itakiona. Mfanyabiasha ambaye wala si raia ana nguvu usipime!

Serikali kupitia wizara ya nishati na madini na Mamlaka ya Udhibiti Huduma za Nishati na Maji (Ewura) wamesema hawakubali kutishwa na mfanyabiashara huyo na kwamba anachunguzwa! Eti anachunguzwa!

Yaani mtu anatoa matamshi makali na ya kuitisha serikali tena kuhusu sekta ya nishati akitetea uasi na mgomo kwenye sekta ya nishati ya petroli ili tu serikali iufyate na kuwaacha waendee kuwakamua wananchi kama hawana mtetezi, bado hatujasikia akiwa ameitwa polisi kujieleza na kusema kwa kina matamshi yake yalilenga nini. Hatujamuona akitiwa msukosuko wa kutosha ili ajue kuwa kuna serikali. Ni kwa nini taifa hili kimefikia hapa lakini?

Tumezoea kusikia viongozi wa kisiasa hasa wa kambi ya upinzani wakikamatwa kwa mambo ya tuhuma za ovyo sana; eti kazidisha muda wa kuhutubia mkutano wa hadhara kwa  dakika 15, eti wamefanya kusanyiko haramu! Eti wameingia chumba cha maiti kijinai. Tuhuma za ovyo kweli kweli.

Ukitazama kwa kina tuhuma hizi dhidi ya wanasiasa utagundua kitu kimoja kiko wazi, serikali haitaki ipewe changamoto, haitaki wananchi waelezwe na wajengwe kutambua kuna madudu yanafanywa na viongozi wao, kwa hiyo vyombo vya usalama ama vimetumwa au vimejituma kufunika sauti huru za kuwaamsha wananchi usingizini. Hatari kweli kweli!

Wakati mambo hayo ya ovyo yakiendelea wanaibuka watu wenye kiburi na jeuri ya fedha wanaipa serikali saa 24 kufanya maamuzi kama watakavyo wao, vinginevyo serikali na taifa litatiwa adabu. Kweli bwana, serikali na wananchi wametiwa adabu kwa kuwa katika kipindi cha saa 24 serikali haikutii maelekezo ya wenye jeuri ya fedha.

Tangu Ewura itangaze bei mpya elekezi za nishati ya mafuta ya petroli, dizeli na taa; wafanyabiashara wa mafuta wameitia adabu serikali na wananchi kwa ujumla wao. Wameamua kukataa kuuza bidhaa hiyo kwa bei elekeki ya Ewura. Walichofanya ni kuonyesha tu kwenye mabango kuna bei mpya kwa mujibu wa bei elekezi ya Ewura, lakini hawauzi bidhaa hiyo. Wanadai eti mafuta yamewaishia.

Ni kweli tumemefikishwa mahali tumekuwa taifa la kondoo; na tuna ukondoo mbaya na wa hatari mno. Haya wanayofanya wafanyabiashara ya mafuta yanaweza tu kufanywa katika nchi inayoongozwa na serikali legelege. Serikali iliyowekwa mfukoni na wafanyabiashara.

Hoja ya serikali legelege imeimbwa mno katika bunge hili, lakini imepingwa na baadhi ya watu wakiamini kuwa ni matusi na kauli za kuudhi. Bila shaka, wanaopinga hoja hii wanasumbuliwa na kukosa kumbukumbu.

Mwalimu Nyerere alisema wazi “serikali dhaifu au legelege hazikusanyi kodi,” ndiyo maana wafanyabiashara hawa wa mafuta wanashangaa ghafla serikali legelege waliozoea ambayo haikusanyi kodi, ambayo haiwabani wafanyabiashara inaamka na kutaka kuwabana. Wanaikemea kwa kuwa wanajua kuwa hiyo si hulka yake.

Ndiyo maana hata baada ya ‘matusi’ ya wafanyabiashara hawa, kuitisha kikao cha pamoja na kuweka mikakati ya kuigomea serikali kuhusu bei mpya ya mafuta, hakuna wanachofanywa.

Ewura inasema ndani ya nchi kuna shehena ya kutosha ya mafuta ya petroli (lita milioni 41.6) inayotosheleza matumizi ya siku 48, dizeli (lita milioni 30) ikitosheleza matumizi ya siku 30 na mafuta ya taa (lita milioni 41.2) ikitosheleza siku 67; lakini kwa mshangao wa wengi vitu vingi vya mafuta hasa jijini Dar es Salaam vimeendelea kukaidi maamuzi ya Ewura ya kupunguza bei kwa kujifanya hawana nishati hiyo.

Uchunguzi uliofanywa na vyombo vya habari tangu kuanza kwa bei hiyo mpya ya nishati ya petroli, dizeli na mafuta ya taa Jumatano ya 3 Agosti 2011, umeonyesha pasi na shaka wafanyabiashara wa mafuta kwa maneno na vitendo halisi wanaitikisa serikali.

Kwa bahati mbaya, hatuoni hatua zozote zikielekezwa kwa wale walioko kwenye mgomo baridi. Ni vigumu kusema serikali ni makini hasa inapochezewa na wafanyabiashara kama hawa wa mafuta, lakini wakati huo huo tukisikia juhudi na mbinu mbaya za serikali hiyo hiyo kutaka kuwadhibiti wananchi wake kama vile alivyodai Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Frederick Werema, kwamba sheria ya kuandamana itafanyiwa marekebisho.

Werema anataka kujenga hoja dhaifu na muflisi kwamba shida za wananchi wa nchi hii ni maandamano, ni uhuru wao wa kukusanyika, ni uhuru wao wa kujumuika katika vikundi watakavyo.

Lakini wafanyabiashara wanaofanya watakalo, kujinufaisha na rasilimali zetu, kuamua ni kodi ipi walipe na ipi wasilipe, kuitisha serikali na kwa uhakika kuiamrisha, kwake si jambo la kumsumbua akili.

Tunapoona hali kama hii, yaani kukwama kwa serikali kama ambavyo imekwama kabisa katika nishati kuanzia kwenye umeme na sasa petroli, dizeli na mafuta ya taa, nashindwa kukwepa kukubaliana na Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, kwamba serikali imechoka.

Sasa ni wakati wa kujiuliza: Bila serikali kujiangalia sasa na kujisahihisha, hakika huko tuendako ni kugumu na kubaya zaidi. Ni jambo la hatari sana kama wafanyabiasha kwa umoja wao au mmoja mmoja anaweza kuwa na jeuri ama ya fedha, au kiburi tu cha kufanikiwa anaitisha serikali na kufanya maamuzi ambayo yanahujumu taifa na yeye aonekane tu kuwa ni sawa.

Serikali sasa inahitaji kuamka na kujitafakari upya kama kweli ipo kuwatumikia wananchi ama ni kweli imemezwa na wafanyabiashara kama hawa.

0
No votes yet