Serikali imekataa kuthamini wafugaji


Navaya ole Ndaskoi's picture

Na Navaya ole Ndaskoi - Imechapwa 30 May 2012

Printer-friendly version

MAPIGANO kati ya wafugaji na wakulima yametokea tena na safari hii ni wilayani Rufiji, mkoa wa Pwani.

Kama ilivyo ada kila mapigano yakitokea hugharimu maisha ya watu na uharibifu mkubwa wa mali na mifugo.

Taarifa zisizorasmi zinasema mapigano hayo yameshagharimu maisha ya watu watano.

Vilevile, umefanyika uharibifu mkubwa wa mali na mifugo mingi imecharangwa mapanga. Damu ya watu pamoja na mifugo inazidi kuiweka pabaya serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ilivyoshindwa kutenga maeneo ya kilimo na malisho.

Bahati mbaya, kila mapigano yakitokea wafugaji ndio hushutumiwa kana kwamba wao ni nuksi katika nchi hii. Hata wakati wa hotuba ya uzinduzi wa Bunge jipya 30 Desemba 2005 mjini Dodoma, Rais Jakaya Kikwete aliweka msimamo mkali dhidi ya wafugaji.

“Mheshimiwa Spika, tutachukua hatua kuboresha ufugaji… tunalazimika kuachana na ufugaji wa kuhamahama ambao unaifanya nchi nzima kuwa malisho… ng’ombe hanenepi mfugaji hanenepi… hatutaweza kuendelea na ufugaji wa jinsi hii katika karne ya ishirini na moja,” alisema huku wabunge wakimshangilia.

Matamshi hayo ya rais yalichochea chuki dhidi ya wafugaji. Watendaji wa serikali pamoja na viongozi waandamizi wa kisiasa wakapata kizingizio cha kuvunja sheria.

Februari 2006 mgawo mkali wa umeme ulipotikisa nchi hasa miji kama Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Mbeya na mingineyo, serikali ya CCM na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wakadai kuwa sababu ya mgawo huo ni kushuka kwa kiwango cha kutisha cha kina cha maji katika bwawa la Mtera, mkoani Dodoma.

Rais Kikwete akapigilia msumari akisema, “…ni bora wafugaji wachache wakasirike, lakini tulinde maisha ya kizazi kijacho.”

Tarehe 18 Mei 2006, serikali ilianza kuwavamia kikatili wafugaji Ihefu, wilayani Mbarali, Mbeya. Polisi, askari wa wanyamapori, wakiwa na silaha nzito wakawaondoa kwa mabavu wafugaji wote Mbarali pamoja na ng’ombe zaidi ya 300,000 bila kuhesabu mbuzi, kondoo na punda.

Modestus Kilufi, Mbunge wa Mbarali, alipata kumdokeza mwandishi wa makala hii kuwa wafugaji walilazimishwa kulipa faini kiasi cha Sh. 10,000 kwa kila ng’ombe na hivyo waporaji hao wa serikali wakajipatia zaidi ya Sh. 3 bilioni kwa dhuluma.

Mwenyekiti wa Baraza la Wafugaji Mbarali, Sangala Matayani anasema wafugaji wa wilaya ya Mbarali walipata hasara ya zaidi ya Sh. 100 bilioni.

Hii ni kutokana na mifugo yao kuporwa na sehemu kubwa ya mifugo hiyo kufa kwenye mazizi ya serikali kama lile lililokuwa pale Igawa; lakini pia walipokuwa wanapelekwa mikoa ya Lindi, Mtwara, Rukwa na Pwani.

Sangala alilazimishwa kulipa Sh.10,708,000 na kupewa stakabadhi Na 000045927. Siku hiyohiyo kaka yake, Kochocho Matayani alitozwa Sh. 10,485,000 na kupewa stakabadhi Na 000045928.

Kochocho alitozwa tena Sh. 4,570,000 na kupewa stakabadhi Na 000045586 Desemba 28, 2006 na kisha akatozwa Sh. 3,490,000 Machi 1, 2007 na kupewa stakabadhi Na 000046218.

Mbali na kuporwa mifugo na fedha taslimu, wafugaji Mbarali walipoteza ardhi yao yenye rutuba. Toka mwanzo mashirika ya kuhifadhi mazingira (WWF) na hifadhi ya taifa (TANAPA) yalidhamiria wafugaji wafukuzwe toka Bonde la Usangu ili kupanua Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

Tarehe 15 Desemba 2007 Rais Kikwete alisaini, bila kusita, sheria ya kupanua hifadhi hiyo kutoka kilomita za mraba 10,300 hadi kilomita za mraba 20,226.

Mashirika ya haki za binadamu yalifanikiwa kuwashawishi wabunge 58 kuishinikiza serikali itoe maelezo ya kina kuhusu dhuluma hii. Tarehe 27 Aprili 2007 serikali ilitangaza bungeni kuwa Tume ya Jaji Othman Chande itachunguza madai ya wafugaji.

Baada ya uchunguzi Chande alimkabithi Kikwete taarifa tarehe 6 Juni 2007. Lakini sasa ni karibu miaka mitano Rais Kikwete hajaweka wazi taarifa hiyo.

Aliyeongoza tume, Jaji Chande ameteuliwa na Rais Kikwete kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania. Vipi wafugaji? Wao wametumbukizwa katika dimbwi la majanga ikiwa ni pamoja na kutangatanga huku na kule bila kuthaminiwa na serikali yao.

Ili kunusuru maisha na mali zao, wafugaji wengi walikimbilia wilaya za mikoa ya Rukwa, Morogoro, Lindi, Pwani. Hivyo ndivyo wafugaji wengi walivyofika Rufiji.

Sasa kama rais na wasaidizi wake wanawakejeli wafugaji na kufumbia macho dhuluma hii, wenyeji wa Rufiji ambako wafugaji walikimbilia watakuwa tayari kuwapokea “wakimbizi” hawa?

Profesa Idris Mtulia, wakati akiwa Mbunge wa Rufiji, alipata kuongea kizushi mara kadhaa hadharani dhidi ya wafugaji.

Tarehe 15 Aprili 2010, alisimama na kuliambia bunge “…hivi karibuni, wakati wa kazi ya uhamishaji mifugo, wilaya ilitarajia kupokea ng’ombe 50, 000 tu lakini badala yake wameingia ng’ombe 300,000.”

Naibu Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk. James Wanyancha, alijibu kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji ilikamilisha kazi ya kuhesabu mifugo katika vijiji 25 vyenye mifugo mingi.

Dk Wanyancha alisema katika kazi hiyo ilibainika kuwa wilaya hiyo ina ng’ombe 124, 058, mbuzi 17, 279, kondoo 12, 479 na punda 329.

Sasa Prof. Mtulia alitoa wapi takwimu zilizokinzana na zile za Wizara ya Mifugo na Uvuvi? Kama Prof. Mtulia anawaona ng’ombe 124,058 Rufiji kuwa ni zaidi ya 300,000, kwanini wenyeji wa Rufiji wenye elimu ndogo wasiwakabili wafugaji?

Vilevile Mtulia aliwahi kusema bungeni, “…sehemu yenye rutuba ibaki kuwa ya kilimo cha chakula na biashara na sehemu ya ardhi, semi-arid, yaani kame, iwe sehemu ya wafugaji.” Aliongeza kuwa lengo ni kutekeleza kauli mbiu ya Kilimo Kwanza.

Sasa kama profesa anafikiri kuwa kilimo kinahitaji ardhi yenye rutuba na mifugo inastahili kufugwa jangwani, unategemea nini kutoka kwa wasio na uelewa mkubwa juu ya umuhimu wa mifugo kwa uchumi wa nchi na lishe ya binadamu?

Kuna taarifa kwamba baraza la madiwani Wilaya ya Rufiji linajiandaa kuwaondoa wafugaji ifikapo tarehe 30 Juni mwaka huu.

Viongozi wakuu wa serikali wamekaa kimya. Je, wanasubiri taifa hili litumbukie katika mauaji ya wenyewe kwa wenyewe?

Mwandishi ni mwanazuoni na mchambuzi wa migogoro ya ardhi. Anapatikana kwa simu: 0754 453 192
0
No votes yet